Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar
Chama cha Mapinduzi CCM Zanzibar kimetoa wito kwa Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Juma Duni Haji, kurejea Chama cha Mapinduzi ili kuendelea kulinda heshima yake kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kupigania Demokrasia Zanzibar na Tanzania kwa Ujumla.
Wito huo umetolewa na Katibu wa Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar. Khamis Mbeto Khamis, wakati akikabidhi msaada wa vifaa vya ujenzi na vifaa vya watu wenye ulemavu Mkoa wa Kusini Pemba vilivyotolewa na Mbunge wa Viti Maalum (UWT) Mkoa wa Kusini Pemba Mhe. Zulfa Mmaka Omar.
Mbeto amesema sio busara kuona hali inayoendelea kwa sasa ndani ya Chama cha ACT Wazalendo kushindwa kumpa heshima inayostahili Mzee Duni kama ambavyo Chama hicho kimetoa heshima kwa wazee waliopita ikiwemo Maalim Seif Sharif Hamad,Mzee Shabani Khamis Mloo na wegineo hivyo njia pekee ya Mzee Duni kulinda heshma yake kwenye siasa ni Kurudi nyumbani CCM.
“Haiwezeka mtu mwenye historia kubwa ya Chama cha CUF na ACT Wazalendo leo anakwenda kugombea kipindi chake cha pili cha Uongozi wananchukulia fomu na kumdhihaki hadharani hivi kweli ni haki? Njoo CCM Mzee Duni tukulindie heshma yako”
Katika hatua nyengine Mwenezi Mbeto amekitaka Chama cha ACT Wazalendo kujitathmini katika kulinda heshima ya Viongozi wao ikiwemo Mzee Duni kutokana na muda wake mwingi walioutumia katika kupambania ukuaji wa demokrasia ambao kwa sasa vingozi wengi vijana ndio wanufaika wakubwa wa Hali nzuri ya kisiasa tunayoendelea kuishuhudia Zanzibar.