Wiki iliyopita ilikuwa ni historia nyingine katika siasa za Tanzania. Tulishuhudia Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Zuberi Kabwe akiachia ngazi baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kumfukuza uanachama. Zitto amefukuzwa uanachama ukiwa mwendelezo wa harakazi na misigishano ya ndani kwa ndani, kubwa likiwa ni kugombea madaraka.

Zilianza kama tetesi, baadae ikathibitika kuwa Zitto akiwa na kundi lake la Profesa Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Mkoa wa Arusha waliandika waraka wa kumhujumu Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe. Hawa walitaka Mbowe asigombee uenyekiti wa CHADEMA kwa mara ya tatu.

Sitanii, sina haja ya kurejea waraka ule, ila niliandika makala wakati huo nikasema waraka ule pamoja na nia yake njema au harakati ndani ya chama, ulikuwa chini ya kiwango. Nilipata tabu zaidi, Profesa Kitila alipokiri kuhariri waraka ule. Ulijaa matusi, ulikosa staha na ulijengwa katika mkakati dhaifu kwa kumtukana Mbowe kama Mbowe badala ya kulenga mfumo na Katiba ya chama.

Ajenda ya akina Zitto, ni mwendelezo wa mnyukano ndani ya CHADEMA. Mnyukano huu ulianza pale aliyekuwa Diwani wa NCCR-Mageuzi, Rasta Chacha Wangwe alipohamia CHADEMA na Udiwani wake pale Tarime, kisha akaanzisha hoja ya ruzuku kupelekwa mikoani. Hilo ndilo lilikuwa chimbuko la mgogoro wa Wangwe na Mbowe.

Nakumbuka mwaka 2004, tulipokwenda Tarime na Mbowe, Philemon Ndesamburo, Jomba Coy, Jacob Nkomola, Shaibu Akwilombe, Grace Kiwelu na wengine kadha wa kadha. Pale Musoma tulimkuta Mwenyekiti wa CHADEMA aliyetambulishwa kwa jina la Mama Vivian. Wakati huo nilikuwa Mhariri Mkuu wa Gazeti la Tanzania Daima.

Kimsingi huyu mama Vivian hakuwa na ofisi ya kueleweka ya CHADEMA. Chacha Wangwe akajitolea kutumia ofisi ya NCCR kukijenga CHADEMA, kwani mbali na kuwa Diwani wa Tarime Mjini ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa NCCR Mkoa wa Mara. Alipendwa mno Chacha, lakini alipodai ruzuku, hali ya hewa ikachafuka. Akina Nkomola waliomuunga mkono, waliishia kunaswa kibao. Wakaitema CHADEMA.

Sitanii, si nia yangu leo kuandika CHADEMA imetokea wapi, ila nimeguswa na Katiba ya CHADEMA iliyotumika Kumuondoa Zitto katika ubunge. Ni vyema nikainukuu Kanuni, ambayo ni sehemu ya Katiba ya CHADEMA, iliyomuondoa Zitto kisha niendelee na mjadala wangu. Kanuni hiyo inasomeka hivi:

SEHEMU B:

KANUNI ZA KUSIMAMIA SHUGHULI, MWENENDO NA MAADILI YA HALMASHURI ZILIZO CHINI YA CHADEMA

8.0. HATUA ZA KINIDHAMU KWA WABUNGE, MADIWANI, WENYEVITI WA VIJIJI/MITAA NA VITONGOJI

UTANGULIZI:

Wabunge, Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji/Mitaa na Vitongoji katika Chama, ni sauti za Chama Serikalini na ni nyenzo za kuweza kutafsiri Sera na Ilani ya Chama kwa vitendo Serikalini. Ni makada wa kuonyesha misimamo ya Chama katika mambo mbalimbali yahusuyo nchi yetu kwa kutumia majukwaa yao kwa mujibu wa nafasi zao.

Ni watu ambao umma umewapa dhamana kubwa kwa heshima yao na heshima ya Chama chetu. Kwa hiyo ni wajibu wa Chama kuwaheshimu, kuwalinda na kuwasaidia kutimiza majukumu na wajibu wao kwa Chama na kwa umma kwa uhuru na kujiamini kwa kufuata taratibu zilizopo kwa mujibu wa Katiba ya Chama.

