Wale wa rika langu, ama wamezaliwa, au wamelelewa na sasa wanaelekea kuzeeka ndani ya malezi yenye misingi iliyojengwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Watanzania wengi waliozaliwa kabla ya mwaka 1992 wanaijua CCM, na kwa kweli hawana namna ya kukwepa kuizungumza, kuijadili na wakati mwingine kuikosoa.
Haishangazi kuwaona baadhi ya wanachama na viongozi walio nje ya chama hiki wakiguswa na nyimbo au hotuba zilizotolewa wakati ule ambao Chama kilishika hatamu za uongozi.
Kwa miaka ile, Mtanzania yeyote ili aweze kusoma, kupata kazi na kufanikiwa katika masuala mbalimbali, ilimlazimu awe mwanachama mtiifu wa TANU, ASP na baadaye CCM.
CCM ilijijenga vilivyo kiasi cha kutambulika kama chama dola kwa muonekano na kwa matendo. ‘Athari’ hizo bado zingalipo hadi leo, ingawa zinapungua kadri siku zinavyosonga mbele. Zinapungua kwa sababu kizazi kipya kilichopatikana wakati wa mageuzi ya kisiasa, hakina habari na CCM.
Nimejaribu kuyasema haya kwa ufupi ili maudhui yangu yaweze kueleweka. Najaribu kuipa hadhari CCM dhidi ya wimbi hili kubwa la mabadiliko. CCM wasithubutu kudharau hiki kinachoendelea sasa.
Habari ya wanachama, makada na viongozi kadhaa kuendelea kukihama chama hicho si habari ya kushitua tena masikioni mwa Watanzania wengi. Kila uchao vyombo vya habari vinaripoti habari za wana CCM wanaojiunga vyama vya upinzani. Kama ilivyotarajiwa, CCM wamejitokeza kuwabeza hao wanaohama. Wamewapachika majina mengi tu yakiwamo ya “makapi”, “oili chafu” na mwishoni mwa wiki tumemsikia Mwenyekiti wa CCM Taifa akisema hicho kinachoonekana (wingi wa watu kwenye mikutano ya Ukawa) ni moto wa mabua.
Wapo wanaoshangazwa na kauli hizo. Sijui kwanini wanashangaa. Hivi wao walitarajia CCM wakae kimya? Je, walitarajia wasimame waeleze au waonyeshe woga kwa kitendo cha kukimbiwa na makada wenzao? Haiwezekani. Hizi ni kauli za kisiasa (political statements) ambazo mara zote zimekuwa za kujipa matumaini.
Waziri wa Habari wa iliyokuwa Serikali ya Iraki, Mohammed Saeed al-Sahaf, alikuwa mtu mwenye maneno mengi ya kuwapa matumaini hewa Wairaki dhidi ya majeshi ya Marekani na washirika wake walipoivamia nchi yake.
Kwa mfano, majeshi hayo ya uvamizi yalipotangaza kuwa yameupiga mji wa Baghdad kwa makombora 300, Al-Sahaf mara moja akasimama na kusema: “Tumehesabu makombora na kubaini ni 19; tena yameanguka katika kiji-eneo kidogo tu cha Baghdad.”
Sasa CCM inakimbiwa na wanachama na viongozi, lakini wakubwa wanasimama na kusema hao wanaoondoka si lolote, si chochote. Hizi ni hauli za kisiasa. Lililo muhimu ni kwamba kama hadharani wanakosa ujasiri wa kukiri hatari hiyo ya kukimbiwa, ni vema wakiwa faragha walikiri hilo.
Pili, majeshi ya uvamizi yalipouteka uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Saddam, mara moja Al-Sahaf, akajitokeza kwenye televisheni na kuwatangazia wananchi: “Uwanja unadhibitiwa na majeshi ya Serikali ya Iraki, adui wamepigwa vibaya sana. Mchana nitawapeleka waandishi wa habari, lakini ngoja kwanza uwanja ufanyiwe usafi (kuondoa mabaki ya makombora na silaha za adui vilivyoteketezwa.”
