Vyama vya CCM na CUF vimeibua mjadala mpya wa kisiasa baada ya Mwakilishi wa Jimbo la Ole (CUF), Hamad Masoud Hamad, kujiandaa kuwasilisha hoja binafsi yenye lengo la kuhoji Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kushindwa kumaliza tatizo la upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa na vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (ZAN ID).
Wakati Hamad akijiandaa hivyo, Mwakilishi wa Rahaleo (CCM), Nasasor Salum Al Jazeera, anamalizia hatua za kuandaa hoja binafsi ya kuitishwa kura ya maoni Visiwani humu kupinga kuwapo kwa serikali hiyo.
Mgongano wa hoja hizo mbili kwa namna moja au nyingine unazusha gumzo na mijadala kwenye viunga vya siasa Visiwani hapa, huku kila upande ukivutia kwake.
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe, aliithibitishia JAMHURI kuwa hoja hiyo itawasilishwa kwa nia ya kuondoa tatizo la kutopatikana vyeti vya kuzaliwa na ZAN ID, hatua inayowafanya wananchi wengi kukosa haki ya kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura.
Shehe amesema ingawa mara kadhaa chama chake kilimtaka waziri mwenye dhamana na mambo ya Katiba na Sheria achukue hatua za kutatua jambo hilo, lakini hatoi majibu ya kuridhisha huku wananchi wengi wakikoseshwa haki ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
“Serikali inapanga kutufanyia mchezo wa kitoto; vyeti vya kuzaliwa na vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi bado ni tatizo. Hata waliokamilisha taratibu hawapewi vitambulisho hivyo. Kuna tatizo zito kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu,” amesema Shehe.
Amesema pamoja na CUF kuwa ni sehemu ya SUK, mfumo unaotumika kuanzia ngazi ya watendaji wakuu hadi wilaya ni sehemu ya Serikali Kuu ambako hakuna mgawanyo kama ule uliofanyika ngazi za wizara za Serikali.
Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka, akihutubia mkutano wa hadhara huko Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja mapema wiki hii, alisema UVCCM imemuomba Mwakilishi wa Raha Leo, Al Jazeera, awasilishe hoja binafsi ili wananchi waulizwe iwepo bado wanaafiki mfumo wa SUK au kurejea mfumo wa anayeshinda achukue vyote.
Shaka amesema uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni mchakato na si jambo la kulifuta au kuliendeleza ikiwa wananchi wenyewe – kupitia kura ya maoni – wataona ipo haja ya kuliondoa na kurudisha mfumo wa zamani.
“Tumefika mahali pazuri tokea iundwe SUK miaka mitano iliyopita. Ile hali ya kutoaminiana na kutoshirikiana imekwisha. Tunafikiri ipo haja ya kuulizwa tena wananchi, iwapo je, wanataka mfumo huu uendelee au urudishwe ule wa zamani kwa kufuata utaratibu wa kuitisha kura ya maoni,” anasema Shaka.
JAMHURI ilipowasiliana na Mkurugenzi wa Usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, Mohamed Juma Ame, amesema si kweli kuwa kuna urasimu wa kupata vitambulisho bali jambo hilo linataka kukuzwa na wanasiasa kwa manufaa yao.
Ame amesema anachokiamini Serikali imepata hasara ya kusajili idadi kubwa ya watu ambao hadi sasa hawajajitokeza kuchukua ZAN ID hasa Kisiwa cha Pemba, hatua ambayo alisema imesababisha hasara kubwa kwa kutumia fedha za umma.
“Nataka kukuhakikishia kuwa hakuna mtu anayenyimwa kusajiliwa ikiwa amekamilisha taratibu za usajili. Usajili ni mchakato wenye taratibu zake, hasajiliwi mtu kwa shuruti za kisiasa. Wanaosema hivyo kwanza wathibitishe ZAN ID zilizoko Pemba wenyewe wako wapi hadi sasa [mbona hawazichukui?],” amesema mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa ADC, Ali Makame Issa, amesema kuendelea kuishi kwa SUK yenye ushirika wa vyama viwili ni jambo gumu na kukitaja kipengele cha kikatiba kinachotaka chama kushirikishwa kwenye SUK lazima kifikishe asilimia 5 ya kura, si halali.
Makame amesema ikiwa CCM na CUF watabaki peke yao serikalini, lolote linaweza kutokea kwa sababu kila upande unawinda ni vipi utaudhoofisha mwingine ili hatimaye upande mmoja ushike uongozi wa juu.
“Tuna matumaini ADC tutapata asilimia 5 mwaka huu. Hata hivyo, hatufurahi kuona vyama vingine vikiwa nje ya SUK. Kuiita hii [Serikali] iliyopo ni Serikali ya Umoja wa Kitafifa wakati wanaoendesha ni marafiki wawili,” amesema Makame.