Mwaka 476 kabla ya Kristu kuna historia ya pekee katika dunia ya sasa. Mwaka huu, dunia ilishuhudia kuanguka kwa Dola Kuu ya Warumi (Rome Empire) iliyokuwa imetawala siasa za Ulaya kwa millennia moja, yaani miaka 1,000. Dola hii ilikuwa ikiongozwa kwa imani za miungu (polytheistic) na inaelezwa kuwa iliangushwa na ujio wa dini ya Wakatoliki waliokuwa wakiamini katika Mungu mmoja (monotheistic).
Sababu hii inatajwa mno kutokana na wimbi kubwa jinsi dini ya Wakatoliki wa Roma walivyopata umaarufu na kutawala siasa za Ulaya wakati huo. Ilifika mahala wafuasi wa dini Katoliki wakasulubiwa kwa imani yao hadi alipokuja Mfalme Constantine aliyezuia uhalifu huo.
Ukiangalia kwa kina, Ukatoliki katika Roma hakukua kwa sababu nyingine. Ukatoliki ulikuwa kutokana na mateso na manyanyaso waliyopata wananchi wa kada ya chini. Wafalme wa Roma waliokuwa wakiamini katika miungu, walianza maisha ya anasa. Wakafikia mahala wakawa na fedha nyingi, wakaweza kuwa na vijakazi hadi 300 kwa familia moja ya kifalme ya Roma.
Sitanii, kodi zikatozwa kwa wingi kugharimia sherehe na harusi za kifahali za wafalme. Hitaji la msingi kwa binadamu, chakula bei yake ikaenda juu kwa kiwango cha kutisha. Wananchi wakawa hawana chakula, rushwa ikatamalaki, ubabe wa Wafalme ukazidi kuongezeka, magonjwa yakaongezeka kwani huduma ya maji, afya na elimu ni sawa na vile zilikoma.
Kila Mfalme alichukuliwa kama Mungu ndani ya Roma, na hiyo ndiyo dhana ya kuamini katika miungu wengi. Dini Katoliki, iliona ni vyema kuwaunganisha wanyonge kupitia imani, ikahubiri Mungu mmoja imani moja. Dini Katoliki ikahubiri mgawanyo sawa wa mapato, upendo, kuheshimiana, usawa mbele ya sheria, usawa wa ajira, kutoingiliwa katika imani, haki ya kuishi, kutotumikishwa kama vijakazi na mengine mengi.
Wakatoliki hawa, walianza kuhubiri ulipaji wa kodi kwa staha. Walidai uwajibikaji. Walihoji kodi zikilipwa zinatumikaje. Zinagharamia huduma za jamii au anasa binafsi kama harusi za kifahari, huku watoto wakifa kwa njaa, watu wazima wakichukuliwa mateka na kutumikishwa kama vijakazi kwa nia ya kuganga njaa?
Sitanii, mwaka 313 Kabla ya Kristo, Mfalme Constantine alizuia matesho dhidi ya wafuasi wa Kanisa Katoliki. Kuepusha shari, aliamua kuigawa Roma katika tawala mbili, Mashariki na Magharibi. Mfalme Constantine aliwabakiza Wakatoli Roma, Italia na Wapagani waliokuwa wakiamini katika miungu wakaenda katika mji aliouita jina lake Constantinople, ambayo ni Istanbul (Uturuki) ya sasa.
Falme ya Roma iliendelea kuzungumza Kilatini na hawa wakabatizwa na kuwa Wakatoliki safi, ambao wengi waliamini katika amri 10 za Mungu zisemazo: (1) Mimi ni Bwana Mungu wako, usiabudu miungu wengine, (2) Usilitaje bure jina la Mungu wako, (3) Shika kitakatifu siku ya Mungu, (4) Wahesimu baba na mama upate miaka mingi na heri duniani, (5) usiue, (6) usizini, (7) usiibe, (8) usiseme uongo, (9) Usitamani mwanamke asiye mke wako na (10) usitamani mali ya mtu mwingine.
Ukiziangalia amri hizi, ziliwekwa kwa nia ya kurejesha maadili katika jamii. Zililenga kurejesha utu wa watu. Zililenga kuzuia vurugu na ubabe katika jamii. Zililenga kuleta usawa. Wananchi walizikubali, wakaziona ni mkombozi wao, kwa maana hata wale waliobaki Istanbul, ambako walikuwa wakizungumza Kigiriki, walivutiwa na yaliyokuwa yakiendelea Roma kwa waliokuwa wanazungumza Kilatini, wakaongoka. Huo ndio ukawa mwisho wa Dola ya Roma.
Hata Yesu alipokuja duniani, wanafunzi wake wakamuuliza. Mwalimu, ni ipi iliyo amri kuu kuliko zote, Yesu akawambia ni upendo. Kwa maana ukimpenda jirani yako huwezi kumwibia. Ukimpenda jirani yako, huwezi kumzini mtoto wake, ukimpenda jirani yako huwezi kumzini mke wake, ukipenda jirani yako huwezi kumtusi, huwezi kumdhihaki, huwezi kumkejeli au kumtoza kodi isiyo halali.