Maneno haya ya Al-Sahaf yanafanana na haya ya CCM ya kuwaambia wapinzani wao: “Subirini Oktoba 25 muone tutakavyowagaragaza wapinzani.”
Kuhitimisha hili ni kwamba pamoja na ghiliba na maneno mengi ya Al-Sahaf ya kuwapa matumaini Wairaki, mwishowe majeshi ya Iraki yalilemewa. Saddam Hussein akakamatwa na akanyongwa baadaye.
Hapa unaona kuwa yale maneno ya kujipa faraja hayakusaidia kulikabili wimbi la kuangushwa kwa Serikali ya Saddam Hussein.
CCM bado ni chama imara, lakini uimara huo si kama ule wa mwongo au miongo iliyopita. Uimara wake hupungua. Hili linathibitishwa na idadi ya kura ambazo wapinzani wamekuwa wakizipata katika uchaguzi wote kuanzia ule wa mwaka 1995. Jedwali linaonyesha kura za wapinzani zimekuwa zikiongezeka. Endapo CCM watalikiri hilo la upanzani kukua, huo utakuwa mwanzo wa kupata njia sahihi ya kujiimarisha ili kukabiliana na moto huu wa Ukawa.
Kauli zinazotolewa na CCM kuwabeza wafuasi wake wanaokihama chama hicho, sidhani kama zina manufaa kwao wakati huu wa kuingia kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu. Ni vema wakaepuka kauli za maudhi kwani zimeonekana kupatiwa majibu yaliyowaingia wapigakura. Kwa mfano, kauli kama ya “Wanaohama ni oili chafu”, imejibiwa na Ukawa kwa kusema: “Dawa ya mchwa ni oili chafu.” Hapa “mchwa” unaotajwa ni CCM, na kwamba oili hiyo chafu itatumika kuua mchwa unaokula au kuharibu mazao na mali za wananchi. Sasa wananchi wanaaminishwa kuwa CCM ni “mchwa” unaostahili kuteketezwa kwa kutumia “oili chafu”.
Nguvu za Ukawa zinaweza isiwe kubwa sana, lakini si za kubezwa hata kidogo. Ushindani wa kisiasa naulinganisha na mapigano baina ya watu wawili wenye miili isiyolingana. Mtu mwenye mwili mkubwa hapaswi kumbeza mpinzani wake mwenye mwili mdogo. Mwili mkubwa si kigezo pekee cha ushindi. Kwenye mapambano kinachotakiwa ni mbinu; na wala si maumbile, nguvu za mwili au vifaa pekee. Nani kasema aliye na kisu hawezi kumshinda mwenye AK47?
Sisi wapenzi wa ndondi tunalikumbuka pambano la Cassius Clay (Muhammad Ali) na Sonny Liston, la Februari 25, 1964. Pambano lile lilikuwa na mvuto wa aina yake. Liston, mtu mwenye miraba minne na bingwa wa dunia wa uzani wa juu, aliogopwa na wengi. Clay, akiwa na umri wa miaka 22 akaingia makubaliano ya kumkabili Liston. Wachambuzi wengi wa masuala ya ndondi walimbeza Clay.
Katika moja ya maandishi yaliyo kwenye vitabu vya ndondi, yanasema: “Few believed Clay could beat Liston, and he was made a seven to one betting underdog. In a poll of sportswriters before the fight, 43 of 46 pick Liston to win.”
Lakini ulimwengu haukuamini pale Clay alipoweza kumpoka Liston mkanda wa ubingwa wa dunia wa uzani wa juu katika raundi ya 6 kati ya 15. Wengi walipigwa butwaa na huo ukawa mwanzo wa umaarufu wa Clay katika ulimwengu wa masumbwi.
Wanasiasa wanapaswa kulitambua na kuliheshimu hilo. Ni kama miaka ile ya 1980 ambako kijana asiyekuwa na jina kubwa kisiasa, Paschal Mabiti alivyoweza kumshinda kwenye ubunge mwanasiasa tajiri na maarufu ndani na nje ya nchi, Paul Bomani. Hakuna aliyetarajia jambo la aina hiyo lakini ni ukweli kwamba aliyedhaniwa dhaifu alimshinda aliyeaminika kwa kila mmoja kuwa ni imara.
