Chadema: Tunataka Serikali 3
A. JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MUUNDO WAKE
1. Kutakuwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo itakuwa ni shirikisho lililoundwa na nchi ya Tanganyika na nchi ya Zanzibar.
2. Kutakiwa na haki kamili ya kila nchi inayounda Jamhuri ya Muungano kujitoa katika Muungano lakini haki hiyo itatumiwa kwa masharti kwamba uamuzi wa kujitoa katika Jamhuri ya Muungano lazima upate ridhaa wa upande husika kwa kura ya maoni (referendum/plebiscite) kwa idadi isiyopungua theluthi mbili ya kura zote halali.
3. Kutakuwa na Serikali ya Muungano ambayo itakuwa na madaraka juu ya mambo ya Muungano pekee. Mambo ya Muungano yatakuwa yafuatayo:
(a) Mambo ya nje yanayohusu masuala ya diplomasia lakini yasiyohusu ushirikiano wa kimataifa;
(b) Ulinzi na usalama isipokuwa kwa masuala ya polisi na magereza;
(c) Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano (Supreme Court of the United Republic);
(d) Uraia na uhamiaji;
(e) Sera za fedha na sarafu;
(f) Sera za biashara ya kimataifa na masuala ya forodha;
(g) Masuala ya ithibati ya elimu ya juu.
4. Kutakuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye atakuwa Mkuu wa Serikali ya Muungano, Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ulinzi ya Jamhuri ya Muungano.
5. Rais wa Jamhuri ya Muungano atachaguliwa na Wajumbe wote wa Bunge la Muungano, Bunge la Tanganyika, Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wenyeviti, mameya na magavana wote.
6. Rais wa Jamhuri ya Muungano atachaguliwa kwa kipindi kimoja cha miaka mitano na anaweza kuchaguliwa kwa kipindi kingine kimoja cha miaka mitano, na atachaguliwa kwa msingi wa kuachiana zamu ya kushikilia madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano Kati ya nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano.
B. MUUNDO WA VYOMBO VYA UTEKELEZAJI WA MAMLAKA YA NCHI
Shughuli zote za mamlaka ya nchi katika Jamhuri ya Muungano zitatekelezwa na kudhibitiwa na vyombo vitatu vyenye mamlaka ya utendaji, VYOMBO vitatu vyenye mamlaka ya utoaji haki na vyombo vitatu vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma.
1. Vyombo vyenye mamlaka ya utendaji vitakuwa ni Serikali ya Tanganyika; Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
2. Vyombo vyenye kutekeleza utoaji wa haki vitakuwa ni Mahakama ya Serikali ya Tanganyika, Mahakama ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mahakama Kuu ya Serikali ya Muungano.
3. Vyombo vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma vitakuwa ni Bunge la Tanganyika, Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Bunge la Jamhuri ya Muungano.
C. MGAWANYO NA UTENGANISHO WA MADARAKA
Mfumo wa sasa wa kikatiba umeondoa mgawanyo na utenganisho wa madaraka kati ya mihimili mikuu ya dola. Mfumo huu umeruhusu Serikali na hasa ofisi ya Rais kuwa na mamlaka makubwa juu ya mihimili mingine, yaani Bunge na Mahakama. Hali hii imeondoa udhibiti wa mamlaka na uwajibikaji katika mfumo mzima wa uongozi na utawala katika nchi yetu. Katiba Mpya iweke utaratibu ufuatao wa mgawanyo na utenganisho wa madaraka baina ya mihimili ya dola:
1. Dhana na nafasi ya Rais kama sehemu ya Bunge iondolewe katika mfumo wetu wa kikatiba bali abakie kama Mkuu wa Serikali.
2. Dhana na nafasi ya mawaziri – ambao pia ni wakuu wa Idara za Serikali – kama Wabunge iondolewe bali Bunge libakie kuwa la Wabunge na mawaziri wawajibike kwa Bunge hilo.
3. Rais asiwe na mamlaka ya kuteua Wabunge na Katibu wa Bunge ili hadhi ya Bunge kama chombo cha uwakilishi wa wananchi na uwajibishaji wa Serikali ilindwe.
