Kiongozi wetu Mkuu anaendelea na ziara ya kuwaaga marafiki wetu wa maendeleo.
Anazidi kuongeza idadi ya safari na siku alizokaa ughaibuni. Kwa Afrika, amejitahidi kuwaga kwa pamoja pale nchini Afrika Kusini. Lakini kwa Ulaya, Asia na Marekani, naona kaamua kwenda kuaga kila nchi kadri anavyoweza. Hii haishangazi kwa sababu kwa miaka 10 safari zake nyingi zimekuwa za Ulaya, Marekani na kidogo Asia.
Wakati akiendelea kuaga, huku nyumbani ni kama karuhusu wasaidizi wake wagawane kila kinachowezekana. Hadi Rais mpya atakapoapishwa, nchi hii itakuwa imesalia mifupa mitupu. Hali ya mambo katika Wizara zote ni mbaya kifedha na kiuongozi. Sijui kama Makatibu Wakuu wanaweza “kufanya makosa” kushindwa kutumia fursa hii.
Wizara kama ya Maliasili na Utalii, kule TANAPA hakuna Bodi ya Wakurugenzi kwa hiyo uchotaji fedha unaofanywa na Katibu Mkuu na Waziri wake, ni mambo yasiyo na mjadala.
Hadi Jumamosi iliyopita, mawaziri 13 walikuwa kwenye harakati za kutafuta wadhamini mikoani. Wote wanausaka urais. Hii ina maana kwa kipindi chote hiki kuna kazi nyingi za mawaziri hao zitakuwa zimekwama. Wananchi wanahoji imekuwaje mawaziri hawa walipoingia kwenye harakati hizi hawakujiuzulu ili kuondoa mgongano wa maslahi na matumizi mabaya ya mali za umma.
Mawaziri karibu wote ukiwasikiliza, ni kama wanasema mkubwa wao amefeli. Tunasikia kauli za mapambano dhidi ya rushwa, ajira, kutokomeza ujambazi na ajali, na kadhalika.
Wote wamesimama kuwaahidi wana CCM na Watanzania kwamba endapo watachaguliwa vita dhidi ya mambo hayo ndiyo itakayopewa kipaumbele. Wanatumia lugha ya staha, lakini ukiketi nao faragha wanasema bwana mkubwa amefeli mengi.
Lakini wakati wakijinadi kwa namna hiyo ya kumponda kirejareja mkubwa wao, mkubwa mwenyewe amejitokeza kwa Watanzania (pengine wasioijua Tanzania) huko India na kutamba kuwa amefanikiwa kwenye mapambano dhidi ya rushwa. Rais anajua kauli kama hiyo inawaingia hao ndugu zetu wa ughaibuni, ndiyo maana kaamua kuisemea huko. Hapa nchini akithubutu kusema hivyo, atakutana na miguno na mbinja.
Ukiingia kwenye tovuti ya Takukuru, kinachoonekana kwenye orodha ya wala rushwa ni majina ya watendaji wa vijiji (VEO), watendaji wa kata (WEO), mgambo wa vijiji na watu wa kada hiyo. Huwezi kukutana na majizi yaliyokubuhu kwenye wizi wa mafuta, ununuzi serikalini, mawaziri watoa leseni kwa marafiki zao; na kadhalika.
Rais Kikwete anasema ndiye aliyeasisi kujadiliwa kwa Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Haya, tukubaliane naye katika hilo. Sasa tumuulize, huo mjadala bungeni umesaidia kuwabana wezi na mafisadi wangapi? Wangapi wametajwa kwenye ripoti, na wangapi wamekamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria? Wangapi wametiwa hatiani?
Ripoti ya CAG kila mwaka inaihimiza Serikali izingatie kitu kinaitwa thamani ya fedha (value for money). Hilo amelifanya? CAG amepinga kwa nguvu zote uteuzi wa wabunge kwenye Bodi za Mashirika ya Umma. Hilo limetekelezwa? Naibu Spika ni Mjumbe wa Bodi ya Ngorongoro. Analipwa vizuri mno. Huyu ataruhusu mjadala bungeni unaohusu ufisadi wa Waziri Lazalo Nyalandu aliyemteua?
