Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),kimesema sheria iliyopo inafifisha uhuru wa vyombo vya habari katika kutekeleza majukumu yao hasa katika kipindi hiki ambacho mikutano ya hadhara imeruhusiwa, jambo ambalo litawanyima fursa ya kutekeleza majukumu yao.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema Jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya uzinduzi wa mikutano ya hadhara ya Chama hicho utakaofanyika Jijini Mwanza Januari 21, 2023. 

Amesema kuwa CHADEMA itasimama na wana habari katika kupigania mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 wakati wa mazungumzo yake na Chama cha Mapindizi (CCM) ili vyombo vya habari nchini viwe huru kuripoti habari kisiasa. 

Mrema amesema sheria iliyopo inafifisha uhuru wa vyombo vya habari na kuchangia kushindwa kutekeleza majukumu yao na kusababisha kuwanyima fursa ya kutekeleza majukumu yao.

“Kwenye mazungumzo yanayoendelea, kati ya sheria ambazo tunafikiri ni sheria za awali za kufanyiwa marekebisho au kuandikwa upya, ni pamoja na Sheria ya Huduma za Habari kwa sababu huwezi kurudi kwenye mikutano kama umevifunga vyombo vya habari mikono nyuma kwani hata taarifa za mikutano haitawafikia wananchi” amesema Mrema.