Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimethibitisha rasmi mahali alipo Mwenyekiti wake Taifa, Mheshimiwa Tundu Lissu, ambaye awali iliripotiwa kutoweka kutoka Gereza la Keko bila maelezo yoyote rasmi.

Katika taarifa mpya iliyotolewa leo, Aprili 19, 2025, CHADEMA imesema kuwa baada ya ufuatiliaji wa karibu na mawasiliano na Jeshi la Magereza, viongozi wa chama wameelezwa kuwa Kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani, Lissu amehamishiwa katika Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam.

Hatua hii imeleta ahueni kwa familia, wanachama wa CHADEMA, na Watanzania waliokuwa na wasiwasi kuhusu usalama na hali ya Lissu kufuatia taarifa ya chama hicho ya kutofahamishwa alipo kiongozi wao.

Taarifa hii inakuja baada ya siku ya sintofahamu ambapo viongozi wa chama, wakiwemo mawakili na familia, walizuiwa kumuona Lissu gerezani Keko, huku wakielezwa kuwa hayupo tena hapo na bila kuelezwa alikopelekwa.

Inaelezwa kuwa ni utaratibu wa kawaida wa mahabusu kuhamishwa kutoka gereza moja kwenda lingine.

Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, Mheshimiwa John Heche, anatarajiwa kumtembelea Lissu gerezani Ukonga leo kwa lengo la kuzungumza naye na kujua hali yake kwa sasa.

Lissu alikamatwa hive karibuni na kupandishwa Mahakamani kwa tuhuma za uhaini, kosa ambalo halina ushahidi.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam tayari lilitoa onyo kuhusu mpango wa CHADEMA kuhamasisha umma kujitokeza mahakamani tarehe 24 Aprili, siku ambayo Lissu anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya uhaini.