Katika toleo la leo tumechapisha habari zinazoonyesha kuwa kuna mgogoro mkubwa unaofukuta ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Mgogoro huu unatajwa kutokana na makundi makubwa matatu yenye kutaka ukuu ndani ya chama hicho. Kundi la kwanza ni la Mwenyekiti Freeman Mbowe. Kundi hili linadaiwa kuukodolea macho urais baada ya kuona kuwa Chadema sasa inakubalika.
Kundi la pili ni la Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Slaa. Kundi hili linajinasibu na mafanikio yaliyopatikana ndani ya Chadema kwa chama hicho kukubalika ndani na nje ya nchi. Kundi hili linampima mafanikio kiliyowahi kupata chama hicho tangu kisajiliwe kwa kigezo cha idadi ya wabunge, madiwani na kura zilizopatikana Dk. Slaa alipogombea urais mwaka 2010.
Kundi la tatu ni la Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe. Kundi hili limekuwa likisema wazi kuwa linafanya hadi harakati za kubadili Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumruhusu Zitto agombee urais. Zitto atakuwa na umri wa miaka 39 ifikapo 2015 na Katiba inataka mgombea urais awe na umri wa miaka 40 na kuendelea.
Tumeshuhudia mgogoro huu kidogo umeanza kuwa hadharani. Baadhi ya wanachama wanatimuliwa na wao wanasimama na kudai wanaanika uozo wa Chadema. Hofu yetu ni kwamba malumbano haya yaliyoanza kidogo ndani ya chama hiki na sasa kufikia hatua hii yanaweza kuhitimisha matumaini ya Watanzania.
Watanzania wengi kwa sasa wameonyesha imani kubwa kwa Chadema. Chama hiki kinaweza kuwa na matatizo ya hapa na pale, lakini kimsingi kimejipambanua na vyama vingine vya siasa hapa nchini. Kupitia Operesheni Sangara na Movement for Change (M4C), Chadema ni chama pekee kilichoweza kukikosesha usingizi chama tawala.
Ndani ya CCM sasa matumbo ni ya moto. Tumeshuhudia katika Mkutano Mkuu uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, CCM wameteka nyara hoja za Chadema ikiwamo kushusha bei ya mabati, saruji, ada katika shule binafsi, kodi za pango, mapambano dhidi ya rushwa na kuangalia uwezekano wa kuwapatia mikopo wanafunzi wote wa elimu ya juu.
Chadema kimekuwa chama pekee kinachojenga hoja kikaeleweka mbele ya jamii na kutikisa mizizi ya CCM. Tunapata masikitiko makubwa kusikia wakubwa ndani ya chama hiki wanagongana. Kugongana kwao ni faida kwa CCM maana wataishia kugawanyika na kusambaratika kama ilivyotokea kwa NNCR-Mageuzi na hatimaye Tanzania Labor Party (TLP).
Sisi hatuna chuki na CCM, lakini kamwe hatuwezi kufurahia CCM kuwa chama pekee chenye nguvu hapa nchini bila kuwapo chama cha upinzani chenye nguvu kama Chadema. Chadema kimekwishaleta matumaini kuwa kinaweza kubadili sura ya mchezo wa siasa hapa nchini na maendeleo tunayotaka kwa ajili ya wananchi yakaja kwa kasi.
Tunawasihi viongozi wa chama hiki kukaa chini na kujadili njia bora ya kumaliza mgogoro huu. Madaraka ni suala la mpito ila matumaini ya Watanzania ni ya kudumu. Chondechonde Mbowe, Dk. Slaa na Zitto malizeni tofauti zenu bila kufikiri hata kufukuzana. Siku zote hakuna bahari isiyokuwa na mawimbi. Tunataraji mmetusikia na mtamaliza mgogoro huu kwa nia ya kutoua matarajio ya Watanzania.
Mungu ibariki Tanzania.