Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, London

Katika kusherekea miaka 47 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni bora kuwakumbusha Watanzania kuwa CCM imeshika hatamu za nchi.

Kwa kutumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa mabadiliko mara nyingi, sheria za nchi yetu na Kamusi Kuu ya Kiswahili Toleo la 2 ya mwaka 2015, ninajenga hoja katika makala haya kwamba chama kushika hatamu ni dhana ambayo ipo kikatiba, kisheria na kimantiki Tanzania.

Ili kuijua vema maana ya dhana hii, ni vizuri kuangalia maana ya maneno yanayoiunda kilugha na kisheria kama ifuatavyo:

Chama ni ‘Kikundi cha watu wenye lengo, maazimio na sheria zinazowaongoza katika kutekeleza majukumu fulani’.

Katika makala haya, chama maana yake ni cha siasa.

Kisheria au kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 151(1), ‘Chama cha Siasa’ maana yake ni chama kilichoandikishwa kikamilifu kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, ya Mwaka 1992.

Hiki ni chombo kinachowaunganisha watu wenye itikadi, shabaha na lengo moja la kushika mamlaka ya kuunda Serikali kupitia uchaguzi halali ili kutekeleza ilani au sera zao kwa manufaa ya taifa.

Chama kinashinda uchaguzi na kinaunda Serikali kupitia wanachama wake. Lakini Chama tawala si Serikali.

Kazi za Chama ni tofauti na kazi za Serikali. Chama kina kazi ya kuisimamia Serikali yake katika kutekeleza sera na ilani ya uchaguzi ya Chama.

Kazi za Serikali ni kutekeleza sera na ilani ya uchaguzi ya Chama kinachounda Serikali.

Chama kinatoa maagizo kwa Serikali. Nayo Serikali inatekeleza maagizo hayo kwani ni chombo chenye miundombinu na taasisi za kutekeleza maagizo ya Chama.

Chama ni kiunganishi kati ya Serikali na wananchi. Ni wajibu wa Chama wakati wote kuyajua matatizo, mawazo na matarajio ya wananchi na kuyafikisha Serikalini.

Ni wajibu wa Chama kuikosoa au kuisahihisha Serikali yake katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi; Serikali nayo inalazimika kujirekebisha na kujisahihisha.

Pia ni wajibu wa Chama kuwaeleza wananchi mafanikio, uamuzi na changamoto ambazo Serikali inakabiliana nazo katika kuitekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama tawala.

Kwa kufanya kazi hizi, Chama tawala hujizatiti, huendelea kuwa kipya na huwavutia wananchi wengi katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. (Rejea Wasia wa Mwalimu Nyerere kwa CCM).

Kushika ni neno linakotokana na kitenzi ‘shika’ chenya maana ya, “tia kitu au mtu mwingine mkononi; kamata.” Rejea Kamusi Kuu ya Kiswahili Toleo la 2 ya mwaka 2015.

Katika makala haya, baada ya Chama kuchaguliwa kihalali kinakuwa kimetia mkononi au kimekamata — Kushika Serikali ili kuweza Serikali.

Hatamu maana yake ni ‘a. Kamba inayofungwa lijamu kwa ajili ya kumwongozea mnyama agh. Hutumika kwa farasi na punda; zimamu b. Uongozi; madaraka, uendeshaji wa chombo.’

Msemo: Ameshika hatamu ni sawa na kusema anaongoza chombo, taasisi au nchi. Kamusi Kuu ya Kiswahili Toleo la 2 ya mwaka 2015.

Hapa maana yake ni Chama kuongoza nchi yetu ambayo ina vyombo vyake dola, mihimili yake ya dola na taasisi zake zote.

‘Serikali’ maana yake ni pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar au Halmashauri ya Wilaya au ya Mji, na pia mtu yeyote nayetekeleza madaraka au mamlaka yoyote kwa niaba ya Serikali au Halmashauri.

Hii ni kwa mujibu wa Ibaara ya 151.-(1) ya Katiba.

