Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amesema CCM hakiko tayari kuacha kuhoji na kufuatilia kwa ukaribu miradi mbalimbali ya kimaendeleo na ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali.
Chongolo ametoa Kauli hiyo leo Januari 30, 2023 katika Kata ya Dumila, Wilaya ya Kilosa aliposhiriki kikao cha Shina namba 10, ikiwa ni Siku ya tatu ya ziara yake mkoani Morogoro, ambapo pia alipata nafasi ya kusikiliza kero na changamoto mbalimbali za Wananchi kwenye Kata hiyo.
Amesema CCM ndio chama kinachoongoza Serikali ya sasa iliyopo Madarakani,Serikali inayoongozwa na Mwenyekiti wake Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hivyo ni Jukumu lake kuendelea kuhoji na kufuatilia kwa Sababu ndio kimepewa dhamana ya Kuwaongoza Watanzania.
“Kuna Jamaa Wajanja wanataka tusihoji wala kufuatilia, Sisi lazima tufuatilie, tuhoji na tuambiane ukweli hadi kieleweke kwa Sababu CCM ndio iliyopewa Dhamana na Wananchi ya kuongoza nchi” amesema Chongolo.
Aidha Chongolo amesema Chama cha Mapinduzi (CCM), hakiko tayari kuharibikiwa ndio maana kinapita kwa Wananchi na kila eneo ili kutimiza wajibu wake kwa Watanzania ili kuona kama Ilani yake ya Uchaguzi ya Mwaka 2020-2025 inatekelezwa kikamilifu.
Kwa Upande wake Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa itikadi na Uenezi Sophia Mjema amewataka Viongozi na Watendaji mbalimbali waliopewa dhamana kuhakikisha Wanasikiliza na Kutatua Kero mbalimbali za Wananchi kwenye maeneo yao.
” Kazi yetu kubwa sisi Wanachama wa Chama cha Mapinduzi ni kuendelea kuisimamia Serikali ili iweze kutatua hizo kero ikiwemo kuizungumzia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ili wananchi waweze kutambua umuhimu wake kwa ajili ya maendeleo ya Taifa” amesisitiza Sophia Mjema.