Na Isri Mohamed

Mwanamuziki mkongwe nchini Uganda, Jose Chameleone anatarajiwa kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kongosho katika Hospitali ya Allina Health Mercy huko Coon Rapids, Minnesota iliyopo nchini Marekani, ndani ya saa 12 zijazo.

Gwiji huyo wa muziki aliyetamba zaidi kwa nyimbo zake kama Jamila na Mama Rhoda, amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kongosho kwa muda mrefu, ambao unatajwa kusababishwa na matumizi yake ya pombe kupita kiasi.

Chameleone alifikishwa hospitali kwa mara ya kwanza Desemba 2024, baada ya kupata maumivu makali ya tumbo, ambapo hali yake iilizidi kuwa mbaya hadi kufikia hatua ya madaktari kumweka chini ya uangalizi maalum kwa siku 11.

Wataalamu wa matibabu nchini uganda walishauri kwamba anahitaji matibabu maalum na haraka nje ya nchi ili kuzuia madhara makubwa yanayoweza kumpata.

Ndipo aliposafirishwa kwenda Marekani, alipolazwa akiendelea kupatiwa huduma.

Kwa kipindi chote alichougua kaka yake na mwanamuziki mwenzake, Weasel Manizo, ndio wamekuwa wakimuuguza na kuwa nae karibu.