Wapo wanasiasa nchini ambao wamezua mtindo wa kuhama kutoka chama kimoja cha siasa na kujiunga na chama kingine. Na wakati mwingine wamekuwa wakihama kwenda chama kingine, lakini baadaye wakirudi katika chama cha awali.
Sababu zinazoelezwa kuhusiana na hatua hiyo ni za kisiasa, kijamii na kiuchumi zikijikita katika hoja kama vile kukerwa na utendaji dhaifu wa shughuli za chama na ndipo wanapohama.
Wakati mwingine wanapendezwa na utekelezaji mzuri wa sera za chama wanachohamia. Inakuwa sababu ya kwenda huko.
Kila chama kina itikadi, falsafa, kanuni na taratibu zake kwa wanasiasa, ambazo kwazo huvuta pia wanasiasa wengine kujumuika nao.
Chama makini cha siasa kina miiko na mizungu yake katika kueleza imani, sera na siasa zake kwa watu mbalimbali. Chama cha siasa hakina tabia ya ‘ukumi’ (ushirika) na chama kingine katika kuongoza na kutawala nchi.
Kama ‘ukumi’ ukitokea, basi tambua kuna dalili ya kutokea ufa katika usalama na umoja wa kitaifa. Daima chama cha siasa hupenda kuongoza peke yake.
Napenda kusikia na kuona chama kinamfunda na kumuoka mwanasiasa wake ndani ya tanuri la siasa na kumuivisha barabara.
Aidha, kumnywesha ‘maji ya imani’ yaani itikadi, kumvisha joho la kinga (demokrasia), kumlea na kumtunza. Na hapa chama kinakuwa na nafasi nzuri ya kujisifu na kujinadi mbele ya watu kwamba kinatekeleza wajibu wake.
Wajibu kama huo na weledi wa kisiasa hakiyumbi au kuwa kama doli la kuchezewa na kila binti mdogo anayejifunzia malezi ya mtoto.
Chama si kama gari la abiria kupakia kila msafiri mwenye nauli. Si taksi kila mwanasiasa ni abiria wake.
Chama kinapohamwa na mwanasiasa wake, basi ifahamike ipo kasoro ndani yake au kasoro kwa mwanasiasa binafsi.
Ni kasoro kwa chama kinaposhindwa kuenzi itikadi na falsafa yake na ni kasoro pia kwa mwanasiasa kutokata kiu ya itikadi ‘aliyonyeshwa’ na kuvaa joho linalombana au linalompwaya kwa sababu hapendezi na hafanani na wenzake katika safari ya kwenda kushika dola.
Ni dhahiri katika hali kama hiyo pana ombwe la kisiasa ndani ya chama. Yaani hapana siasa safi; uhuru na ukweli; na hapana uongozi bora, wajibu na haki.
Katika madhila kama haya ni nadra kupatikana demokrasia ya kweli na ni wazi mwanasiasa makini atahama chama.
Aidha, katika ombwe hili pia kuna ubinafsi. Huu una mikono yenye matamvua ya choyo na dhuluma, wizi na ufisadi, ubaguzi na upendeleo na ung’ang’anizi wa madaraka.
Matendo kama haya yanapokubaliwa ndani ya chama ni tiketi ya mwanasiasa mzalendo kuhama chama.
Ombwe kama hilo hutengeneza malumbano kati ya chama na mwanasiasa kuhusu sababu za kuhama. Chama huamini mwanasiasa wake amerubuniwa na kuhongwa. Mwanasiasa ‘hujikosha’, hizo si sababu za kweli. Ni ufitini na udhalilishaji kisiasa dhidi yake.
Leo wananchi tunashuhudia uhamiaji huu unavyosindikizwa na sababu za utoaji hongo, viongozi kurubuniwa, viongozi kuwajibika na utekelezaji mzuri wa sera n.k. Lakini bado wananchi hatujapata ushahidi halisi na kweli kuthibitisha sababu hizo.
Ni jambo jema chama cha siasa kuchukua hadhari kisipoteze uasili wake kutokana na mtindo wa kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine, kwa imani kila anayehama ni mwanasiasa makini au mzalendo.
Ikumbukwe; dirisha likiachwa wazi hupitisha hewa safi, lakini mbu na inzi hupita ingawa si kusudio.