Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani hapa kimeunga mkono uamuzi wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kuwapitisha Dkt Samia Suluhu Hassan, Dkt Hussein Mwinyi na Dkt Nchimbi kuwa wagombea Urais kupitia CCM mwaka huu.
Pongezi hizo zimetolewa na Viongozi mbalimbali wa chama hicho kwenye maandamano ya amani yaliyofanyika juzi mjini hapa ambapo walieleza kuwa hatua hiyo imetokana na kasi na weledi mkubwa walioonesha katika utendaji wao.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Said Mkumba amesema kuwa wamefanya maandamano hayo ili kuunga mkono uamuzi huo kwa kuwa viongozi hao 2 wameonesha uwezo mkubwa na kusimamia kwa asilimia 100utekelezaji ilani.
‘Uamuzi huo ni ishara tosha kwamba wanaCCM tumeridhishwa na uwezo wao na kasi yao ya kusimamia utekelezaji ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 kwa asilimia 100 na tuna imani kubwa kwao’, ameeleza.
Amebainisha kuwa uamuzi huo unamaanisha kwamba Rais Samia na Mgombea mwenza Dkt Nchimbi ndio chaguo la wanaCCM kwenye urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais Mwinyi kwenye urais wa Zanzibar.
Nkumba ameeleza kuwa kasi ya maendeleo yaliyoletwa na Rais Samia na Rais Mwinyi kule Zanzibar ni kielelezo tosha kuwa Viongozi hawa wanatosha kupewa mitano tena na huo ndio uamuzi wa mwisho wa wanaCCM wote.
‘Rais Samia ni mwanamke shujaa na kiongozi makini mwenye maono makubwa ya kimaendeleo, tumepokea uteuzi huo kwa mikono miwili, Tabora tunaunga mkono mapendekezo hayo kwa asilimia 100’, amesema.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mohamed Nassoro amesema kuwa CCM ni chama imara na kitaendelea kuchagua Viongozi makini, wazalendo, wachapa kazi, wanaojali watu na siyo maslahi binafsi na wenye kauli safi.
Amebainisha kuwa Rais Samia, Rais Mwinyi na Emanuel Nchimbi ni chaguo sahihi, wana kila sifa zinazotakiwa na watanzania wote na wameonesha uwezo mkubwa katika utendaji wao.
‘Watanzania wana kila sababu ya kuwashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa maamuzi hayo ambayo yatawapa nafasi wagombea hao wa CCM kujipanga vizuri kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaohusisha vyama vya upinzani’, amesema.
Naye Katibu wa CCM Mkoa Wilson Nkambaku ameeleza kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wameonesha ukomavu mkubwa wa kisiasa na huo ndio ukweli, hata katiba ya chama inawapa nafasi ya kuendelea kushika nafasi hiyo.
Amebainisha kuwa wapinzani hawajawa na uwezo wa kuongoza nchi, hivyo akawataka kuendelea kujifunza kwa Chama Cha Mapinduzi hadi watakapokuwa na uwezo wa kujisimamia huku akiongeza kuwa serikali ya CCM itaendelea kuwaletea maendeleo wananchi pasipo kujali itikadi zao.