Raia wa Chad walipiga kura hapo jana katika uchaguzi mkuu ambao serikali imeusifu kuwa ni hatua muhimu ya mpito wa kisiasa, baada ya miaka mitatu ya utawala wa kijeshi.

Hata hivyo uchaguzi huo ulishuhudia idadi ndogo ya wapiga kura huku upinzani ukitoa wito wa kuususia kutokana na madai ya udanganyifu.

Rais Mahamat Idriss Deby Itno, alichukua madaraka mwaka wa 2021 baada ya kifo cha babake, ambaye alikuwa aliiongoza nchi hiyo kwa miongo mitatu na kisha kushinda katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Mei mwaka jana ambao wagombea wa upinzani waliukosoa kuwa ulikumbwa na udanganyifu.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Transformers alisema wapiga kura walisikia mwito na wengi wao wakasalia majumbani mwao. Vituo vya kupigia kura vilifuatiliwa na karibu waangalizi 100 wa kigeni na wawakilishi wa vyama vya kisiasa.