TABORA

Na Moshy Kiyungi

Eti mmoja wa wanamuziki mashuhuri Afrika Mashariki, Jose Chameleon, hutumia nguvu za giza kujiimarisha kiutajiri na umaarufu.

Tuhuma hizi nzito zinaelekezwa kwa mkali wa muziki wa ragga na raia wa Uganda, mtu wa kwanza kuzitoa akiwa ni Badman Denzo.

Badman, msanii aliyewahi kutamba na kibao cha ‘Big Mouth By Far’, anadai kwamba umaarufu wa Chameleon barani Afrika unatokana na ‘unyunyiziaji wa ndumba’ huku akidai kuwa: “Husafiri mara kwa mara kwenda Tanzania kukutana na waganga wake.”

Katika mahojiano na kituo kimoja cha runinga nchini Uganda, Badman anadai kumkuta Chameleon jijini Dar es Salaam akisaka ndumba.

Hata hivyo, Chameleon, anazipuuza tuhuma hizo akisema msingi wa mafanikio yake ni jitihada binafsi, mengine ni kuchafuliana majina katika soko la muziki.

“Mimi ni Mkristo, si rafiki wa shetani. Kwa hiyo kwangu uchawi hauna dili,” anasema.

Chameleon anaaminika kuwa tajiri zaidi miongoni mwa wanamuziki wa Uganda, akikadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Sh bilioni 1.5 za Tanzania; na zaidi ya dola za Marekani milioni 5.

Mwaka 2013 alitajwa kuwa miongoni mwa wasanii sita matajiri Afrika.

Utajiri wake ni nyumba za kupangisha (apartments) ziitwazo Daniella Villas jijini Kampala, nyingine ipo Arizona, Marekani, jengo zuri katikati ya Jiji la Kigali, Rwanda pamoja na jumba la kifahari kwenye vilima vya Sekulu hapo hapo Kampala.

Pia anamiliki studio, ufukwe wa Coco Beach uliopo mwambao wa Ziwa Victoria, barabara ya Entebbe, mikataba minono na kampuni kadhaa za Afrika na katika kuthibitisha kauli yake kuwa ‘muziki unalipa’, Joseph Mayanja a.k.a Chameleon, anamiliki magari kadhaa ya kifahari kama Cadillac Escalade, BMW, Premio, Toyota Ipsum, Land Cruiser VX na Mercedes Benz la bei kubwa.

Chameleon alizaliwa mwaka 1976 na kupewa jina la Joseph Mayanja. Alianza muziki mwaka 1996 akiwa ‘DJ’ katika ukumbi wa Missouri, Kampala.

Mmoja miongoni mwa nyimbo zake za kwanza ni ‘Bageya’, aliomshirikisha Redsan wa Kenya.

Wimbo wa ‘Kipepeo’ unatajwa kama ndio uliomtambulisha Chameleon kama msanii wa kiwango cha juu Afrika Mashariki.

Vibao vya nguvu vya ‘Jamila’, ‘Bei Kali’ na ‘Mama Rhoda’ vilimuimarisha kimuziki na kutikisa soka la Afrika, kabla hajafyatua ‘Wale Wale’, ‘Nkoleki’, ‘Vale Vale’, ‘Dorotia’, ‘Tubonge’, ‘Agatako’ na ‘Pam Pam’.

Tayari mwamba huyu amekwisha kufyatua zaidi ya albamu 12 tangu mwaka 1999 alipotoa albamu ya kwanza nchini Kenya.

Awali, alishirikiana kikazi na Bebe Cool kabla ya kupishana na kuibua upinzani mbaya kuwahi kutokea miongoni mwa wasanii Afrika Mashariki.

Chameleon anatumia mitindo mchanganyiko, akichanganya utamaduni wa Kiganda, rhumba ya Afrika ya Kati, zouk na ragga.

Kwa upande wa kijamii, yeye ni mwanachama wa muungano wa wanamuziki unaosaidia kuondoa umaskini na mapambano dhidi ya ukimwi.

Mbali na Afrika Mashariki, kazi za Chameleon zimetikisa na kukubalika hata ughaibuni, akifanya maonyesho ya kuvutia Marekani, Uingereza, Sweden na mataifa kadhaa ya Ulaya.

Onyesho lililohudhuriwa na mashabiki wa muziki zaidi ya 40,000 lililofahamika kama ‘Tubonge Live’ katika Uwanja wa Kriketi wa Lugogo, ndilo lililoweka rekodi ya kuhudhuriwa na watu wengi zaidi na kumpa umaarufu mkubwa.

Awali, Bebe Cool na Navio walijitangaza kuwa ndio matajiri zaidi Uganda, kabla ya Chameleon kuweka wazi mali zake.

Desemba 2014, alifanya onyesho kubwa kwa kiingilio cha Sh milioni moja za Uganda, na kununua viatu kwa dola 12,000 za Marekani huku akijigamba kwa kusema ameizawadia miguu yake kama sehemu ya kuirudishia shukrani kwa kusimama naye na kumuwezesha kufika alipo.

“Haya kamwe si majivuno, bali ni njia ya kumshukuru Mungu kwa kunijalia ukwasi huu,” anasema.

Katika kutetea uamuzi wake wa kununua viatu kwa fedha nyingi, Chameleon, aliwakumbusha mashabiki wake kuwa miaka kadhaa iliyopita nusura apate ulemavu wa kudumu baada ya kupata ajali.

Ikumbukwe kwamba Chameleon alijirusha kutoka ghorofa ya tatu katika Hoteli ya Impala mjini Arusha na kuvunjika miguu yote.

Bado haijafahamika sababu zilizomfanya kujirusha kutoka ghorofani.

Pamoja na kuonekana kama jeuri na mtata mbele ya mashabiki, Chameleon ni baba wa familia ya mke na watato wanne; wa kwanza, Ayla Mayanja Onsea, alizaa na Dorotia kabla ya kufunga ndoa na Daniella na kupata watoto watatu; Abba Marcas Mayanja, Alfa Mayanja na Alba Shyne Mayanja.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada mkubwa wa mitandao.

Mwandaaji anapatikana kwa namba: 0713331200, 0784331200 na 0767331200.