Tambo za CCM au yale mazoea ya kujiaminisha kuwa ikiingia kwenye uchaguzi inashinda, ziachwe. Ushindi hauwezi kupatikana kwa hisia au kujipa moyo kutokana na mazoea au historia ya chama. Mambo yamebadilika sana. Bahati mbaya haya tukiyasema, wapo watu ndani ya CCM wanaohitimisha kwa kutuita Ukawa. Hawataki kuambiwa ukweli. Anayewaambia ukweli ni mpinzani wao na wako tayari kumpa majina mengi mabaya na hata kumtenga!
Uchaguzi wa mwaka huu umeanza kuonyesha kuwa CCM wanachofanya ni kile ambacho wataalam wa siasa wanakiita “defensive”; na Ukawa wamekuwa “offensive”. Mara zote ukishakuwa “defensive” unakuwa ni mtu wa kusubiri mpinzani wako amekuibulia nini, na wewe unabaki kumjibu tu. Mbinu hii kwenye medani ya kisiasa ni ya kushindwa.
Mgombea wa Urais kupitia CCM, Dk. Magufuli, amekuwa na aina fulani ya mambo ambayo tunaweza kusema ndiyo yanayomtambulisha. Amekuwa na brand fulani inayomtofautisha na wenzake wengi aliowashinda kwenye uchaguzi wa kumpata mpeperusha bendera ya chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu. Asijaribu kuipoteza brand yake.
Baadhi ya mambo yanayomtambulisha ni kama vile uwezo wake wa kusimamia sheria au kile anachokiamini kuwa ni sahihi. Watanzania wana kiu ya kumpata kiongozi mkuu ambaye akisema jambo fulani litatekelezeka, kweli waone likitekelezwa. Wanaamini Magufuli anafaa na ni mtu wa aina hiyo.
Dk. Magufuli, wanajua ni mtu anayetaka timu anayoiongoza iwe ya wachapakazi kweli kweli. Tumeshuhudia mara kadhaa anavyowabana walio chini yake. Aina hii ya uongozi kwake ni brand inayomfanya awe tofauti na wagombea wengi. Wapo Watanzania wanaoamini akiwa rais anaweza kabisa kujenga mfumo wa uongozi wa kumfanya kila Mtanzania mwenye uwezo wa kufanya kazi, afanye kazi. Wana shauku ya kuona chini ya uongozi wake habari ya mtumishi wa umma au sekta binafsi kuacha ofisi na kushiriki kitchen party, vikao vya harusi na mambo mengine ya aina hiyo, yanapungua na hata kukomeshwa ili muda mrefu utumiwe kufanya kazi na kujiletea maendeleo.
Dk. Magufuli hatarajiwi kuonekana kwenye dansi au matamasha ambayo kimsingi hayana hadhi wala ulazima wa kumfanya rais kuacha kuwaza au kutafuta mbinu za kuwapa wananchi kile wanachokitaka kwa ustawi wa nchi na wananchi. Siku watakapomuona Dk. Magufuli amejiingiza kwenye matamasha ya aina hiyo, atakuwa amewaudhi kwa kuwa wanajua yeye si wa aina hiyo. Hayo mambo si brand yake!
Kama ilivyo kwa Dk. Magufuli, ndivyo ilivyo pia kwa mgombea urais kupitia Ukawa, Edward Lowassa. Lowassa hana mchezo linapokuja suala la kazi na uwajibikaji. Wote hawa wawili wana mambo ambayo ni brand za zinazowatofautisha na viongozi wengine, akiwamo anayemaliza muda wake.
Kufanana huko ndiko kunakolifanya pambano la mwaka huu liwe gumu. Kosa moja la kiufundi linatosha kumwangusha mgombea yeyote kati ya hawa wawili.