MADIWANI wa Manspaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro wamemwandikia barua Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakimuomba akubali kusaini makubaliano ya mkopo wa Sh bilioni 19 za ujenzi wa kituo kipya cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi kilichopo eneo la Ngangamfumuni mjini Moshi.

Japhary Michael ni Meya wa Manspaa hii anayesema wanakusudia kuingia ubia na Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) kujenga kituo cha kisasa. Baraza hilo linaongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Chadema kimemwandikia Waziri Mkuu barua mara mbili na kutuma ujumbe wa wataalamu kutoka ndani ya Manispaa na Benki ya TIB, lakini hadi sasa hajajibu maombi yao.

 

Ujenzi wa kituo cha mabasi unalenga kutatua kero ya msongamo wa mabasi kwani kwa sasa mabasi yamekuwa mengi hususani yanayotoka nchi jirani. Meya anasema Baraza limefanya upembuzi yakinifu katika michoro ya ujenzi wa kituo cha mabasi, lakini Mkurugenzi wa Manspaa, Benadette Kinabo anadaiwa kukwamisha mpango huu kuepusha kukipa umaarufu CHADEMA. Anadaiwa pia kukwamisha ujenzi wa kijiji cha michezo kinacholenga kukuza utalii katika uwanja wa Moimoria wenye sifa zote.

 

“Hapa Waziri Mkuu akituidhinishia barua hiyo ni dhahiri wananchi watanufaika na miradi mbalimbali kwani kutakuwepo na hoteli, ofisi na hata biashara mbalimbali kuzunguka kituo hicho,” anasema Japhary.

 

Ukiacha kero ya kituo cha mabasi, wanafunzi 9,828 wanaosoma katika shule za sekondari za Kata Manispaa ya Moshi kwa mwaka 2012/2013 Mkurugenzi wa Manispaa anawawekea mikingamo wasilipiwe ada kwa madai kuwa kuwalipia ada ni kukiuka sera ya elimu ya serikali. Baraza la Madiwani katika Manspaa hii liliahidi kutoa elimu ya bure kwa wanafunzi kwa kutenga shilingi milioni 194 kwa ajili ya kuwalipia ada ya shule wanafunzi hao ili kuweza kupunguzia makali ya maisha kwa wazazi wa wanafunzi hao.

 

Baraza liliazimia kila mwanafunzi atalipiwa ada ya Sh 20,000 hatua hiyo inafuatia wazazi wengi kushindwa kuwalipia ada watoto wao na hivyo kurudishwa nyumbani mara kwa mara na hivyo kuchangia kuporomosha maendeleo ya elimu kutokana na hali ngumu ya uchumi inayowakabili wananchi. Utekelezaji wa sera hiyo ni matokeo ya wadau mbalimbali kujitokeza na kuweka uthubutu katika kuboresha sekta ya elimu nchini na kuwaondoa waananchi katika wimbi la ujinga.

 

Licha ya kuboresha elimu katika Manispaa bado wamefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi milioni 351 kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato ya halmashauri na kwamba Manispaa imeweza kukusanya zaidi ya Sh bilioni 4.5 kwa mwaka. Awali walikuwa wanakusanya chini ya bilioni moja.


Sehemu ya fedha hizo itatumika kuwalipia ada wanafunzi wote na kuongeza matundu ya vyoo katika baadhi ya shule za sekondari zinazokabiliwa na upungufu wa matundu ya vyoo.


Halmashauri hii ilikusudia kuwalipia ada za shule ya sekondari watoto yatima 1,200 na wale wanaotoka katika mazingira magumu, lakini kutokana na umuhimu wa elimu na wazazi wengi kutokuwa na fedha za kuwalipia ada wanafunzi 9,828 nao watalipiwa ada bila ubaguzi.

Mkurugenzi Kinabo ajibu

Kinabo anasema Halmashauri haina bajeti ya kuwasomesha bure wanafunzi hao na kuwa sera hiyo inakinzana na sera ya Serikali Kuu ambapo inatamka wazi kwamba kila mzazi lazima achangie Sh 20,000 isipokuwa watoto yatima.

“Mimi ninatekeleza Sera ya Taifa inayosema asilimia 84 inachangiwa na Serikali Kuu na asilimia 14 inachangiwa na wazazi,” anasema Kinabo.


Kuhusu ujenzi wa kituo cha mabasi, anasema yuko katika mchakato wa kujua gharama halisia za ujenzi wake unaofanywa na wataalamu kutoka Chuo cha Ushirika na Stadi za Biashara Moshi. Anasema hajawahi na wala hana mpango wa kukwamisha ujenzi huo.


Anasema jitihada zake zimeivutia benki ya TIB na mchakato unaendelea, lakini anasikitishwa na lawama na kejeli zinazotolewa na Meya na madiwani kutoka Chadema dhidi yake.


Anasema tangu waingie madarakani mji wa Moshi umeanza kuwa mchafu licha ya kushika nafasi ya kwanza miaka sita mfululizo kitaifa katika usafi wa miji na manispaa nchini.


Kinabo anasema TIB pia inakusudua kutoa mkopo mkubwa kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa la Mbuyuni mjini hapa miradi ambayo ikikamilika itakuwa imetoa mwanya mkubwa ajira na fursa za kibiashara na hivyo kukuza uchumi.


Waafanyabiashara wa matunda na mboga mboga wanalazimika kuweka vijiwe vyao ovyoovyo katika mji wa Moshi kutokana na madiwani wa Chadema kuruhusu wafanyabiashara kuvamia mji nyakati za jioni.

Anasema Mji wa Moshi umeanza kuwa mchafu huku shutuma zote akizielekeza kwa madiwani ambao wanawaruhusu wafanyabiashara ufanya biashara barabarani nyakati za jioni.

Mwandishi wa mahala haya anapatikana kwa namba: 0762 032 296.