Na Happiness Shayo, JamhuriMedia, Makete
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewaasa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete Mkoani Njombe kuacha kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa huku akiwataka kuyatumia maeneo hayo katika kujiongezea kipato ili kuwa na uhifadhi endelevu.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua rasmi semina ya kuwajengea uwezo wadau wa uhifadhi kuhusu uanzishaji wa Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMAs) na mikakati ya kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete leo Aprili 15,2025.

“Wilaya hii inapakana na maeneo yaliyohifadhiwa kama vile Hifadhi ya Taifa Kitulo, Pori la Akiba la Mpanga- Kipengele na misitu ya hifadhi ya Chimala, Maguli inasimamiwa na TFS na Msitu wa Living Stone na Ipuji unaosimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Makete na inapitiwa na ushoroba wa Ndukunduku unaounganisha Hifadhi ya Taifa Kitulo na Pori la Akiba Mpanga Kipengele hivyo ni muhimu kuyatunza na kuyalinda, tusiweke mashamba au makazi kwenye maeneo haya” amesisitiza Mhe. Chana.
Amefafanua kuwa kupitia mafunzo hayo wananchi watajifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu, kupambana na masuala ya moto pamoja na uanzishaji wa Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori.
Aidha, Mhe. Chana ameweka bayana kuwa katika kutatua changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu, Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za utatuzi ikiwemo kuendesha doria za ushirikiano wa taasisi za TAWA, TANAPA na Wilaya ya MAKETE; kutumia teknolojia katika udhibiti wa wanyamapori ikiwemo ndege nyuki, mikanda maalum ya mawasiliano (GPS Satellite Collars), mabomu baridi, kutoa semina ya kujenga uelewa kwa Maafisa Wanyamapori 122 kutoka Halmashauri za Wilaya mbalimbali nchini ikiwemo za Mkoa wa Njombe.

Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii (anayeshughulikia Maliasili), CP Benedict Wakulyamba amewahasisha wananchi wa Makete kuanzisha eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori kutokana na uwepo wa Ushoroba wa Ndukunduku katika wilaya ya hiyo.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 Wizara imepanga kuendelea kujenga uwezo kwa wadau mbalimbali nchini kuhusu usimamizi wa WMA, Shoroba na mikakati ya kudhibiti migongano baina ya binadamu wa wanyamapori.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Makete, Mhe. Kissa Kasongwa ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuandaa mafunzo hayo huku akisisitiza kuwa Makete ni eneo zuri la Utalii na uhifadhi kutokana na misitu yake.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Makamishna Wasaidizi wa Kanda kutoka TAWA, TANAPA na TFS, Wataalam kutoka Wizara ya Maliasili, Utalii, Wadau mbalimbali wa uhifadhi kutoka kata za wilaya ya Makete, Viongozi wa dini na Serikali kutoka Wilaya ya Makete.


