Tanzania ilikuwa nchi inayofuata mfumo wa chama kimoja hadi mwaka 1992, wakati nchi wahisani za magharibi ziliposhinikiza nchi zote duniani zinazoendelea, kuanzisha mfumo wa vyama vingi kama ishara ya kujenga misingi bora ya demokrasia kwa jamii.
Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilikuwa haihitaji sana mfumo wa vyama vingi, lakini kwa kuhofia kunyimwa misaada na nchi wahisani, ikabidi ikubali kuanzisha mfumo wa vyama vingi. Lakini vyama vya upinzani havikuanzishwa kwa kufuata taratibu za uanzishwaji wa mfumo huo.
Hivyo, tukaanzisha vyama vya upinzani ambavyo havina sauti zaidi ya kupewa fursa ya kuhubiri majukwaani.
Wakati wa mfumo wa chama kimoja cha CCM tulikuwa tunasema chama kimeshika hatamu. Kwamba chama ndicho kinachoongoza Serikali, na kwa bahati mbaya tukaunganisha Serikali na chama kikawa kitu kimoja; kila ofisi ya Serikali kukawa na tawi la CCM na viongozi wa chama ndani ya wizara na idara mbalimbali za Serikali, ndiyo wakawa wabunifu na viongozi wakuu wa shughuli za Serikali.
Chama kikawa na sauti kwenye kila idara ya Serikali, kwa kupanga na kusimamia majukumu ya idara hizo bila kujali uwezo wa viongozi hao wa chama kitaaluma!
Wakati tumesema chama kimeshika hatamu pia tukasema pesa za chama hazifanyiwi ukaguzi wa mahesabu, na tunajua fika kwamba chama hakina biashara yoyote ile inayoweza kukiwezesha kupata mapato ya kujiendesha, bali kilikuwa kinategemea kupewa pesa ya walipakodi kutoka hazina!
Kwa utaratibu huu chama kikawa kimetoa mwanya wa ufisadi ndani ya chama chenyewe, kwenye idara za serikali na jamii kwa ujumla. Katika mazingira hayo ukawekwa utaratibu wa kuchukua pesa za walipakodi kutoka hazina na kuzipeleka kwenye chama kugharamia matumizi mbalimbali yakiwamo ya chama.
Kutokana na hali hiyo, kila mtu akawa anajitahidi ajiunge na chama na agombee uongozi wa ngazi ya juu ili aweze kupata mwanya wa kutumia fedha hizo.
Wakati chama kimeshika hatamu, kiliweza kuchukua pia baadhi ya mali za umma ambazo ni pamoja na majengo ya Serikali kwa ajili ya kuyafanyia shughuli mbalimbali za kichama, viwanja na mashamba kwa kutumia kigezo kwamba Serikali na chama ni kitu kimoja.
CCM pia kilichukua baadhi ya magari ya Serikali na kuyamiliki, na wakati mwingine ilichukua pesa hazina na kununua magari mapya kwa ajili ya chama. Ilichukua pia kiwanda cha uchapishaji cha KIUTA na kukifanya mali yake. Kiwanda hicho ndicho kilichokuwa kinamiliki magazeti ya Uhuru na Mzalendo.
Kuna baadhi ya mali za Serikali ambazo zilichukuliwa na chama, lakini zimeangukia mikononi mwa ‘wajanja’ wachache na wameshazifanya mali zao binafsi!
Mwaka 1992 nchi ilianza kufuata mfumo wa vyama vingi, lakini bado CCM imeendelea kushika hatamu kwa kuendelea kuvifanya baadhi ya vyombo vya dola kuwa kama idara ndani ya chama hicho, hivyo kuvifanya vyama vya upinzani kukosa nguvu nchini.
Mazingira kama haya yamevifanya vyama vya upinzani wakati mwingine vionekane kama si vyama halali kikatiba, na hivyo kuvifanya viwe dhaifu katika suala zima la kuthibitisha kuwapo kwao na kutetea maslahi ya umma.
Ndiyo maana pamoja na nchi kukumbwa na kashfa nyingi za ubadhirifu wa mali za umma, vyama vya upinzani havijaweza kukemea ufisadi ipasavyo. Matokeo yake baadhi ya rasilimali za nchi zinahujumiwa na watumishi wasio waadilifu. Pesa ya EPA imepotea hivi hivi. Kulikuwapo pia habari za twiga kusafirishwa mchana kweupe – tena kupitia kiwanja cha ndege cha kimataifa, kwamba eti wamepata soko huko Uarabuni.
Makontena ya pembe za tembo wa Tanzania yamekamatwa huko China na Vietnam, lakini wahusika hawajachukuliwa hatua zinazostahili. Wachina wamevuna magogo huko Lindi na Mtwara hadi wamepeleka mirunda ya miti adimu ya Mpingo makontena kwa makontena.
Vyama vya upinzani vimenyamaza kimya vinasubiri eti kwanza viingie madaraka ndipo vianze kuyashughulikia! Mtaingiaje madaraka wakati hamjatambuliwa ipasavyo? Sasa mtatumia miujiza gani mshinde uchaguzi?
Wakati tunaanzisha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, siasa za kikomunisti zilikuwa zimeshakufa duniani, mwasisi wa mfumo huu wa vyama vingi alikuwa Mwalimu Nyerere pamoja na kwamba alikuwa ameshastaafu, lakini ilitokea tu tukajikuta yeye tena ndiye mwasisi wa mfumo huu.
Kiutaratibu alipaswa akivunje chama cha kikomunisti cha CCM na mali zote za chama hicho zirudishwe serikalini, ndipo sasa awaruhusu wanasiasa na wanaharakati kuunda mfumo wa vyama vingi, ili vyama vyote viwe na nguvu sawa na viwe na uwezo wa kutetea haki za wananchi na maslahi ya Taifa kwa ujumla.
Binafsi ninapendekeza kuwa katika kipindi hiki ambacho tunaitafuta Katiba mpya tuhakikishe kwamba tunakitenganisha chama tawala na Serikali, pia kuhakikisha CCM inarejesha mali ilizochukua kutoka serikalini na hazina na kuzirejesha serikalini.
Tukifanya hivyo, tutakuwa tumejenga mazingira mazuri ya demokrasia ya kweli hapa nchini, pia tutavipa nguvu vyama vya upinzani viweze kusimama imara na kutetea maslahi ya umma.
Mwandishi wa makala haya, Dk. Noordin Jella (PhD in Economics), ni Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu Huria, Chuo Kikuu cha Kampala (KIU) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa sasa ni Mwandishi wa Kujitegemea na Mchambuzi wa masuala ya siasa. Anapatikana kwa email: [email protected].
Simu: +255 782 000 131