Wajumbe wa Bodi kama ile ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, juzi walikomba mabilioni ya fedha kutoka TANAPA na Ngorongoro kwa maelekezo ya Waziri wa Maliasili. Wakaundiwa safari yenye malipo manono. Lengo lilikuwa bajeti yake ipitishwe. Rais haya anayajua. Anajua hii ina kila dalili na sifa ya kuitwa rushwa. Amefanya nini kulinda fedha za umma?
Rais huyu huyu anajua ndiye aliyebeba uamuzi wa kufikishwa mahakamani kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ngorongoro, Mzee Pius Msekwa, kwa ufisadi wa kutisha ndani ya Mamlaka hiyo. Maelezo yote ya ufisadi yako hadharani. Ripoti ipo. Je, anapowaeleza ndugu zetu wa India kuwa amefanikisha mapambano ya rushwa, nafsi yake inamweka katika hali gani?
Je, si katika utawala wake ambako wezi wa fedha za umma wamejulikana, wamefuatwa, wakaombwa warejeshe fedha na mambo yakaishia hapo? Wapi kwenye nchi yenye uongozi makini katika ulimwengu huu ambako mwizi anakuwa na fursa ya kujadiliana na Serikali na mwisho akaachwa atambe? Haya ndiyo mafanikio anayojivunia?
Rais huyu huyu anawajua watu walioshiriki kujitwalia shirika la umma la UDA. Anamjua rafiki yake aliyeingiziwa shilingi milioni zaidi ya 300 kwenye akaunti yake. Mwisho wa siku, Rais anajua namna kesi hiyo ilivyofutwa. Kuna maneno mengi yanazungumzwa juu ya uhusiano wa kufutwa kwa kesi hiyo, wanunuzi wa UDA na familia ya Rais. Haya yanasemwa pembeni sasa, lakini huenda muda haupo mbali –akishastaafu -mambo mengi yakawekwa bayana.
Rais Kikwete ameshajiuliza kwanini Bandari haina mchango wa maana kwenye uchumi wa Taifa letu? Je, watu walioongoza Bandari akiwamo Madeni Kipande, mambo waliyoifanyia Bandari kweli wangestahili leo kuwapo mitaani au Keko?
Rais anaposema amepata mafanikio kwenye vita dhidi ya rushwa anawaambia nini Watanzania maskini wanaokosa huduma Polisi, Mahakama na Hospitali kwa sababu ya rushwa?
Je, hivi kweli kwa miaka 10 aliyokuwa madarakani ameshasahau vilio vya wananchi makabwela wanaokufa kwa kukosa huduma muhimu kwa sababu ya rushwa? Hawaoni mamia ya Watanzania maskini wanaoangua vilio kwenye mikutano ya Waziri wa Ardhi, William Lukuvi, kwa sababu ya kudhulumiwa ardhi zao?
Kwa miaka 10 Rais ameshindwa kumaliza mgogoro katika eneo la Loliondo. Anazo taarifa za namna NGOs zinavyohonga na kuvuruga amani katika eneo hilo. Oktoba au Novemba anaondoka Loliondo ikiwa kama sehemu ya Kenya. Imevamiwa na wageni kiasi cha kuifanya isitawalike. Yuko kimya.
Amezungumza kuhusu suala la ajali. Alichoendelea kukifanya, kama walivyo wasaidizi wake, ni kulalamika. Eti anasema ajali ni nyingi kwa sababu madereva wanakunywa viroba. Akatoa mfano wa pale Chalinze.
Kama Rais anajua Chalinze na sehemu zote za barabara kuna viroba vinauzwa na madereva wanavitumia, kitu gani kimemkwaza kumaliza chanzo hicho cha ajali? Amemwajibisha Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kushindwa kukabiliana na chanzo hicho cha ajali?
