Katika maisha ya jadi niliyoishi kijijini, kila kitu kilichotokea kilihusishwa na Mungu. Kama kuku hawakutaga mayai mengi kutokana na kutopewa chakula cha kutosha, watu walisema ni amri ya Mungu.

Kama mtu alikufa kwa ugonjwa kwa sababu ya kucheleweshwa kupelekwa hospitali, watu walisema ni amri ya Mungu. Na kama watoto walichezea moto ukaunguza nyumba, watu walisema ni amri ya Mungu.

Mungu. Mungu. Mungu wakati wote! Hayupo aliyefikiri kisayansi.

Mawazo ya siku zile za jadi hayatofautiani na mawazo ya mataifa makubwa leo. Mataifa makubwa huamini kwamba uchaguzi huru na wa haki ni ule ambao chama cha upinzani hushinda. Chama tawala kikishinda uchaguzi, basi uchaguzi haukuwa huru na haukuwa wa haki. Mataifa makubwa yanashindwa kufikiri kisayansi.

Hivi kwanini chama tawala kilichofanya vizuri kisishinde uchaguzi katikati ya vyama vya upinzani ambavyo wananchi hawakuona mchango wao katika maendeleo ya taifa?

Kwa upande wa kwetu Tanzania, vyama vya upinzani vimenaswa na mtego huo wa upotofu. Navyo vimeshindwa kufikiri kisayansi.

Tazama! Mtu akitoa maoni yanayotofautiana na yao, wapinzani husema mtu huyo anatumiwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tazama! Jeshi la Polisi likichukua hatua halali dhidi ya wapinzani wanaofanya vibaya, wapinzani husema jeshi hilo linatumiwa na CCM.

Tazama! Vyama vya upinzani vikishindwa uchaguzi, husema CCM imeiba kura au imetoa rushwa kwa wapigakura.

Kila kitu CCM. CCM! Wapinzani hawajaona kwamba hata vitendo vyao na kauli zao zinaweza kuwakosesha kura.

Hakuna asiyeona umuhimu wa vyama vya upinzani. Vyama vya upinzani vina mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa. Ndiyo maana tulirejesha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Vyama vya upinzani huifanya Serikali iwe macho wakati wote katika kuwahudumia wananchi. Vyama vya upinzani hulifanya Bunge kuwa chombo kinachowakilisha maoni ya wananchi wote. Na vyama vya upinzani huchochea maendeleo ya taifa.

Lakini vyama vya upinzani vinapohusisha CCM na kila jambo linalotokea katika maisha ya kila siku ya taifa bila kufikiri, lazima vioneshwe tabia hiyo inayoathiri vyama vyenyewe vya upinzani ila vikitaka vijirekebishe.

Kwanza, tabia ya kuihusisha CCM na kila jambo wakati wote inasababisha wapinzani wasiaminiwe hata katika jambo ambalo wanaweza kuihusisha CCM kwa haki. Wapinzani wanaonekana kuwa hodari wa kusingizia!

Kwa hiyo, wanapoihusisha CCM na jambo fulani kwa haki kabisa, watu huona kwamba ni wale wenye tabia ya kusingizia CCM kila kitu na kila siku.

Pili, upinzani si uhasama, kwa hiyo wapinzani wanapoisema vibaya CCM kila siku hata pasipo haki, wanaonekana ni watu wanaotafuta uhasama na CCM kila siku.

Tatu, tabia ya kusema watu wenye heshima zao na akili zao kwamba wanatumiwa na CCM inadhalilisha sana watu hao. Kwa upande mmoja inaleta picha kwamba watu hao hawana uwezo wa kufikiri wenyewe mpaka waambiwe na CCM cha kufanya. Na kwa upande mwingine inaleta picha kwamba watu hao wanapewa chochote na CCM ili watumike. Kwa kifupi, watu wanaohusishwa na suala la kutumiwa na CCM wanaonekana hawana msimamo.

Nne, watu wanaohusishwa na CCM isivyo halali kwa sababu tu wametofautiana mawazo na upinzani, huchochewa kuwa karibu na CCM.

Ni mfano wa mume ambaye wakati wote anamhusisha mkewe na mwanamme fulani isivyo halali. Anamchochea mkewe kuwa karibu na mwanamme huyo.

Tano, ni vyema wapinzani wakajua kwamba tabia ya kuihusisha CCM na kila kitu inakatisha tamaa wafuasi na mashabiki wa vyama vya upinzani. Inawaaminisha kuwa CCM ni jitu lisilowezekana na lenye uwezo mkubwa wa kufanya jambo lolote. Kwa hivyo wanachochewa kuwa karibu na CCM.

Sita, tabia ya kulihusisha Jeshi la Polisi na CCM kila wakati jeshi hilo linapochukua hatua dhidi ya wapinzani wanapotaka kufanya vibaya, inadhalilisha jeshi hilo. Inafanya jeshi hilo lionekane kwamba halina kazi yoyote nyingine ya kufanya ila kuitumikia CCM.

Saba, tabia ya wapinzani ya kuleta picha kwa wafuasi wao kwamba Jeshi la Polisi halitendi haki kwa vyama vya upinzani, inachangia kujenga uhasama kati ya wafuasi wa vyama vya upinzani na jeshi hilo. Uhasama huo huishia kwenye wafuasi wa vyama vya upinzani kupambana na polisi wakati wote.

Hali hiyo husababisha wapinzani kuonekana kuwa watu wasiopenda amani. Itawasaidia sana wapinzani wakijua mambo mawili.

La kwanza, Watanzania ni wapenda amani. Kwa hiyo, siasa za mapambano zinazoendeshwa na wapinzani zinawaweka mbali wapinzani na wapigakura.

La pili, kushindwa kwa wapinzani katika chaguzi mbalimbali kunachangiwa sana na vurugu zao na kauli zao.

Hebu fikiria, kiongozi wa upinzani unapotangaza kuwa utafanya maandamano au mkutano uliozuiwa na polisi, chama chako kinaonekana cha vurugu na unawaweka wananchi roho juu.

Fikiria tena, kiongozi wa upinzani anaposema Nyerere si mtakatifu katikati ya Wakatoliki wanaoshughulika na mchakato wa kumfanya Nyerere kuwa mtakatifu, anatarajia chama chake kupigiwa kura na Wakatoliki na wapenzi wa Nyerere?

Katikati ya vurugu na kauli chafu za wapinzani, CCM ikishinda uchaguzi wapinzani husema CCM imeiba kura au imetoa rushwa. Wanasahau kuwa vurugu zao na kauli zao zinachangia wao kukataliwa na wapigakura.

Basi wapinzani wayatafakari hayo. Wachunge vitendo vyao na kauli zao, vinginevyo wataendelea kuihusisha CCM na kila kitu, na kuonekana kuwa kila siku ni hodari wa kusingizia.