Na Tatu Saad, JamhuriMedia
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimechambua ripoti ya CAG ambapo wamesema Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kutengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), haitoshi bali hatua zaidi zinatakiwa kuchukuliwa.
CHADEMA wamesema hayo kupitia Katibu Mkuu wa CHADEMA,John Mnyika leo April 10, 2023 katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Mnyika amesema ni vizuri umma ukafahamu kama mzizi wa matatizo uliopelekea kuondoka kwa mkurugenzi huyo ni ununuzi wa ndege za serikali ambazo zimewekwa na kutumika na kampuni ya ATCL.
Mnyika amesisitiza ni lazima mchakato wa ununuzi wa ndege na hasara ya uendeshaji wa ATCL utazamwe kwa makini kwani kumuondoa mtendaji mkuu wa wakala wa ndege pekee haijitoshelezi.
“Lazima tutazame mchakato wa ununuzi wa ndege hizi na pia hasara ya uendeshaji wa ATCL, hatua ya kumuondoa mtendaji mkuu wa wa kalazwa ndege pekee haijitoshelezi Ibu sawa na kufunika kombe”, amesema Mnyika.
Vilevile Mnyika ametoa wito kwa Rais Samia kuchukua hatua na kuweka bayana madai yote ya ufisadi na hasara ya uendeshaji wa ATCL kwa kuanza na mawaziri na makatibu wakuu waliohusika na mchakato huo,kwani kwa upande wao hawajaridhishwa na hatua zilizoelezwa na Ikulu jana,wanahitaji hatua zaidi.
“Kwenye jambo hili vile vile hatua zilizoelezwa jana na Ikulu hatujaridhika nazo na tunahitaji hatua zaidi”, amesema Mnyika.