Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amekutana na Kamati ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani Ofisini kwake Ilala Boma jijini Dar es Salaam.
RC Chalamila akiongea na ujumbe huo wa JWTZ amemshukuru CDF John Jacob Mkunda na Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kufuatia Mkutano huo Mkubwa wa Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani kufanyika hapa Tanzania hususani Mkoa wa Dar es Salaam ambapo amesema mkutano huu utafungua fursa za kiuchumi kwa Watanzania na ni kiashiria cha nguvu ya Diplomasia katika kukuza uchumi wa Taifa letu.
Aidha RC Chalamila amesema katika Kipindi cha uongozi wa Rais Dkt Samia Taifa linashuhudia kuimarika kwa Diplomasia ya Uchumi kwa kasi kubwa ambapo mwezi uliopita Mkutano Mkubwa wa kujadili mtaji wa rasilimali mali watu ulifanyika hapa nchini na kuhudhuriwa na mataifa zaidi ya 40 vilevile mwezi huu Septemba tunatarajia kuwa na Kongamano kubwa la mifumo ya Chakula Afrika ( AGRF SUMMIT) inayotarajiwa kuanza tarehe 4-8 Septemba 2023 Jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa JNICC,.
Hayo yote ni matunda ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika Kuimarisha Diplomasia ndani na nje ya nchi, hivyo Mkoa kwa heshima kubwa ya Mhe Rais umepokea kwa furaha taarifa ya kufanyika tena kwa kwa Mkutano Mkubwa wa Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani hiyo ni fursa nyingine kwa taifa sio tu kwa upande wa michezo bali ni fursa ya kukuza uchumi wa Watanzania, hivyo Mkoa uko tayari kutoa ushirikiano wa kutosha kufanikisha mkutano huo.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi Meja Jenerali Francis Mbindi amesema mkutano huo unatarajiwa kufanyika hapa nchini, Mkoani Dar es Salaam kuanzia tarehe 12- 19 May 2024 nchi zaidi ya 140 zitashiriki, Ufunguzi utafanyika May 14,2024 mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu na utafungwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan hivyo wamekuja kukutana na mkuu wa Mkoa kwa lengo la Kujitambulisha na kuomba msaada wa hali na mali katika kufanikisha mkutano huo wa kihistoria