(a) WABUNGE & WENYEVITI WA HALMASHAURI:

Ili hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya Mbunge au Mwenyekiti wa Halmashauri hatua zifuatazo zinatakiwa zifuatwe:-

i. Malalamiko juu ya utovu wa nidhamu au jambo lolote linalolalamikiwa yafikishwe kwenye kikao cha Kamati Kuu kwa maandishi kupitia ofisi ya Katibu Mkuu.

ii. Kamati Kuu bila kulazimika kuita pande zinazohusika, itajadili mantiki ya lalamiko na kuona kama kuna hoja ya msingi katika lalamiko husika.

iii. Kamati Kuu ikiridhika kuwa kuna hoja ya msingi itaunda Kamati ya watu kati ya 5 na 7 ili kuchunguza suala linalo lalamikiwa kwa kuwapa hadidu za rejea.

iv. Kamati katika uchunguzi wake italazimika kuwaita walalamikaji na mlalamikiwa na kuwahoji juu ya suala husika na kupata ushahidi wa pande zote.

v. Kamati hiyo haitakuwa na uamuzi wowote juu ya suala hilo bali itaandika taarifa ya uchunguzi na kutoa mapendekezo kwa Kamati Kuu.

vi. Kamati Kuu baada ya kupokea mapendekezo hayo inawezi kuchukua hatua za dharura kama itaona inafaa juu ya suala hilo ili kunusuru Chama kama kuna hali ya kutishia hatima na uhai wa Chama, na kupendekeza hatua za mwisho kwenye Baraza Kuu.

vii. Baraza Kuu litatoa uamuzi juu ya suala hilo bila kulazimika kuita pande zinazohusika na kuruhusu hatua ya rufaa kwenye Mkutano Mkuu.

viii. Kama upande wowote katika kesi hiyo haukubaliani na uamuzi wa Baraza Kuu utakata rufaa kwenye Mkutano Mkuu, lakini kwa wakati wote kabla ya rufaa yake kusikilizwa upande huo ukubali na utii maamuzi ya Baraza Kuu. Kushindwa kufanya hivyo litakuwa ni kosa la kinidhamu ambalo adhabu yake ni kubatilisha (kutupwa) kwa rufaa yake.

ix. Mkutano Mkuu utakuwa na maamuzi ya mwisho kwa jambo lolote na pande zinazo husika ni lazima zitii maamuzi ya Mkutano Mkuu. Mtu yeyote atakayeshindwa kutii uamuzi wa Mkutano Mkuu atakuwa anatofautiana na Chama na kuanzia saa hiyo uanachama wake utakuwa umekoma.

x. CHADEMA itashughulikia matatizo ya viongozi na wanachama kwa kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba ya Chama, wala hata siku moja haitashughulikia mambo kama hayo Mahakamani. Mwanachama atakayeshindwa kufuata taratibu na ngazi za Chama hatavumiliwa na atafukuzwa uanachama.

xi. Upande wowote unaohusika na mgogoro unaweza kuomba kuitwa na kikao chochote kinachoshughurikia suala hilo ili kuota ufafanuzi zaidi.

Kanuni ya 8 (x) ya Kanuni za Kusimamia Shughuli, Mwenendo na Maadili ya Halmashuri Zilizo Chini ya CHADEMA, inamzuia mbunge yeyote kwenda Mahakamani kudai haki yake. Adhabu ya mtu kutafuta haki yake mahakamani ni kufukuzwa uanachama. Kanuni ya 8 (xiii) pia inamtaka Mwanachama kutii maamuzi ya Baraza Kuu hata kama ameonewa.

Hapa maana yake ni nini? Baraza Kuu linaloongozwa na Mwenyekiti hata kama litaamua kukuonea, kwa mujibu wa Kanuni hii unapaswa kukubaliana na uonevu huo. Ukishindwa kufanya hivyo, basi hata rufaa yenyewe itatupwa haitasikilizwa. Mkutano Mkuu wa CHADEMA pia utakuwa na maamuzi ya mwisho yasiyohojiwa kokote.

Sitanii, katika sheria kuna Kanuni tunazoziita Kanuni za Kujivua Uwajibikaji (Exemption clauses). Kanuni hizi ni sawa na kwenda kwenye hoteli au nyumba ya wageni, ukaambiwa “Hoteli haitahusika na wizi utakaotokea kwenye gari lako uliloegesha nje au haitahusika na wizi utakaotokea kwa bidhaa za thamani utakazoziacha chumbani.”

