Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeeman Mbowe amewataka viongozi wa CHADEMA wa mikoa yote nchini kujipanga kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kushiriki maandamano yanayotarajia kufanya Septemba 23, mwaka huu.
Mbowe ameyasema hayo katika mkutano wa CHADEMA uliofanyika katika ofisi zao Mikocheni jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku chache baada ya mazishi ya aliyekuwa mjumbe wao wa sekretarieti, Ali Mohamed Kibao.
“Nimetangaza hadi kufikia Septemba 21, 2024 tunategemea tuone hatua za watu kuwajibika kuwarejesha waliotekwa na viongozi kadhaa kujiuzulu, kama hawatochukuliana hatua wenyewe kwa wenyewe sisi kuanzia Septemba 23, 2024 Jiji lote la Dar es Salaam kila kata kila Mlmtaa, wawe tayari.
“Ndugu zangu tumekuwa tunafanya utani mara nyingi ‘this time around’ hatuna utani, kuanzia Jumatatu Septemba 23, 2024 sisi tutaingia barabarani kudai uhai wa watu wetu waliopotezwa ‘unless’ Serikali ichukue hatua za haraka na za makusudi kuwarejesha , watu, kujiuzulu na watu wote kuwajibika” amesema.
Aidha Mbowe amesema kabla ya maandamano hayo kamati kuu ya CHADEMA itakutana Septemba 16 na 17 kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ikiwemo utekaji, mauaji na kupotea kwa viongozi wao.