Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, kimetamba kwamba kitatumia nguvu ya umma kuishinikiza Mahakama imtoe rumande Mbunge Salvatory Machemli. Mahakama ya Wilaya iliamuru Mbunge wa Ukerewe apewe adhabu ya kwenda jela siku 14 kuanzia Novemba 6 hadi 20, mwaka huu, kutokana na kudharau amri iliyomtaka ahudhurie mahakamani kusikiliza kesi ya uchochezi namba 19/2013 inayomkabili.
Pia, Machemli ametakiwa kukabidhi polisi hati yake ya kusafiria, na amepigwa marufuku kutoka nje ya wilaya hiyo bila kibali cha Mahakama.
Tamko la kuishinikiza Mahakama imtoe mbunge huyo rumande lilitolewa katika kikao cha dharura cha wajumbe 14 wa Kamati ya Utendaji ya Chadema Wilaya, kilichofanyika Novemba 8, mwaka huu mjini Nansio, Ukerewe.
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Ukerewe, Mgaya Msilanga, amesema: “Mahakama itoe uwazi wa dhamana kwa sababu dhamana ni haki ya mshtakiwa.
“Pia, Mahakama ni chombo kinachosimamia sheria, kisimamie haki bila kuingiliwa na siasa kama inavyoonesha kwa sasa, hasa katika kesi hii.
“Tarehe 8, mwezi wa 11, mwaka 2013 viongozi wa Chadema tumefika mahakamani kuomba dhamana ya mbunge, kitu cha kushangaza hata file (jalada) la kesi hii halikuonekana mahakamani.
“Kama Mahakama haitatenda haki ya kumpa dhamana mbunge wetu, tutatumia nguvu ya umma kushinikiza apewe dhamana ili apate haki yake kisheria.”
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe, Faustine Kishenyi, aliamuru Mbunge Machemli atupwe rumande baada ya upande wa mashtaka kuomba mshtakiwa huyo afutiwe dhamana.
Mahakama ilisema Machemli na wadhamini wake ambao ni Shellifu Ngelezya, Max Mhogo na Konsolata Machemli, wamekosa sifa baada ya kushindwa kufika mahakamani kuwezesha kesi inayomkabili kusikilizwa kama ilivyopangwa.
Mwendesha Mashtaka wa Jeshi la Polisi, Inspekta Samweli Onyango, aliieleza Mahakama hiyo kwamba mshtakiwa kwa makusudi hakufika mahakamani zaidi ya mara tano bila kutoa taarifa wakati kesi yake ikitajwa.
Katika utetezi wake, Machemli alisema alishindwa kufika mahakamani kama ilivyopangwa kwa sababu ya tarehe ya kesi yake kuingiliana na vikao vya Bunge.
Awali, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, ASP Denis Rwiza, alidai mahakamani hapo kwamba mshtakiwa huyo alitenda kosa la uchochezi Oktoba 23, 2011 katika Kijiji cha Nyamanga, kisiwani Ukara, wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa wananchi ulioandaliwa na Chadema.
Alifafanua kwamba mshtakiwa kwa makusudi aliwachochea wananchi kutenda kosa la shambulio, akiwaelekeza kutumia silaha za jadi zikiwamo rungu na panga kuwazuia, hata kuwashambulia askari polisi watakaokwenda kisiwani hapo kutafuta watuhumiwa wa uhalifu nyakati za usiku.
Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka, kipindi hicho ulikuwapo msako wa watuhumiwa wa mauaji ya watu wanne waliouawa na wananchi Desemba 10, 2010 mbele ya askari polisi kutokana na tuhuma za ujambazi.