Shirikisho la soka barani Afrika CAF limetangaza droo ya michuano ya CHAN inayoandaliwa mwaka huu kwa ushirikiano wa nchi ya Kenya,Tanzania na Uganda.
Droo hiI ilitangazwa siku moja tu baada ya michuano hiyo kuahirishwa kutoka mwezi Februari hadi Agosti mwaka huu kwa ajili ya kutoa fursa kwa nchi wenyeji kukamilisha maandalizi .
Viongozi wa soka,wadau,wachezaji na mashabiki wametoa kauli zao kuhusu droo hiyo pamoja na kuzungumzia hatua ya kuahirishwa kwa mashindnao hayo.
Rais wa shirikisho la soka nchini Tanzania Wallace Karia ameunga mkono hatua ya kuahirishwa kwa michuano akisema itatoa fursa kwa ligi kuu ya Tanzania iliyosimamishwa awali ili kuipisha CHAN kufikia Agosti.
Kuhusu droo ya michuano hiyo,Wallace amesema Taifa stars ya Tanzania haiogopi timu yoyote kutoka Afrika akipuuza madai kuwa Tanzania imepewa kundi rahisi.
Rais huyo wa TFF amesema Tanzania ina uwezo wa kuwabwaga timu vigogo na kufika hatua za nusu fainali ama hata kunyakua ubingwa wa mashindano hayo kwa mara ya kwanza katika historia.
Rais wa klabu ya Yanga nchini Tanzania aliyehudhuria droo hiyo Said Hersi amesema umewadia wakati wa timu za Afrika mashariki kumaliza utawala wa timu za Afrika Magharibi katika soka la Afrika.
Amesema ana Imani Tanzania itatoboa hatua ya makundi kwa urahisi.
Rais wa Soka nchini Kenya Hussein Mohamed ametofautiana na mashabiki wa Kenya waliosisitiza kuwa Kenya imejikuta katika kundi gumu dhidi ya Morocco,Jamhuri ya demokrasi ya Congo,Zambia na Angola akiahidi kuwa Kenya itafaulu hatua ya makundi kwa maandalizi bora.
Mchezaji wa Harambee Stars ya Kenya Keneth Muguna amefurahishwa na kuahirishwa kwa michuano hiyo akisema itawapa fursa kujenga kikosi thabiti pamoja na kumpa kocha mpya Francis Kimanzi aliyejiunga nao hivi karibuni muda wa kupanga kikosi bora.
Mfungaji wa pili bora katika timu ya Taifa Stars Mrisho Ngassa, amesema michuano hii itatoa jukwaa kwa wachezaji chipukizi wanaofanya vyema katika timu ya Tanzania kuonekana na mawakala wa kimataifa wa soka hivyo kuwafungulia soka katika vilabu vya ulaya.
Waziri wa michezo nchini Kenya Salim Mvurya upande wake amekanusha uvumi wa kuwa Kenya ndio sababu ya CHAN Kuahirishwa akisisitiza kuwa ilikamilisha ukarabati na mikakati yote iliyotakiwa na CAF kwa michuano hiyo.