Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetahadharishwa kujiepusha na hulka ya kuwapokea wanachama wanaotoka Upinzani, badala yake kijikite katika siasa za ukombozi zinazogusa ustawi wa maisha ya watu.

Mhadhiri katika Idara ya Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ali, ametoa rai hiyo alipokuwa akihojiwa na JAMHURI mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mahojiano hayo yalihusu mwendelezo wa wanasiasa wakiwamo wabunge na wapinzani walioteuliwa na Rais John Magufuli kuvihama vyama vyao.

Bashiru amesema hatua ya wanasiasa kuhama chama kimoja kwenda kingine, haina tija kwa umma na Taifa isipokuwa kujinufaisha binafsi.

Amesema vyama vya siasa vinapaswa kujitanabahisha kwa kuchangia ufanisi katika nyanja za uchumi na jamii, na kwamba ongezeko la wanachama linapaswa kuwa sehemu ndogo ya shughuli za vyama hivyo.

“Hivi sasa vyama vinafanya siasa huria, mtu ana hiyari ya kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine bila kikwazo chochote, hata kubaki bila kuwa mwanachama wa chochote cha siasa,’’ anasema.

Miongoni mwa wanasiasa waliovihama vyama vyao ni pamoja na wabunge watatu wakitanguliwa na aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu.

Nyalandu alitangaza kuihama CCM na kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Wengine na vyama walivyokuwamo kwenye mabano, Maulid Mtulia (CUF-Kinondoni) na Godwin Mollel (Chadema-Siha), walitangaza kuvihama na kwenda CCM.

Mtulia alijiondoa CUF Desemba 2, mwaka huu wakati Mollel alitangaza kujivua uanachama wa Chadema na kujiuzulu ubunge Desemba 14, mwaka huu.

Wakati Nyalandu alizitaja sababu kadhaa ikiwamo kuminywa kwa demokrasia na uhuru wa kujieleza kunakofanywa na Serikali, vimechangia kuondoka kwake CCM, Mtulia na Mollen wameelezea kuridhishwa na utendaji kazi wa Rais Magufuli.

Pia Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo, na aliyekuwa Mshauri wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo, walijiondoa na kuhamia CCM.

“Nimefanya kazi na wananchi wenye itikadi tofauti mkoani Kilimanjaro na ninakiri kuona CCM ikibadilika, ikiwa kinyume na vitendo vya rushwa, yenye kusisitiza nidhamu katika utumishi, nimeona nitamke wazi kuungana na wana- CCM wanaopenda mabadiliko,” amesema.

Mghwira ametoa kauli hiyo kwenye Mkutano Mkuu wa Tisa wa Umoja wa Wanawake Tanzanzia (UWT) uliofanyika hivi karibuni mkoani Dodoma.

Lakini, Bashiru anasema, ‘‘Aina hii ya siasa imeua siasa ya ukombozi  ambayo kimsingi inahitajika nchini, hata CCM imemezwa na siasa huria badala ya kujikita katika kujiimarisha kiitikadi.”

Bashiru amesema kwa umri wa CCM iliyozaliwa Februari 5, 1977, ingetarajiwa kujitanabahisha kwa kuwahakikishia wananchi maisha bora na kuimarisha vyama vinavyosimamia makundi mbalimbali ya jamii.

Anasema hali hiyo ingepunguza umaskini kwa wananchi wa kawaida walio wajenzi wa kweli wa chama cha siasa.

KUMSIFIA JPM

Hata hivyo, Bashiru anaungana na hoja zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa hususani wanaotoka Upinzani kwenda CCM, kuhusu kuridhishwa na utendaji kazi wa Rais Magufuli.

Amesema utendaji kazi wa Rais Magufuli umeonesha nia, utayari na ari ya kuboresha maeneo yenye upungufu katika kuwahudumia wananchi.

“Lakini siyo sahihi kumsifia kwa kiwango kinachoonekana kikifanywa na baadhi ya watu kwa sasa, huo ni unafiki kwa sababu hali bado hairidhishi – hata yeye (Rais Magufuli) amekuwa akisikika akikiri hilo,” amesema Bashiru.

Ametoa mfano kwamba miongoni mwa viwanda zaidi ya 160 ‘vilivyokufa’, wahusika wa kadhia hiyo wamo baadhi ya makada wa CCM hususani waliowahi kuwa viongozi wa ngazi za juu.

KUJITATHIMINI

Amesema CCM inayokadiriwa kuwa na wanachama zaidi ya milioni 10, inapaswa kufanya tathmini ili kubaini sababu za kwa nini hawajitokezi wote kuipigia kura wakati wa Uchaguzi Mkuu.

“Majibu ya tathmini kama hiyo yakipatikana kwa vitendo, itakuwa tafsiri ya siasa za ukombozi zinazohitajika,’’ anasema.