Na Mwandishi wetu JAMHURI MEDIA Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Albert Chalamila ametoa rai kwa wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga waliolikimbia soko la Mwenge Cocacola kurudi mara moja katika maeneo rasmi waliyopangiwa ndani ya wiki moja.

Wamachinga  hao wanalalamikiwa na wafanyabiashara wenzao waliobaki katika soko hilo kwa kukiuka utaratibu uliopangwa na serikali na kwenda kupanga biashara zao kando kando ya barabara karibu na eneo walilokuwa wakifanyia biashara zamani ambalo kwa sasa kinajengwa kituo cha daladala Mwenge.

Chalamila ametoa rai hiyo leo Juni 30, 2023 alipofanya ziara ya dharula katika soko la Mwenge Cocacola,mara baada ya  kufanya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa kituo cha daladala cha Mwenge jijini Dar es salaam.

“Sasa nitangaze rasimi kwamba wale wote ambao wametoka hapa waanze kurudi wenyewe, na kama wataona ni muhimu mimi niweze kutumia njia zingine za wao kuwasogeza huku basi nitafanya hivyo.”amesema Chalamila

Aidha amewashukuru wafanyabiashara walioendelea kusalia katika soko hilo kufanya bishara zao kwa kuonyesha ukomavu katika utii, na kuamuru mamlaka zichukue hatua haraka kwa waliokiuka ili kuhakikisha waliobaki katika soko wanapata wateja ili kuweza kuendesha Maisha yao.

“Tumetembea kutoka mwanzo wa soko hili mpaka mwisho tumeona wapo wafanyabiashara ambao wameonyesha ukomavu wa utii wapo hapa na wanafanyabiashara zao.” Amesema

“Lakini malalamiko ni kwamba kama wenzao wachache wameondoka wamekwenda mahali pengine ambapo ndipo pia kunaweza  kukawa na mapito pia ya  wateja wengi maana yake wao watabaki kule kwenye maeneo haya wakakosa wateja na mwisho wa siku watashindwa kumudu familia zao na  watashindwa kumudu mahitaji yao ya msingi.” Amesema Chalamila