Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa onyo kwa watia nia wote wanaoanza kujipitisha kwenye majimbo na kata mbalimbali na kutoa chochote kwa wajumbe ili wawaunge mkono kwenye kinyang’anyiro cha uteuzi ndani ya chama.
Onyo hilo limetolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Steven Wasira alipokuwa akiongea na Viongozi na wanachama wa CCM kwa nyakati tofauti Wilayani Sikonge na katika mkutano wa hadhara Mjini Tabora.
Alisema kuwa CCM ni Chama cha wananchi wote, wenye fedha na wasio na fedha, na hakichagui au kuteua viongozi kwa kuangalia uwezo wao wa kifedha, bali kinatoa nafasi kwa wanachama kuchagua kiongozi wanayemtaka.

‘Tunazo taarifa za wale wote ambao wameshaanza kujipitisha kwa wananchi na kuwapatia fedha, chama kitawashughulikia, tunataka kiongozi atakayechaguliwa awe chaguo la wananchi na sio anayemwaga fedha’, alionya.
Makamu Mwenyekiti aliwataka wale wote wanaotaka udiwani na ubunge kwa kutoa rushwa kutumia fedha hizo kununua zao la tumbaku ili kunufaisha wakulima na sio kutoa rushwa ili wananchi wawaonee huruma na kuwachagua.
‘Hatuhitaji wabunge na madiwani wanaonunua vyeo, tunataka wale walio chaguo la wananchi ambao wataenda kuwatumikia kwa moyo mmoja, kusikiliza kero zao na kuzifanyia kazi na sio kwenda kujinufaisha, hawa hatuwataki’, alisema.
Alisisitiza kazi kubwa ya CCM kuwa ni kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa wananchi katika sekta zote, ndiyo maana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan baada ya kuingia madarakani alikuja na na kauli mbiu ya KAZI IENDELE.
Kauli hii ni mwendelezo wa kauli mbiu ya HAPA KAZI TU iliyoanzishwa na mtangulizi wake Rais Dkt John Pombe Magufuli aliyetwaliwa na Mungu mwaka 2021, hii ikimaanisha kwamba CCM itaendeleza mazuri yote yaliyoanzishwa.
Wasira alidokeza kuwa CCM ni chama cha ukombozi chenye misingi imara kuanzia ngazi za chini kwa mabalozi wa nyumba kumi, ndiyo maana kimeendelea kuwa chaguo namba 1 kwa watanzania na kuwaletea maendelea makubwa.
Alibainisha kuwa CCM imejengwa katika misingi ya haki na amani hivyo kitaendelea kusimamia hayo na hakitaruhusu mtu au kikundi fulani cha watu kuvuruga amani iliyopo nchini.