Kwa hiyo, Kikatiba, Kisheria, Kilugha na Kimantiki dhana ya Chama Kushika Hatamu maana yake hapa ni CCM iliyoshinda uchaguzi halali na kuunda Serikali ina mamlaka ya Kikatiba na Kisheria kutoa msukumo kwa Serikali yake kutekeleza ilani ya uchaguzi ambayo inatoa maelekezo kwa Serikali yake ya nini kifanyike, kwa nani, wapi, kwa nini, kwa muda gani na kwa namna gani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa kuwa Chama tawala kina dhamana ya kuongoza nchi au Kimeshika Hatamu za nchi, basi mihimili mingine ya Bunge na Mahakama pamoja na vyombo vyote vya dola vina wajibu wa kutekeleza ilani ya uchaguzi katika maeneo yake yote kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Na hili halina maana ya kuingilia uhuru wa Bunge au Mahakama.

Mazingira ya dhana ya ‘chama kushika hatamu’

Katika nchi nyingi duniani dhana ya Chama Kushika Hatamu ipo Kikatiba na kisheria katika mazingira ya aina mbili:

(i) Mazingira ya chama kimoja cha siasa. Mfano nchi kama China, Cuba, na Korea Kaskazini.

(ii) Mazingira ya vyama vingi vya siasa. Mfano huu ni katika nchi zenye mfumo wa vyama vingi vya siasa kama ilivyo Tanzania, Marekani, Ufaransa, Afrika Kusini, Kenya na kwingineko.

Jambo la muhimu kufahamu hapa ni kwamba katika nchi zenye mfumo wa chama kimoja au vyama vingi vya siasa, Chama cha siasa kinaunda Serikali baada ya kufanyika uchaguzi halali ili kupata ridhaa ya wananchi ya kuunda Serikali.

China wanafanya uchaguzi. Marekani wanafanya uchaguzi. Kila nchi inasema uchaguzi wake ni halali.

Chama kinachounda Serikali hushika hatamu

Duniani kote hakuna Chama kinachounda Serikali halafu kisiwe na mamlaka ya kushika hatamu na kuongoza shughuli za Serikali na mihimili mingine ya dola katika nchi husika.

Chama hicho hakipo iwe katika mfumo wa kibepari wa nchi za magharibi na wafuasi wa mfumo huo au katika mfumo wa nchi za kikomunisti na kijamaa.

Vyama vya siasa vinaposhirikiana kuunda Serikali basi vinakuwa vimeshika hatamu kwa pamoja kama ilivyo sasa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kati ya CCM na ACT-Wazalendo au kama ilivyokuwa Tanzania chini ya Tanganyika African National Union (TANU) na Afro Shiraz Party (ASP) kuanzia Aprili 26, 1964 baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hadi vyama hivyo vilipoungana na kuzaliwa CCM Februari 5, 1977.

Na pale penye vyama viwili au zaidi vya siasa ambapo Chama kimoja kimeshinda uchaguzi wa Rais na kuunda Serikali na Chama kingine kimeshinda uchaguzi wa wabunge na kuongoza Bunge kama ambavyo hutokea kila mara huko Marekani, basi Chama kinachounda Serikali (kwa sasa Democratic) kina nguvu zaidi kuliko Chama kinachoongoza Bunge (kwa sasa Republican) katika kuiongoza nchi ya Marekani.

Hatamu za nchi ya Marekani bado ziko mikononi mwa Democratic kinachounda Serikali kwani ndicho chenye Rais ambaye ni Mkuu wa Nchi, Amiri Jeshi Mkuu na alama ya nchi ingawa kuna vuta nikuvute katika masuala ya bajeti na maslahi binafsi ya vyama hivi na lengo kuu ni kutaka kupata ushindi wa kuunda Serikali katika uchaguzi utakaofanyika Novemba 2024.

Katika Marekani vyama vya Democratic na Republican hushindana sana katika kuhakikisha

vinaupata Urais ili kuwa na fursa ya kuwateua majaji wengi na hasa majaji katika Mahakama ya Rufani ya nchi hiyo.

Lengo la vyama hivi ni kushika hatamu katika mhimili huu wa Mahakama na kushawishi uamuzi.