Kama Rais anashuhudia Watanzania 40 wanakufa katika ajali, halafu anashindwa au anapuuza kwenda eneo husika ili kuonyesha kuguswa na jambo hilo, nani ataamini kuwa Rais ana dhamira ya kupunguza ajali? Juzi akiwa ng’ambo Watanzania 23 wamekufa ajalini Iringa. Wala hakuona sababu ya kukatiza safari ili kuzililia roho hizi za watu wake. Ameendelea kufaidi ziara kana kwamba hakuna tatizo zito nyumbani. Juzi, pale Marekani mbaguzi mmoja Mzungu kaua Waafrika tisa kanisani. Rais Barack Obama kalibutubia Taifa juu ya jambo hilo. Ule umekuwa msiba wa Taifa. Sisi hapa wanakufa watu 23, wanakufa watu 40 katika ajali Rais hashituki. Tunashangaa nini watia nia wanapojitokeza wengi wakiwa na dhamira ya kufuta aina hii ya uongozi.
Anaposema ndani ya miaka 10 magari milioni 1.5 yameongezeka kwenye idadi ya magari milioni 1.7 yaliyokuwapo wakati akiingia madarakani; je, amefanya nini kuweka miundombinu ili kukabilianana hali hiyo? Je, anaondoka akiamini foleni hizi mbaya ni dalili kweli ya maendeleo?
Itoshe tu kusema Rais Kikwete amejitahidi kufanya pale alipoweza. Watanzania watamkumbuka kwa mazuri yake, lakini hawatakoma kumkumbuka kwa kufeli kwake kwenye mambo mengine mengi.
Anaondoka reli ikiwa inachungulia kaburi na aliyehusika sasa anakitaka kiti chake. Anaondoka watoto wa Tanzania wakiendelea kuketi chini ilhali kukiwa na misitu mikubwa ambayo mbao zake zinawafaidisha watu wa mataifa mengine. Anaondoka viwanda vikiwa vinachechemea na vingine vikiwa vimefungwa.
Anaondoka mifuko ya plastiki ikiwa imeipamba miji yetu kana kwamba ni sifa njema. Anaondoka fukwe za umma zikiwa mali za watu binafsi.
Ukiyatafakari haya, kama nilivyosema siku kadhaa zilizopita, unaona wana CCM wengi wamejitokeza kuwania urais, si kwa sababu ni haki yao kikatiba tu, bali ni kwa sababu wanadhani wanaweza kufanya vizuri zaidi yake.
Kinachoendelea ndani ya CCM wenyewe wanasema ni ukuaji wa demokrasia. Kuna ukweli na upotoshaji. Wapo wagombea mapandikizi. Hawana nia ya dhati.
Hao watapambana na wenzao ambao wameingia kwenye urais si kwa sababu ya kusaka sifa au ukwasi, bali kwa ajili ya kurejesha heshima ya Tanzania na ya Watanzania.
Miongoni mwao wamo wenye nia ya dhati ya kuona wanapambana kweli kweli na wala rushwa na wahujumu uchumi. Wamo wenye uwezo na kasi ya kuibadili Tanzania hata ikaweza kufikia kiwango cha kuwa super power katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. Bahati nzuri wana CCM wengi wameshalijua hilo. Kiu ya Watanzania wengi ni kuona nchi inarejeshwa kwenye mstari. Wanataka kuifanya Tanzania iwe ya Watanzania.
Safari hii mizengwe inaweza kuiumiza CCM. Wapinzani wanapaswa kuwa kitu kimoja ili waweze kutumia makosa ya CCM kujiimarisha. Watanzania wako radhi kuamini na kutenda kama Wachina wanaoamini kuwa: “Paka ni paka bila kujali rangi yake, alimradi anakamata panya”.
Watanzania kuiadhibu CCM kwa sababu tu ya kushindwa kukidhi matakwa na kiu yao si jambo la ajabu. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alishawahi kusema: “Watanzania wanataka mabadiliko, wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM.”
Nguvu za dola au ujanja ujanja haviwezi kuwarudisha nyuma Watanzania kumpata kiongozi wanayemtaka. Watu wanataka mabadiliko. Waliwekeza matumaini makubwa mno kwa Rais Kikwete, mwishowe hawakuridhika.
Ndiyo maana wengi wanaamini kuwa endapo CCM hawatagawana mbao safari hii, basi ule usemi wa Mwalimu Nyerere wa “Upinzani wa Kweli Utatoka CCM”, utakuwa na safari ndefu kuufikia.