Na Mwandishi Wetu

Mchungaji Peter Msigwa, ambaye awali alihusishwa na tetesi za kurejea chama chake cha awali, Chadema, amepewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) jukumu muhimu la kupigania ushindi wa chama hicho katika Kanda ya Nyasa.

Akihutubia maelfu ya wanachama wa CCM mjini Iringa, Katibu wa NEC, Itikadi, Mafunzo na Uenezi wa CCM, CPA Amos Makalla, aliweka wazi kuwa wale waliodhani kuwa Msigwa angerudi Chadema walikuwa wanapoteza muda. Alisisitiza kuwa Msigwa ni “mtoto wa Chama cha Mapinduzi,” na hana mpango wa kurejea upinzani.

Akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika leo katika uwanja wa Mwembetogwa, CPA Makala alikosoa vikali kauli za wapinzani kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, akiwataja kuwa wanaangalia zaidi maslahi yao ya kisiasa badala ya ustawi wa wananchi wa kawaida, wakiwemo wakulima, wafugaji na makundi mengineya kijamii.

Akitoa elimu kuhusu mabadiliko ya sheria za uchaguzi, Makala alieleza kuwa mchakato wa maboresho ya sheria umezingatia maoni ya wananchi, hatua iliyochangia kupitishwa kwa sheria mbili muhimu:

Alitaja sheria ya kwanza kuwa ni ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, inayotoa nafasi kwa wananchi wenye sifa kuomba nafasi kwenye tume hiyo kupitia mchakato wa uteuzi uchini ya Jaji Mkuu na Jaji wa Zanzibar.

Aliizungumzia sheria ya pili kuwa ni ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge, na Madiwani, inayowaondoa wakurugenzi wa halmashauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo yao na hakuna mgombea anayepita bila kupingwa.

“Kama katika mazingira ya maboresho ya sheria hizi za uchaguzi Chadema wanataka kususia uchaguzi ujao, huo ni uamuzi wao, lakini uchaguzi utaendelea kwa mujibu wa Katiba, si kwa matakwa ya CCM,” alisema.

Aidha, alitetea uamuzi wa CCM wa kumteua Dkt. Samia Suluhu Hassan mapema kama mgombea wa urais, akisema ni uamuzi wa chama na si wa mtu binafsi. Aliwataka wapinzani kutambua kuwa Chadema haina maandalizi wala rasilimali za kushiriki uchaguzi mkuu, na iwapo watasusia, hilo litakuwa anguko lao kisiasa.

Alisema; “endapo Chadema itaendelea kususia uchaguzi, inaweza kupoteza kabisa nafasi yake kama chama kikuu cha upinzani nchini.”

“Najua kesho watakua hapa Iringa na kama kawaida yao watakuja kututukana. Mimi nisema niko tayari kubeba matusi kwa niaba ya CCM, leteni mawe kwangu, nipo tayari,” alisema kwa ujasiri.

Katika hatua nyingine aliyekuwa Katibu wa Chadema jimbo la Iringa Mjini, Paschal Chibala amejitoa katika chama hicho na kujiunga na CCM.

Akipokelewa na Makala katika mkutano huo Chibala alizungumzia maendeleo makubwa yaliyoletwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan mjini Iringa na Tanzania kwa ujumla kwamba ni sehemu ya sababu iliyompeleka CCM.