Katika Marekani Mahakama iko katika muundo wa kiitikadi na kisiasa na inafanya kazi zake hivyo – chini ya ushawishi wa vyama vya siasa na itikadi.

Dhana hii kwa Tanzania

Dhana hii Tanzania imekuwepo Kikatiba na kisheria katika mazingira ya chama kimoja cha siasa na mazingira ya vyama vingi vya siasa.

Chama Kushika Hatamu ni dhana ambayo imekuwepo tokea kupatikana kwa uhuru

wa Tanganyika na Zanzibar na imeendelea kuwepo tokea kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1964.

Vyama vya TANU na ASP vilikuwa vimeshika hatamu. Mnamo Juni 3, 1975, Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais, Ndugu Rashid Kawawa aliwasilisha katika Bunge Muswada wa Kubadili Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1965 na alitoa hoja kwamba dhana ya Chama Kushika Hatamu iwekwe katika Katiba.

Mwaka 1977 ilitungwa Katiba mpya baada ya kuzaliwa kwa CCM. Dhana hii ikawekwa katika Ibara ya 3 ya Katiba ya mwaka 1977 na kuipa CCM mamlaka ya kushika hatamu za vyombo vyote vya dola na kuwa Chama pekee cha siasa nchini kwa tamko kwamba:

(i) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania taifa la kidemokrasia na kijamaa lenye Chama kimoja cha siasa.

(ii) Chama kina mamlaka ya utendaji kwenye mambo yote kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Chama.

(iii) CCM ni Chama pekee cha siasa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 1984 ambayo yaliingiza Tangazo la Haki za Binadamu katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 nayo yaliendelea kuipa mamlaka CCM ya kushika dola na kuwa Chama pekee cha siasa nchini kilichoshika hatamu.

Dhana hii katika mazingira ya Chama kimoja cha siasa ilifutwa kufuatia mabadiliko ya Katiba ya mwaka 1977 yaliyofanyika mwaka 1992 na kuruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.

Mabadiliko hayo ya Katiba yalifuta ibara ya 10 ya Katiba ya mwaka 1977 iliyokuwa na tamko kwamba CCM ni Chama pekee cha siasa nchini.

Mabadiliko hayo ya Katiba yaliweka bayana kwamba:

(i) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi yenye kufuata mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi vya siasa.

(ii) CCM na vyama vingine vya siasa vinaweza kuunda Serikali baada ya kushiriki na kushinda uchaguzi halali wa kidemokrasia kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria za nchi.

Kufutwa kwa ibara ya 10 ya Katiba ya mwaka 1977 kuliondoa mamlaka ya CCM kuwa Chama pekee ambacho kinaweza kushika hatamu za nchi katika mazingira ya vyama vingi vya siasa.

Ilikuwa ni lazima ibara ya 10 ifutwe ili CCM iwe sawa na vyama vingine vya siasa vyenye lengo la kushiriki uchaguzi halali ili kuunda Serikali.

Kama ibara ya 10 ya Katiba isingefutwa, ina maana kwamba katika mazingira ya vyama vingi vya siasa na hata kama CCM ingeshindwa katika uchaguzi halali na kukosa sifa za kuunda Serikali, CCM ingeendelea kuwa na mamlaka kushika hatamu za nchi Kikatiba.

Huu ni utata mkubwa. Ilibidi ibara ya 10 ifutwe ili kuondoa utata huu.

Jambo muhimu la kuelewa hapa ni kwamba kufutwa kwa ibara ya 10 kulifuta dhana ya Chama Kushika Hatamu katika mazingira ya Chama kimoja cha siasa nchini, lakini hakuna maana kwamba dhana ya Chama Kushika Hatamu haipo katika mazingira ya Tanzania yenye vyama vingi vya siasa. Ipo.

Katika Mazingira ya Vyama Vingi vya Siasa, dhana ya Chama Kushika Hatamu ipo Kikatiba na Kisheria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni nchi changamani (complex state).

Makala haya yameandaliwa na Dk. Amani Millanga wa London, Uingereza

Itaendelea…