Shughuli za Chama cha Kutetea Haki na Masilahi ya Walimu Tanzania (CHAKAMWATA) zimebatilishwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Ajira baada ya kubaini chama hicho kukosa bodi ya wadhamini.
Ofisi ya Msajili imefikia uamuzi huo wakati chama hicho cha walimu kikiwa katika maandalizi ya mkutano mkuu wa dharura wa taifa uliolenga kuwachagua viongozi wake wapya. Mkutano huo ulitarajiwa kufanyika Agosti 4, mwaka huu, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa barua ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Ajira yenye namba ya kumbukumbu RTU/U/194/02/49, iliyoandikwa Julai 30, mwaka huu kwenda kwa mwenyekiti wa chama hicho inaelekeza kusudio la ofisi hiyo kuzuia mkutano huo mkuu wa taifa.
Barua hiyo iliyosainiwa na Kaimu Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Ajira, Pendo Berege, inaeleza kuwa ofisi yake ilipata taarifa za kuitishwa kwa mkutano wa CHAKAMWATA ngazi ya taifa ilhali chama hicho hakijasajili bodi ya wadhamini.
Kasoro zilizoorodheshwa katika barua hiyo ni pamoja na ukiukwaji wa makusudi wa Katiba ya CHAKAMWATA, Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 na Sheria ya Usajili wa Wadhamini Sura ya 318 ya mwaka 2003.
Kutokana na kasoro hizo, kaimu msajili huyo amesitisha shughuli zote za chama hicho huku kosa la kutosajili bodi ya wadhamini akilifananisha na kosa la uhaini.
Katika barua hiyo amesema bodi ya wadhamini ndicho chombo hai cha kisheria cha kuendesha, kusimamia, kulinda na kumiliki mali za chama, kushtaki na kushtakiwa ikiwa ni pamoja na kutetea masilahi ya chama na wanachama, hivyo uwepo wa bodi hiyo ni sehemu ya matakwa ya kisheria.
Aidha, barua hiyo imeeleza kuwa ofisi ya msajili haikitambui chama hicho na kwamba kimekosa uhalali wa kuendelea na shughuli zake.
Barua hiyo inawatahadharisha viongozi wa chama hicho kutokukiuka agizo hilo na endapo watalikiuka hatua kali zitachukuliwa.
Mwenyekiti wa CHAKAMWATA taifa, Japhet Magesa, amelieleza JAMHURI kuwa chama chao kimeonewa na ofisi ya msajili.
Amesema msajili hakupaswa kubatilisha shughuli za chama chao na badala yake alipaswa kukipa mwongozo wa kujiendesha kwa ufanisi.
“Sisi tangu tumesajili chama hiki mwaka 2015, ni kweli tumekiendesha bila kuwa na bodi ya wadhamini na kwa vile kiko kwenye mwelekeo wa kukua tulikuwa kwenye mchakato wa kuchagua viongozi wa chama,” amesema Magesa.
Hata hivyo anabainisha tangu amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho kumekuwa na migogoro ya makusudi inayotengenezwa na mahasimu wa chama hicho ili kukidhoofisha.
“Tumekuta chama hiki kikiwa na hali mbaya kifedha hata wanachama walikuwa hawajiungi nacho lakini kwa muda mfupi tumeweza kuwashawishi walimu na wamehamasika,” amesema na kuongeza kuwa makato ya asilimia moja kwa mwanachama anayejiunga na chama hicho yamevutia walimu wengi kiasi kwamba wamekuwa wakijiondoa kwa idadi kubwa kutoka katika Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ili kujiunga CHAKAMWATA.
“Sasa hawa wanaona uwepo wa CHAKAMWATA tishio ndiyo maana unaona kuna nguvu kubwa inatumika kutaka kututoa kwenye lengo la kumuokoa mwalimu,” amedai Magesa.
Ameeleza kuwa tangu Februari mwaka huu CHAKAMWATA imekuwa haifanyi kazi kwa madai kuwa inasumbuliwa na migogoro. Kwa mujibu wa maelezo yake, mgogoro unaotajwa kuwa kwenye chama hicho umekuzwa na baadhi ya viongozi wa serikali.