4. Rais asiwe na mamlaka au uwezo wa kuvunja Bunge kwa sababu yoyote ile. Aidha, ili kuhakikisha Bunge linakuwepo muda wote ili kuisimamia Serikali muda wote, uchaguzi wa Bunge au sehemu yake utenganishwe na uchaguzi wa Rais.
5. Rais asiwe na mamlaka ya kupanga mishahara, posho na marupurupu ya Wabunge, bali kazi hiyo ifanywe na Tume huru ya Utumishi wa Bunge.
6. Mfumo mzima wa uteuzi wa Jaji Mkuu na majaji wengine wote wa Mahakama za juu ubadilishwe ili kuhakikisha Mahakama ina viongozi na watendaji wenye uadilifu, uwezo wa kitaaluma na uzoefu wa kiutendaji katika utoaji wa haki. Ili kutekeleza jambo hili, mfumo wa uteuzi wa majaji unapaswa kuwa kama ifuatavyo:
(a) Wanaotaka kuteuliwa kuwa majaji wa Mahakama ya Tanzania wapeleke maombi katika (Tume), wasailiwe na kuchujwa na, Tume huru ya Utumishi wa Mahakama katika mchakato ulio wazi;
(b) Majina ya Waombaji wenye sifa stahili za kuteuliwa majaji yapelekwe kwa Rais ili aweze kufanya uteuzi kutokana na mapendekezo ya Tume huru ya Utumishi wa Mahakama;
(c) Watakaoteuliwa na Rais wapelekwe Bungeni ili Bunge liridhie uteuzi wao kwa kutumia mchakato ulio wazi na baada ya kusikiliza maoni ya wadau wengine (confirmation hearings);
7. Rais asiwe na mamlaka ya kumwondoa, kumsimamisha au kumpatia kazi nyingine Jaji wa Mahakama ya Tanzania bali utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya majaji uwe huru na wa wazi ili kuhakikisha uhuru wa Mahakama unalindwa kama ifuatavyo:
(a) Hoja yoyote ya kumwondoa Jaji wa Mahakama ya Tanzania ipelekwe kwa maandishi katika Tume huru ya Utumishi wa Mahakama;
(b) Tume huru ya Utumishi wa Mahakama ifanye uchunguzi wa awali (preliminary inquiry) ili kujiridhisha kwamba kuna sababu za msingi za kuanzisha uchunguzi wa kina wa kinidhamu juu ya Jaji husika;
(c) Tume huru ya Utumishi wa Mahakama iunde Tume huru ya Uchunguzi ya Kijaji (Judicial Commission of Inquiry) itakayojumuisha majaji kutoka ndani na nje ya Tanzania ili kufanya uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Jaji husika;
(d) Tume ya Uchunguzi ya Kijaji ifanye uchunguzi wake kwa kufuata utaratibu ulio wazi na huru na utakaohakikisha Jaji husika anapatiwa fursa kamili ya kusikilizwa na ya kujitetea;
(e) Endapo Tume ya Uchunguzi ya Kijaji itathibitisha tuhuma dhidi ya Jaji husika basi Jaji huyo atalazimika kujiuzulu, na endapo Tume haitathibitisha tuhuma hizo basi Jaji ataendelea na madaraka yake lakini atakuwa na haki ya kulipwa fidia na/au gharama zake;
8. Rais asiwe na madaraka ya kuongeza muda wa ajira ya Jaji kwa sababu yoyote ile, na wala asiwe na mamlaka ya kupanga mishahara, posho na marupurupu ya majaji bali kazi hiyo ifanywe na Tume huru ya Utumishi wa Mahakama.
9. Rais asiwe na mamlaka ya kuteua watendaji wengine wote wa Mahakama wasiokuwa majaji bali watendaji hao wateuliwe na Tume huru ya Utumishi wa Mahakama kwa kufuata utaratibu wa wazi.
Wiki ijayo tutakuletea sehemu ya pili ya mtazamo wa Chadema juu ya Katiba mpya. Sehemu hii itaanza na mfumo wa Serikali ya Tanganyika utakuwaje.