Sitanii, kichwa cha makala hii kinasema “CCM inaanguka polepole kama Dola ya Warumi.” Nimewaza sana kabla ya kuandika makala hii. Nimefikiria historia nikarejea enzi za watumwa, vijakazi na watwana katika miji ya Athens (Ugiriki), Sparta (Ugiriki) na Constantinople (Uturuki).
Miji hii yote ilikuwa sehemu ya dola kuu ya Warumi. Walikuwa wakiishi katika maisha ya sherehe. Wakubwa hawa walimiliki mapande ya ardhi kuliko mtu yeyote katika dunia ya sasa. Nimetangulia kusema hapo awali, kuwa wafalme walitoza kodi kwa ajili ya kuendesha starehe zao na familia moja ikafikia kumiliki vijakazi hadi 300.
Nikivuta hisia na kuangalia kinachoendelea hapa kwetu hakuna tofauti. Chama tawala kimetugeuza vijakazi. Kodi ya mafuta ya zinapanda kwa wakubwa kukutana kwenye sherehe tu, wakakubaliana. Sasa kodi za daladala bila hata kupitia bungeni, zimepanda mara mbili bila mashauriano kwa kuwa wakubwa wamependa iwe hivyo.
Fedha zetu zilizokuwa zinabishaniwa katika akaunti ya Escrow, zimetolewa na kugawiwa kwa wakubwa na wazee wakakabidhiwa viroba. Waliozipokea wameanza kutukejeli. Wakati Chenge anajiita joka msaka fedha, tena lenye makengeza, na akiitia bilioni 1 vijisenti, Profesa Anna Tibaijuka anatwambia anatumia Sh milioni 10 kununua mboga ya siku mbili.
Brother Jay, James Rugemalira anatwambia Sh bilioni 125 alipewa ni vijipesa vya ugoro. Mnikulu Shaban Gurumo, anasema hakumbuki alivyotumia Sh milioni 80 maana kwa utajiri wake anatoa fedha mfuko wa kulia na kuweka wa kushoto kiasi hakujua kama kiasi hicho cha fedha kiliingia kwenye akaunti yake!
Sitanii, kama ilivyokuwa katika Dola ya Warumi, kama wewe hukuwa sehemu ya mtandao wa wafalme, hataka kama ungekuwa na akili kiasi gani. Ilitosha kukuita kijakazi, ukakosa sifa ya kuwa kiongozi. Viongozi walikuwa wanakaa kwenye sherehe, bila hata kupiga kura wanateuana nani aongoze dola.
Leo, tunashuhudia hata kama wananchi wanakupenda kiasi gani, kama hukubaliki katika kilinge cha ‘Wafalme’ ndani ya Kamati Kuu ya CCM, ujue wakubwa wanaamini hata wakileta shati litachaguliwa tu, tena bila kuhoji hata swali moja. Abdulrahman Kinana Katibu Mkuu wa CCM, anakumbuka shuka kumekucha.
Sitanii, Kinana anasema hakuna mtu ambaye jina lake litakatwa kama anakubalika kwa wananchi. Rejea kilichotokea kwenye serikali za mitaa. Watu wameuza nyumba kwa ajili ya kuhonga wapate ujumbe wa Serikali za mitaa, waliokuwa pangu pakavu wakatoshwa, wakapitishwa wenye nazo.
Ukisikiliza siasa za majukwaani, wengi wanasema wanapingana na mafisadi, lakini kumbe wanaandaa mrija wa kunyonya pasi kusumbuliwa. Wiki iliyopita nikiwa katika kipindi cha Agenda 2015 cha Star TV, nilisema kuwa rushwa ilipofikia sasa si ufa, bali ni dirisha.
Mtazamani mmoja akaniletea ujumbe akasema si dirisha, bali ni geti, tena la kupitishia malori. Wakubwa wanatumia rushwa kuanzia ngazi ya mtaa. Ukienda hospitalini unaambiwa wazi, kuwa kama huna fedha utakufa unaona. Watoto shuleni walimu wanawadai ‘dambwe’ na inafika mahala hata shule za binafsi wazazi wanakolipa hadi Sh milioni 2, bila soni walimu wanadai watoto walipie masomo ya ziada (tuition).
Sitanii, ukiangalia kimantiki ni sawa na kusema walimu wanaofundisha kwenye shule za Serikali, wanakwambia wakubwa tayari wamechukua chao kwenye madini na kila pahala, hivyo nao ni zamu yao kuchukua ‘dambwe’ kutoka kwa wazazi. Ajira zinapatikana kwa undugu, si kwa nani anaelewa nini.
Binafsi, sitaki kuishia kulalamika. Tutafanya kosa la mwaka, ikiwa tukimchagua Rais asiye na maono. Nasema bila kujali ni chama gani anatokea, Rais ajaye lazima atueleze akichaguliwa atafutanyia nini. Hatutaki Rais anayetokana na Kamati Kuu za vyama eti kwa sababu tu, ni mwenzao, ana sura nzuri au atawalinda.
