Ni vuta nikuvute. Ndivyo unavyoweza kuelezea kile kinachoendelea katika kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kinondoni na Siha kwa wagombea wa CUF, CCM na CHADEMA kuchuana kuwania uwakilishi wa wananchi.

Katika mikutano iliyofanyika jana kwenye maeneo tofauti, wagombea hao waliendelea kumwaga ahadi ili kuwashawishi wananchi wawachague katika uchaguzi utakaofanyika Februari 17.

Hata hivyo, jana mgombea wa Chadema Jimbo la Kinondoni, Salum Mwalimu alishindwa kuomba kura kutokana na majonzi ya msiba wa mmoja wa watu wa timu yake ya kampeni, Tambwe Hiza.

Akiwahutubia wananchi katika viwanja vya Brazil, Kata ya Hananasif, mgombea wa CUF Rajab Salum alitaja vipaumbele vyake vitano ambavyo atavishughulikia endapo watamchagua.

Alivitaja kuwa ni elimu kwa kuwapigania walimu waongezewe mishahara ili wakidhi mahitaji na pia ataiomba Serikali itenge fungu kwa ajili ya mlo mmoja kwa wanafunzi wa shule za msingi.

“Katika afya, nitapigania bima ya wazee, wajawazito na watoto na nitapigania kutolipishwa ada ya maiti. Katika ajira nitasajili bodaboda na bajaji na kuwawekea mwanasheria ili kutetea haki zao,” alisema Rajabu.

Kuhusu ulinzi alisema atawashirikisha wananchi huku akisema jingine ni sanaa akiahidi kwamba atahakikisha kazi za wasanii zinalindwa kwa hakimiliki.

Alisema Kinondoni inahitaji mbunge ambaye atakuwa chachu ya maendeleo katika jimbo na hakuna anayeweza hilo zaidi yake.

… Vilio kampeni za Chadema Dar

Mkutano wa Chadema uliofanyika Mwananyamala kwa Kopa, ambao ulianza kwa kusimama kwa dakika moja kwa heshima ya Tambwe Hiza, ulitawaliwa na vilio na simanzi.

Baadhi ya wapenzi na wafuasi wa chama hicho waliojitokeza katika viwanja hivyo walionekana wakibubujikwa machozi kutokana na kifo hicho kilichotokea ghafla jana asubuhi huku Mwalimu akizungumza kwa kifupi.

Baada ya kusimama jukwaani, Mwalimu alisema, “Nimesimama hapa lakini akili yangu haiko hapa, nimepata pigo kubwa. Jana (juzi) tulipokuwa kwenye mkutano Tandale kuna jambo lilikuwa linapita kwenye akili yangu lakini sikujua ni nini.

“Jana (juzi) yeye ndiye aliyeninadi jana, yeye ndiye aliyenishika mkono na kuwaambia wana Kinondoni mchagueni Mwalimu, yeye ndiyo anayefaa kuwa mbunge wenu. Kumbe ndiyo alikuwa ananiaga, anawaaga Watanzania,” alisema Mwalimu huku ukimya na huzuni vikitawala uwanjani hapo.

Alisema mara baada ya kumaliza mkutano walikwenda katika vikao vya tathmini usiku na Tambwe Hiza akiwapo. “Nilikuwa mkali kwenye kikao hicho bila kujijua, tukifanya tathmini yetu na Tambwe akiwemo.”

Alikumbusha kauli ya marehemu ya hivi karibuni, “Aliwaambia Watanzania kuwa alipokuwa CCM aliona madhambi ndiyo maana akaja upinzani. Naomba maneno ya Tambwe Hiza yatamalaki kwenye mioyo yenu.”

Mwalimu akizungumza kwa unyonge alisema “leo (jana) siombi kura zenu, naomba yeyote aliyefika kwenye mkutano huu kura yake iwe ni sadaka kwa Tambwe Hiza. Sijui nizungumze nini leo, siwezi! Siwezi,” kisha akashuka jukwaani.

