Na WAF – DSM

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila ameiasa timu ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia wapatao 35 kuja na majibu ya kitafiti kutoka kwa wagonjwa watakayokuna nayo wakati wa kambi ya siku sita ili kupata suluhisho la magonjwa yanayosumbua kwenye Mkoa huo.

Chalamila ametoa wito huo leo Oktoba 15, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akiwapokea timu Madaktari hao watakaotoa huduma kwa siku sita kuanzia tarehe 15 hadi 19 Oktoba 2024 katika hospitali mbalimbali za Wilaya na Halmashauri za jiji hilo.

Mhe. Chalamila amesema mkoa huo una idadi kubwa ya watu wa matabaka mbalimbali wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali, hivyo kuna uwezekano mkubwa wataalamu hao kupata mawazo ya utafiti pindi watakapomaliza kutoa tiba.

“Mnapoendelea kutibu wagonjwa mbalimbali, mtajifunza pia, tunapenda zaidi mnapomaliza tusikie mmebaini nini kwa mkoa huu, tunaamini mtaanza mchakato wa pili wa utafiti kuhusu magonjwa kadhaa ambayo mtabaini ni nadra, mkija mwakani mnakuja na matokeo yatakayowasaidia kujipanga upya,” amesema Chalamila.

“Tunamshkuru sana Rais kwa ubunifu mkubwa wa kupata madaktari bingwa wanaotoa huduma za kibingwa ndani ya mipaka ya Taifa letu hususani katika ngazi ya msingi, madaktari hawa ni matokeo chanya na suluhisho la uchunguzi na matibabu wa magonjwa mbalimbali yanayowasumbua wananchi wa jiji hili,” ameongeza Mhe. Chalamila.

Naye Kaimu Katibu Tawala wa mkoa Mhandisi Amani Mafuru amesema Mhe. Rais ametoa kipaumbele katika sekta ya afya kwa kutoa Madakatri hawa kuzunguka nchi nzima kwa ajili ya kutoa huduma kwa watanzania, amepigania sekta ya afya na kuzunguka katika halmashauri zote ni kumpa sifa Rais kwa kuwajali wananchi wake.

Madaktari hao watatoa huduma mbalimbali zikiwemo za magonjwa ya kinywa na meno, uzazi na magonjwa ya wanawake, upasuaji wa magonjwa mbalimbali, huduma za watoto wachanga na magonjwa ya ajali.      

Please follow and like us:
Pin Share