Tulipofika sasa, hatuhitaji kushangazwa na uamuzi wa wachache. Tunapaswa kuwa na Rais anayesimama akasema saruji itakuwa shilingi ngapi akishika dola, nidhamu ya utumishi wa umam itakuwaje, elimu yetu itagharimiwaje, bei ya bati na misumari itakuwa shilingi ngapi, na si Rais wa kusema Ilani ya chama inasema.
Kama alivyofanya Mfalme Constantine, tusema kubaguana kwa misingi ya vyama, dini, kabila, nani anaunga mkono falsafa za nani, sasa kukome. Leo, inawezekana hata wewe unavyosoma makala hii, badala ya kufikiria ujumbe uliomo, unaanza kuwazi, huenda huyu kwa mstari au mshororo huu anampigia debe Wasira, Makamba, hapana Mrema.
Kwa Tanzania tunapaswa kutoka hapo. Maisha ya kubahatisha yalikuwa enzi za ujima. Mchezo wa wakubwa kukwepa kodi, wadogo wakabanwa mbavu usitishwe. Tufika mahala sasa, nchi yetu iseme kwa sauti nzito na ya wazi kuwa madaraka ya kupeana kama zawadi yakome.
Viongozi wenye kutaka kutuongoza, wasimame waombe wenyewe, si sisi tutumie kauli eti wapigakura wamuombe mtu kugombea udiwani, ubunge au urais. Huyu tutakayemuomba kugombea, ikiwa yeye hana wazo au hajapata kufikiri kushika wadhifa husika, mwisho wa siku asipotekeleza lolote hatuwezi kuwa na swali kwake.
Tukimhoji kwa nini hakututumikia vyema, anaweza kusema mliniomba kugombea urais, lakini hamkunipa vitendea kazi na mawazo jinsi ya kuifanya kazi ya urais. Rais Barrack Obama wa Marekani, alisimama akawambia Wamarekani “Nichagueni nitoe bima ya afya kwa kila Mmarekani.” Leo Wamarekani wote wana bima ya afya.
Sitanii, hivi kweli leo Watanzania bado tunayo dhana ya kuchaguliwa kiongozi? Hata baada ya viongozi wetu kutukejeli na kutamba kwa utajiri ambao hawakupata kuwekeza jasho, bali unatokana na kodi zetu? Kwamba fedha za Escrow ni jasho la mama anayewasha kibatari kijijini, si siri.
Leo, unakutana na mtu mzima, ambaye ulidhani ana akili timamu, anatumia muda wake kukupigia simu na anasema wazi kuwa fedha za Escrow hazikuwa mali ya Watanzania. Unamuuliza kama hazikuwa mali ya Watanzania kwa nini zilifunguliwa akaunti maalum hadi mgogoro uishe, anasema hayo tuyaache.
Unapombana maswali zaidi anadiriki, tena kijinga kabisa, kukwambia kuwa “hata kama unataka kumfurahisha huyo kwa kuandika hivyo, uhalisia hauko hivyo.” Sitaki, kukosa adabu, lakini nadhani kama isingekuwa gazeti ni kumbukumbu ya kudumu katika jamii ningemvurumishia tusi moja la nguvu.
Sitanii, enyi vijakazi Watanzania wenzangu mnaozalisha wakachota wenye nyadhifa wafalme na kuturejeshea makombo amkeni. Amkeni tupinge ubaradhuli huu. Nchi hii ni yetu sote. Tuamke, tudai haki zetu kama walivyofanya Waroma waliokuwa malofa. Tusikubali kuamriwa na wachache wenye kulinda masilahi yao.
Kimsingi zimenikera mno kauli za viongozi hawa kutukejeli. Sijajua kwa nini hadi sasa Gurumo bado ni Mnikulu. Huyu mwenye jukumu la kutunza mali za Ikulu, hajatueleza kama anafanya biashara. Leo anatukejeli kuwa Sh milioni 80 hakupata taarifa kama ziliingia kwenye akaunti yake?
Wakati umefika. Tujiandikishe kwa wingi, hii ndiyo silaha kuu tuliyonayo mkononi. Sishauri tuchukue mkondo wa Warumi, waliopigana vita siku tatu na kuiangusha dola hii, bali nashauri Oktoba mwaka huu, yeyote aliyeweka jina lake kama hatimizi matarajio, usione soni kumpigia mgombea wa CCM kama wewe ni mpinzani ikiwa unaona anafaa, na vivyo hivyo wewe mwana-CCM usisite kumpigia kura mgombea wa upinzani ukiona CCM wamekuuzia mbuzi kwenye gunia.
Sitanii na nahitimisha, uamuzi tutakaoufanya Oktoba mwaka huu, utaendelea kufanya kazi kwa miaka 10 ijayo. Tukichagua mateso, na hata baada ya kushuhudia aina ya viongozi tulionao, viongozi wasiojua shida zetu, viongozi wenye kuamini kama mikate imeisha tule keki, hakika tutajuta. Uamuzi uko mikononi mwetu. Tukajiandikishe kwa wingi, shahada ya kura iwe silaha yetu Oktoba. Mungu ibariki Tanzania.