Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)Fadhili Maganya amesema Chama hicho kinajivunia miaka 48 ya kuzaliwa kwake ambapo maadhimisho yake yanatarajiwa kufanyika Februari 5 mwaka huu Jijini Dodoma kwa kuanza na kongamano Februari 2 mwaka huu.

Mwenyekiti huyo ameeleza hayo leo January 30,2025 Jijini hapa wakati akizungumza na Waandishi wa Habari akiwa ameongozana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi,Ally Hapi na kueleza kuwa Amani, upendo na ushirikiano ndiyo nguzo pekee inayowaweka pamoja.

Amesema kongamano hilo litashirikisha wadau mbalimbali na kushirikisha mada mbalimbali na watajadiliana kwa pamoja inapotoka,ilipo na iendapo CCM.

“Natumia fursa hii kuwaomba wanadodoma wafuatililie vyombo vya habari,tumeanza kama Wazazi na Jumuiya zingine zinafanyika,”amesema Maganya.

Ametaja mada zitakazowasilishwa ni pamoja na malezi,mchango wa CCM katika maendeleo ya Taifa,mchango wa Dk Samia Suluhu Hassan katika kuijenga CCM,mchango wa vijana na elimu katika maendeleo.

Mwenyekiti huyo amesema CCM tayari imepata wagombea wake lakini Chadema yenyewe bado inatibu vidonda na majeraha ya uchaguzi wao.

“Tayari tumepata mgombea sisi tumejiandaa na uchaguzi,tunaendelea kujiandaa yapo yanazungumzwa na upinzani wala sisi hatuna wasiwasi hakuna sehemu imetulia kama sasa hivi,wao wamemaliza wakaanza kutibu vidonda na majerehe.

“Tunakwenda kufanya vizuri katika uchaguzi na wala hatuna shaka katika hili,”amesema Maganya.

Hali kadhalika Maganya ametumia nafasi hiyo kupiga dongo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kudai uchaguzi wa kuwapata viongozi wa juu wa Chama hicho umewaachia vidonda,majereha na makovu yasiyoisha hivyo hawana shaka watashinda kwa kishindo katika uchaguzi Mkuu mwaka huu.

Ikumbe haya yanatokea ikiwa hivi karibuni Chadema ilifanya uchaguzi wa kuwapata viongozi wa juu wa Chama hicho ambapo Tundu Lissu aliibuka na ushindi katika Nafasi ya Mwenyekiti mara baada ya ‘kumgaragaza’ Freeman Mbowe ambaye amekiongoza Chama hicho kwa zaidi ya miaka 20.