Na Happiness Shayo, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Sekretarieti ya Mkataba wa Kikanda wa Lusaka (Lusaka Agreement Taskforce-LATF) wa kukabiliana na ujangili na biashara haramu ya wanyamapori na mazao ya misitu unaovuka mipaka ya nchi.
Kikao hicho kimefanyika leo Februari 17, 2025 jijini Dar es Salaam ambapo ujumbe wa Sekretarieti ya Mkataba huo kutokea Makao Makuu yaliyopo jijini Nairobi nchini Kenya uliongozwa na Mkurugenzi wa LATF, Bw. Edward Phiri.

Kama mwanachama hai wa Mkataba huu, Tanzania imekuwa ikinufaika katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na operesheni zaidi ya 15 dhidi ya biashara haramu ya wanyamapori na mazao ya misitu. zilizoratibiwa na Sekretarieti ya Mkataba huo, ambapo watuhumiwa kadhaa walikamatwa wakiwa na nyara mbalimbali kinyume cha sheriaā€¯ alisema Mhe. Chana.
Pia, amesema Tanzania inatambua mchango wa Mkataba wa Lusaka katika kuwajengea uwezo Maafisa wa Himasheria na kusisitiza kwamba Tanzania chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Wizara ya Maliasili na Utalii inatumia kila mbinu kuhakikisha rasilimali za wanyamapori nchini zinalindwa kwa kutekeleza taratibu za kisheria za ndani, kikanda na kimataifa dhidi ya ujangili na biashara ya wanyamapori na mazao ya misitu.
Aidha, amesema kama nchi mwanachama hai wa Mkataba wa Lusaka, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kutekeleza maamuzi ya Baraza la Uongozi la Mkataba ambapo Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Baraza la 14 la Uongozi utakaofanyika mwezi Mei 2025.

Naye, Mkurugenzi wa LATF, Bw. Edward Phiri ameshukuru kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 14 wa Baraza la Uongozi wa nchi wanachama (Governing Council) wa Makataba wa Lusaka utakaofanyika mwezi Mei, 2025 ambapo katika Mkutano huo Waziri wa Maliasili anatarajiwa kupokea nafasi ya Rais wa Baraza la Uongozi kutoka kwa Waziri wa Maliasili Kenya ambaye anamaliza muda wake.
Kikao hicho kimehudhuriwa na baadhi ya Watendaji kutoka Idara ya Wanyamapori, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).