“Viongozi wasio waadilifu katika serikali ya Rais John Magufuli wanashirikiana na CWT kulazimisha walimu wakatwe asilimia tatu, yaani asilimia mbili ya CWT na asilimia moja ya CHAKAMWATA, jambo lililoonekana kama kumkandamiza mwalimu,” amesema.
Amesema wameomba ufafanuzi kuhusu azima hiyo ya kumtaka mwalimu asikatwe asilimia tatu ilhali sheria ya kujiunga na vyama vya wafanyakazi inamtaka mtu kuchagua chama anachopenda.
“Rais John Magufuli aliwahi kusema walimu waachwe wajiunge na chama wanachokipenda. Hawa wenzetu wanapanga mkakati wa kurudisha walimu wote walioko CHAKAMWATA warudi CWT. Hii barua kabla ya kutufikia sisi walianza kupelekewa CWT wakaisambaze, sasa hapo unaweza kuona uhalali wa kilichoandikwa humo, kwa nini barua inayotuhusu waipate watu wa CWT na waanze kusambaziana wao kwa wao?” amehoji.
Aidha, amesema kama CWT iliyoanzishwa mwaka 1993 imefanya usajili wa bodi ya wadhamini mwaka 2015, kwa nini wao ambao ndio wanaanza kukua waonekane kutenda makosa ya kihaini kwa kutokuwa na bodi hiyo.
“Kwenye katiba yetu tumeainisha namna tutakavyokiendesha, ukiisoma katiba yetu sura ya 6, kifungu cha 33 (4) kinasema katibu wa CHAKAMWATA wa ngazi husika atakuwa ndiye mtunzaji mkuu wa mali za chama zisizohamishika na zinazohamishika.
“Chama chetu kinakua kwa kasi, ndani ya miezi mitatu ambayo tulikuwa tumeamua kuzunguka mikoani kusajili wanachama tumefikia walimu 14,000.
“Mkutano wetu uliozuiliwa ulikuwa uhudhuriwe na wanachama takriban 200 kutoka mikoa yote nchini na wengi ni wale waliokuwa wanachama wa CWT,” amesema.
Amedai kuwa CWT wanashirikiana na aliyekuwa naibu katibu mkuu wa CHAKAMWATA, Meshack Kapange, pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali kukihujumu chama hicho.
Kwa mujibu wa Magesa, Kapange amefukuzwa unaibu katibu mkuu wa chama hicho.
“Sisi tunajua anayetuvurugia chama, na tunafahamu wanaotuvuruga. Viongozi wenye masilahi na CWT wanamtumia Kapange kutuvuruga hadi leo anahudhuria mikutano ya wizara pindi viongozi wa vyama vya wafanyakazi wanapohitajika, unaweza kujiuliza anayempa nafasi hiyo ni nani?” amehoji Magesa.
Hata hivyo amesema walimuengua kwenye uongozi wake baada ya kupoteza sifa ya kuwa mwanachama na kwamba alishiriki kuhamisha fedha za chama hicho kwenda kwenye akaunti alizozianzisha.
Anazitaja akaunti ambazo fedha zilihamishwa kuwa ni akaunti ya Tabora ambako alihamisha Sh milioni 12, akaunti ya Rungwe Sh milioni 12, Kinondoni Sh milioni 37.5 na Mbeya vijijini amehamisha Sh milioni 4.5.
Kutokana na ubadhirifu wa fedha za CHAKAMWATA ambao ulikuwa ukifanywa na katibu huyo, mwenyekiti amesema ameshirikiana na viongozi wengine wa chama kuzifunga akaunti zote za chama zikiwemo zilizopo Mbeya.
Gazeti la JAMHURI limezungumza na Kaimu Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Ajira, Pendo Berege, kuhusiana na barua aliyoiandika kwenda CHAKAMWATA.
“Kweli mimi ndiye nimesaini kwenye ile barua, ila tunafuata utaratibu, mpigie katibu wangu atakupa ufafanuzi mzuri kuhusu barua hiyo. Mimi baada ya kusaini barua kazi yangu ilikomea pale, maelekezo mengine au ufafanuzi wowote unatoka kwa katibu, wasiliana naye atakujibu,” amesema Berege.
