WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk Pindi Chana amekabidhi malori matano na mitambo mitano mitano yenye thamani ya Sh bilioni 6.4 za Kitanzania viliyonunuliwa kupitia mradi wa Dharura kwa Uhifadhi na Utalii Tanzania kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW).
Akizungumza katika makabidhiano hayo, leo Desemba 2, 2024 katika ukumbi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (Mpingo House) jijini Dar es Salaam, Chana amesema vifaa hivyo vitaenda kusaidia shughuli za uhifadhi na kuboresha miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, Nyerere na Pori la Akiba Selous kupunguza athari zilizosababishwa na janga la UVIKO-19 kwenye utalii na uhifadhi.
Kufuatia hatua hiyo, Chana aliiagiza Bodi na Wakuu wa Mashirika ya Tanapa na Tawa kuhakikisha vitendea kazi hivyo vinatumika kufanya kazi zilizokusudiwa za uhifadhi wa maliasili na utalii na kutunzwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za matumizi ya vifaa vya serikali.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Tanapa, Jenerali Msaafu George Waitara aliipongeza Serikali ya Ujerumani kwa kuendelea kusaidia uhifadhi nchini Tanzania hasa katika miradi ya dharura.
“Msaada huu wa dharura umetuwezesha kuvuka kipindi cha dharura cha UVIKO- 19 kwa kazi za uhifadhi kuendelea bila kuyumba kwenye mifumo ya kiikolojia, kutumika kuboresha na kuimarisha juhudi za uhifadhi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesisitiza.
Mkurugenzi Mkazi wa Frankfurt Zoological Society (FZS), Dk Ezekiel Dembe amesema kuwa Frankfurt Zoological Society imekuwa Tanzania kwa zaidi ya miaka 65 na kwamba inajivumia kufanya kazi na Wizara ya Maliasili na Utalii, Tanapa, Tawa na wadau wengine kwa sababu wamekuwa wakitekeleza makubaliano ya mikataba ipasavyo.