Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema wabunge ambao hawakufanya vizuri katika majimbo yao wala kurudi kwa wananchi, wasitarajie msaada wowote kwa kuwa walishapewa nafasi lakini walishindwa kuitumia ipasavyo.

CCM imesisitiza kuwa ili kuhakikisha inapata wagombea ubunge na udiwani wanaokubalika kwa wananchi, imeamua kubadili mfumo wake wa kupata wagombea kwa kupanua wigo wa demokrasia na kuongeza idadi ya wapiga kura.

Hayo yalielezwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira jana wakati akizungumza mjini Tabora katika mkutano wa hadhara akihitimisha ziara yake mkoani humo.

Alisema chama sasa kinataka mgombea ambaye anakubalika na wananchi, ambaye hata akirudi kwao baada ya uchaguzi, atapokelewa kama mmoja wao kwa kuwa hakuwasahau.

“Ukifanya vizuri wananchi wanakukumbuka. Lakini kama ulipewa nafasi ukapotea, halafu ukaja tena kipindi cha uchaguzi na kusema ‘nimerudi nyumbani’ ulikuwa umeenda wapi? Na kwa nini hukuwaaga waajiri wako?” alihoji Wasira.

Alisema CCM haitawasaidia wagombea waliopoteza imani ya wananchi na kwamba mchakato mpya wa kupatikana kwa wagombea utaendeshwa kwa ushirikishwaji mpana ili kuhakikisha wanapitisha viongozi wanaokubalika kwa ngazi ya kata na majimbo.

Wasira alieleza kuwa ifikapo Juni 28 hadi Julai 5, chama kitakuwa tayari kimebaini majina ya wagombea watakaopeperusha bendera ya CCM, huku akifichua kuwa baadhi ya watu tayari wameanza kujipitisha majimboni kwa nia ya kuwania nafasi hizo, jambo ambalo chama kinafuatilia kwa makini.

“Hatufuatilii waliopo tu, hata wa zamani tunawaangalia. Hatupendi watu wanaotumia mbinu za kuzuia wengine kushiriki. Sheria hairuhusu kupita bila kupingwa. Kura ya maoni ni muhimu, hatuwezi kuruhusu mtu mmoja apitishwe bila ridhaa ya wananchi,” alisema.

Alisema kwa sasa wapiga kura kwenye mchujo wameongezeka kutoka mamia hadi maelfu, hivyo haiwezekani tena ‘kununua’ wapiga kura kama zamani. “Huenda hata ukijaribu, utakufa kabla hujawalipa wote,” alitania.

Alikumbusha kuwa Tabora ni miongoni mwa maeneo ambayo hayajawahi kuwa na vurugu na ndipo Mwalimu Julius Nyerere alilia machozi kwa ajili ya amani ya nchi.

Alisema amani hiyo haiwezi kuruhusiwa kuvunjwa na watu wachache wenye ajenda za vibaraka na wakoloni mambo leo.

Wasira alisisitiza kuwa haki ya kweli hupatikana kupitia taasisi rasmi kama Mahakama, ambayo imo ndani ya Katiba. “Kama unadhani hufanyiwi haki, nenda Mahakamani. Huo ndio utaratibu halali, si kuichoma nchi,” alionya.

Alitahadharisha Watanzania kutosikiliza watu wanaotaka kutumia nguvu, kwani hupelekea kuvunjwa kwa haki za wanyonge na kuharibu huduma za jamii kama kliniki, shule, na miundombinu ambayo serikali imewekeza kwa ajili ya wananchi.

Katika hotuba yake nyingine aliyotoa mjini Dodoma, Wasira alisisitiza kuwa CCM itaendelea kuhubiri amani kwa sababu ndani ya amani kuna haki.

Alisema wanaodai kuwa CCM inazungumzia amani bila haki, ni watu wenye mtazamo mgumu kuelewa.

“Wengine wanasema CCM haizungumzi haki. Ukweli ni kwamba, ndani ya amani kuna haki. Amani ikikosekana, wanyonge ndio wa kwanza kuumia na wanawake, watoto, masikini. Tumeona nchi za jirani, watu wake wakikimbilia Tanzania,” alisema.