Naye Meshack Kapange, amelieleza Gazeti la JAMHURI kuwa wanaomtuhumu ni matapeli na si viongozi wa CHAKAMWATA.
Amesema kuwa hao wanaojiita viongozi walipewa nafasi hiyo kwa muda na ilipofika Februari 2, mwaka huu walivuliwa nyadhifa zao.
Aidha, amewaonya viongozi hao kutochafua jina lake kwa kumhusisha na mbinu zinazotumiwa na Chama cha Walimu (CWT) kuidhoofisha CHAKAMWATA, na badala yake amesema Magesa ndiye ambaye amekuwa akiunda njama hizo za kukiua chama kwa kuwatumia viongozi wa CWT.
“Hawa watu wametumiwa na viongozi wa CWT, kwanza waliingilia uchaguzi wa mwaka jana, badala ya mwenyekiti kuchaguliwa kwa kura, wajumbe walielekezwa kuinua mikono juu. Huyu hana sifa za kuwa kiongozi kwenye chama, kwa sababu katiba inasema ili uweze kugombea ngazi yoyote ya uongozi ni lazima uwe umetimiza miaka mitatu ya kukitumikia chama, hana sifa hiyo.
Amesema tuhuma za upotevu wa fedha anazohusishwa nazo si za kweli na kwamba anazushiwa ili kumuondoa kwenye chama, kwani yeye ndiye mtetezi wa fedha za wanachama zilizoko kwenye akaunti za chama hicho.
Amesema Julai 24, mwaka huu wanaojiita viongozi wa CHAKAMWATA walishindwa kesi mahakamani na kwamba ndicho chanzo cha kutaka kuitisha mkutano mkuu wa dharura ili wamuengue.
“Tumefanya ukaguzi kwenye akaunti za chama tukabaini ameiba Sh 35,235,100 na mpaka anaenguliwa kwenye uongozi pamoja na genge lake wamekiibia chama zaidi ya Sh milioni 80,” amedai Kapange.
Kapange amedai uongozi wa CHAKAMWATA anaoutambua ni Mwenyekiti wa chama hicho, Ipiana Kavije, Makamu wake, Juma Zongoli na katibu wa chama hicho ambaye ni yeye mwenyewe.
Gazeti la JAMHURI limeona nyaraka za kesi ya uhujumu uchumi namba 5 ya mwaka 2019 iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya dhidi ya Kapange na wenzake.
Katika kesi hiyo Meshack Lupakisio Kapange na wenzake wawili, Peter Kanyosa na Gladness Ephron wanashitakiwa kwa wizi wa Sh 19,719,150.
Hukumu hiyo inaeleza kuwa mnamo Oktoba 31, 2018, watuhumiwa wakiwa eneo la Uyole, jijini Mbeya waliiba pesa hizo kutoka kwenye akaunti ya NMB ambayo inamilikiwa na CHAKAMWATA.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Kapange na wenzake walitekeleza kosa la matumizi mabaya ya ofisi kwa mujibu wa Kifungu cha 96, Sura (1) na (2) ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2016.
Naye Mratibu wa CHAKAMWATA Mkoa wa Dar es Salaam, Patrick Emmanuel, amelieleza Gazeti la JAMHURI kuwa mgogoro ndani ya CHAKAMWATA unatengenezwa na viongozi wa CWT wakimtumia Katibu wa CWT Gairo, Waziri Banga.
Emmanuel anadai katibu huyo anashirikiana na Kapange kuratibu hujuma zote dhidi ya chama chao.
Anaomba Rais John Magufuli kuingilia kati migogoro inayofukuta ndani ya vyama hivyo viwili, yaani CWT na CHAKAMWATA.
Naye Waziri Banga amelieleza Gazeti la JAMHURI kuwa hajawahi kukaa wala kuzungumza na Meshack Kapange japo wanakutana katika mikutano mbalimbali ya vyama vya walimu.
“Hao viongozi wa CHAKAMWATA wapambane na hali yao, waache kutuingiza CWT kwenye vitu visivyo na msingi.
“Mimi ni kiongozi wa CWT huku Gairo vijijini, mambo ya CHAKAMWATA ninaweza kuyajulia wapi? Wapambane kivyao bwana,” amesema Banga.