Mara baada ya kushuka, Mwenyekiti wa kampeni hizo, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alisimama na kusema, “Mgombea wetu ni kama mlivyomuona, ameshindwa kuzungumza, kwa niaba yake ninamuombea kura zenu.”

Katika kampeni za CCM, mgombea wake, Maulid Mtulia aliahidi kwamba atahakikisha bodaboda zinasajaliwa kama teksi ili zitambulike na kwamba vijana watakopeshwa ili wajiajiri.

Pia alisema, “Tutakwenda kuhakikisha watu wote waliovunjiwa nyumba zao hawapati athari badala yake wapate maeneo. Mheshimiwa Rais (John Magufuli) hashindwi kuwapa viwanja waliovunjiwa nyumba zao.”

Awali akimnadi mgombea huyo, mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde maarufu Kibajaji alisema, “Acheni siasa za unga wa ngano kubadilika badilika, wana Dar es Salaam acheni siasa za mpira, Juma Kaseja mzuri akiwa Simba akienda Yanga bomu.

“Sisemi Mtulia ataondoa shida zote, hapana, mwenye uwezo huo ni Mwenyezi Mungu pekee, lakini mwenye uwezo wa kushirikiana na Serikali kutatua matatizo ya Wana Kinondoni ni Mtulia.”

Dk Mollel na matibabu bure

Mgombea ubunge wa Siha kupitia CCM, Dk Godwin Mollel akiwa katika Kijiji cha Kilingi, Kata ya Sanya Juu na Kishisha, Kata ya Ivaeni alisema endapo atachaguliwa tena kuliongoza jimbo hilo, atahakikisha wazee wanapata huduma za matibabu bure.

Dk Mollel ambaye alihama Chadema na kugombea tena nafasi hiyo kupitia CCM alisema, wapo wazee ambao wamekuwa wakipata shida wanapofika hospitalini au kwenye vituo vya afya kutokana na kukosa fedha za matibabu hivyo akishinda ataboresha mazingira na kuhakikisha wanapata huduma za afya bure.

Alisema ataelimisha wananchi kuepuka kuuza ardhi kiholela na badala yake wajenge nyumba bora za makazi na za kudumu pamoja na kusambaza majisafi na salama katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo.

“Natambua kuna maeneo ambayo bado wana changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji na hii inatokana na ongezeko la idadi ya watu, sasa naombeni mnipe tena nafasi hii ili nihakikishe nashughulika na matatizo yenu,” alisema.

Awali, mbunge wa Korogwe Mjini (CCM), Mary Chatanda aliwataka wananchi wa Siha kuepuka kurubuniwa na kuuza shahada zao za kura kwa kuwa hiyo itawafanya wakose fursa ya kupiga kura na kumchagua kiongozi bora atakaye waletea maendeleo.

Jana asubuhi, Wanachama wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Kinondoni walisema watampigia kura Mtulia ili awatatulie kero zao tano mahsusi.

Kero hizo ni kusumbuliwa kwa vijana wao bodaboda, tatizo la maji katika baadhi ya kata, mikopo ya kina mama na vijana inayotolewa na halmashauri, kuhakikisha Kinondoni kuwa na amani na utulivu na kuboresha miundombinu ya barabara na hospitali.

Kauli hiyo ilitolewa na katibu mkuu wa jumuiya hiyo, Anna Makilagi kwa niaba yao wakati wa kikao cha tathmini kuhusu mwenendo wa kampeni ya mgombea wao kilichofanyika ukumbi wa CCM Mwinyi Juma, Mwanyamala.

Makilagi ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu, alisema wana imani na Mtulia lakini ahakikishe akichaguliwa anashughulikia changamoto hizo hasa kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali wakiwamo wa mkoa wa Dar es Salaam.

Imeandikwa na Elizabeth Edward, Bakari Kiango, Kalunde Kamali, Peter Elias na Fortune Francis (Dar) na Florah Temba (Siha).