Kimsingi hizi ni kanuni za kujifurahisha tu. Kama sheria ya nchi ingeruhusu hali kama hiyo bila kudhibitiwa, basi watu wangejenga nyumba za wageni au hoteli nzuri, kisha wakaajiri magenge ya wezi. Ukiegesha gari, ukirudi hulikuti. Ukiingia na begi zuri, ukitoka nje ya chumba unakuta nguo zimechambuliwa nzuri zimechukuliwa na umeachiwa taulo tu.

Ni katika misingi hiyo, mahakama zilipewa mamlaka ya asili (inherent powers) kutafsiri sheria (kanuni) zilizotungwa na taasisi, mamlaka au watu binafsi, iwapo zimetungwa kisheria na hazikiuki sheria za nchi au sheria mama, Katiba.

Ibara ya 107A (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inasema wazi kuwa  “Mamlaka yenye kauli ya mwisho katika utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa ni Mahakama.”

Sitanii, CHADEMA kimesajiliwa kwa mujibu wa Ibara ya 20 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayosema: “Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani, na hasa zaidi kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.”

Ni kwa msingi huo, uwapo wa CHADEMA unatokana kwa kiasi kikubwa na Katiba ya Tanzania. Ibara ya 64 (5) ya Katiba ya Tanzania inasema bayana kuwa sheria yoyote itakayotungwa katika nchi hii, ikikiuka Katiba kwa mfano kumzuia mtu asitafute haki yake mahakamani kinyume na Ibara ya 107A(1), sheria hiyo au kanuni hiyo itakuwa batili kwa kiwango inachokiuka Katiba ya Tanzania.

Mpendwa, msomaji huhitaji kuelezwa ubatili wa kanuni hii ya CHADEMA. Misingi ya haki na mgawanyo wa madaraka imeasisiwa rasmi kuanza Novemba 14, mwaka 1616, wakati Mwanasheria Mkuu wa Uingereza wakati huo, Sir Edward Coke, alipomzuia Mfalme James II kutoza wananchi kodi bila kupitia bungeni. Mfalme James II alikasirika akamfukuza ujaji mkuu Sir Coke, lakini tangu mwaka huo, yakatokea mabadiliko makubwa.

Sir Coke aligombea ubugne kwa tiketi ya upinzani akaingia katika Bunge la Uingereza, na tangu wakati huo akapigania sheria ya Haki za Binadamu (Petition of Rights – 1628), ambayo pamoja na mambo mengine iliondosha madaraka ya mfalme kutoza kodi Waingereza bila kupitia bungeni, kisha Mfaransa Charles Montesque katika karne ya 18 akaendeleza kazi ya Jaji Mkuu Coke kwa kuanzisha mgawanyo wa madaraka (Separation of Powers).

Dhana hii tunayoitumia hadi leo ya Bunge kutunga sheria, Mahakama ikazitafsiri na Serikali ikazisimamia, iliepusha mianya ya ubabe, ukandamizaji, na ufalme. Kwa ufupi, CHADEMA, chama kinachokua kwa kasi kubwa, kinataka kusema kikiingia madarakani kitarudisha mahakama zinazoitwa Kangaroo. Kwamba ndani ya chama watahukumu kila kitu, na mahakama zote zitafungwa.

Sitanii, ikiwa hili ndilo napata tabu. Misingi ya utawala bora na demokrasi haikubaliani na Katiba ya aina ya CHADEMA. Kama alivyosema Zitto kuwa aliijua Kanuni hiyo, na ukasema mkondo wa kumfukuza kama angeamua kuwasumbua ulikiukwa, basi nadhani wakati umefika kwa CHADEMA kuondoa doa hili, kwa misingi kwamba demokrasi kinayoipigia chepuo na hasa ukirejea jina lake kuwa ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ionekane kufanya kazi ndani ya chama.

Haiwezekani katika karne hii na siasa za ushindani tukawa na chama ambacho kinazuia watu wake kupata haki mahakamani. Hii ni kurejesha usulutani, udikiteta na wakati mwingine hatari ya mtu mmoja kufanya uamuzi mzito unaoweza kuliangamiza taifa hili. Nasema, CHADEMA rekebisa kanuni hii, vinginevyo mtajiondolea heshima katika jamii.