Leo naandika makala hii nikiwa hapa jijini Accra, nchini Ghana. Ghana ni nchi iliyokuwa ya kwanza kupata uhuru barani Afrika.
Nchi hii ilitutangulia miaka minne kupata uhuru kwa maana ya kupata uhuru Machi 6, 1957 ambapo Dk. Kwame Nkrumah alitangazwa kuwa Waziri Mkuu, cheo alichoshika hadi mwaka 1960 Ghana ilipotangazwa kuwa Jamhuri na hivyo Nkrumah akachaguliwa kuwa Rais wa kwanza mzalendo wa Ghana.
Itakumbukwa kuwa Tanzania tulipata uhuru Desemba 9, 1961, ambapo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitangazwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika, kisha mwaka mmoja baadaye kwa maana ya Desemba 9, 1962 Tanganyika ikawa Jamhuri na hivyo Mwalimu Nyerere akaachia madaraka yake kwa Mzee Rashidi Kawawa, kisha akachaguliwa kuwa Rais wa Tanganyika.
Historia ya nchi zetu inafanana kidogo, kwani wakati mwaka 1965, hii ikiwa ni mwaka mmoja baada ya Tanganyika kuungana na Zanzibar, ambapo Tanzania ilifuta mfumo wa vyama vingi na kuanzisha mfumo wa chama kimoja. Hatua hii ilileta msuguano mkubwa ndani ya Chama cha TANU, ambapo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Oscar Kambona, alilazimika kukimbilia uhamishoni Uingereza.
Kabla ya mwaka 1965, itakumbukwa kuwa mwaka 1964 lilikuwapo jaribio la mapinduzi ya kijeshi ambalo halikufanikiwa. Januari 19, 1964, askari kadhaa wa Bataliani ya Kwanza waliasi na wakaungwa mkono na Bataliani ya Tabora. Jaribio hili lilizimwa na ombi la Mwalimu Nyerere kwa Uingereza, ambao walileta ndege kubwa za kivita na askari wanamaji waliowafanya hata waasi waliosalia wajisalimishe.
Jaribio hili lilimsukuma Mwalimu Nyerere kuvunja Jeshi la Kikoloni la King’s African Rifles (KAR) na kuunda Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Septemba 1964. Itakumbukwa kuwa wakati jeshi linaasi, ilikuwa ni siku saba tu baada ya Mapinduzi Matufuku ya Zanzibar ya Januari 12, 1964. Kwa hofu kubwa, ilibidi nchi hizi mbili – Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar – ziungane haraka Aprili 26, 1964.
Kwa upande wa Ghana, mwaka 1966 wakati Dk. Nkrumah akiwa ughaibuni kuhubiri umoja wa Afrika, alipelekewa taarifa kuwa amepinduliwa na jeshi. Ghana waliendelea na mapinduzi ya hapa na pale. Hadi sasa nchi hii imetawaliwa na marais 12 akiwamo Nii Amaa Ollennu, aliyechaguliwa na kuapishwa Agosti 7, 1970, lakini akapinduliwa Agosti 31, 1970 kwa maana kuwa aliongoza taifa hili kwa siku 24 tu.
Sitanii, nimegusia historia hii ya Ghana na Tanzania kwa nia ya kuonesha nchi zetu zilivyotawaliwa na ugomvi na majungu yalivyotuchelewesha katika maendeleo. Kwa Tanzania, ukiacha hiyo migogoro niliyoitaja, mwaka 1984 ilikuwapo migogoro mingine miwili mikubwa – kuchafuka kwa hali ya hewa Zanzibar na jaribio la mapinduzi.
Hapa, mwaka 1984; aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, aliondolewa madarakani na kuwekwa kizuizini. Watu walioongoza uasi wakiwamo akina Uncle Tom, Muchwampaka na wengine ambao leo wanajihusisha na masuala ya soka, wakati huo walikimbia nchi na JWTZ ikawadhibiti vilivyo.
Mwaka 1988, ndani ya CCM walishikana uchawi. Tukashuhudia akina Seif Shariff Hamad, Shaaban Mloo na wenzake wakitoswa kutoka CCM na hao ndiyo waliokwenda kuunda Chama cha Wananchi (CUF). Chokochoko zimeendelea ndani ya CCM. Mwaka 2002 ndipo lilipoanza hili zengwe la kutenganisha kofia.
Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete akiwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na pia akiwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, mwaka 2002 alizushiwa kuwa alitaka kutumia nguvu yake ya mtandao ndani ya chama kumvua Rais Benjamin Mkapa wadhifa wa Mwenyekiti, kwa nia ya kutenganisha kofia ya urais na uenyekiti wa chama.
Katika Kamati Kuu iliyoketi Zanzibar, Kikwete alilazimika kuwatolea uvivu waliokuwa wakisambaza uvumi huu kwa kuwaambia: “Mnaeneza mno majungu. Urais ni suala ambalo kama Mungu amekupangia utakuwa, na kama hakukupangia basi ujue hutokuwa.” Maneno yake yalitimia, kwani pamoja na mbinu nyingi, mwaka 2005 alifanikiwa kuwa Rais wa Tanzania.
Sitanii, mafundi wa uchonganishi ndani ya chama hicho walianza kupiga hesabu za mbali. Itakumbukwa kuwa mwaka 2006 nchi ilipata ukame mkubwa wa kutisha. Gridi ya Taifa ilikuwa inakabiliwa na tishio la kuzimika. Wataalamu wa siasa za uchokonozi wakaona huo ndiyo uliokuwa mwanya wa kupitisha ajenda yao ovu ya kuwagombanisha Kikwete na Edward Lowassa.
Walianza kumwaminisha Kikwete kuwa Lowassa anamhujumu. Wakafika mahala wakahamishia ajenda hiyo kwenye Richmond. Narudia, hadi leo Richmond haijawahi kulipwa hata senti tano ya Serikali, lakini akina Harrison Mwakyembe wakaidanganya dunia na umma wa Watanzania kuwa Richmond ilikuwa inalipwa Sh milioni 152 kila siku. Uongo huu umeendelea kuwapo, na Mwakyembe hachukuliwi hatua yoyote kwa kulidanganya Taifa.
Yaliyotokea tunayafahamu kwamba Lowassa alilazimika kujiuzulu uwaziri mkuu, Alhamisi, Februari 7, 2008. Kundi la wapenda ugomvi wakaona hiyo haifai na wala haijatosha, wakaanzisha ajenda ya “Rais wa Kipindi Kimoja.” Hoja hii wakaipenyeza kama moto wa nyika kukoleza uhasama kati ya Kikwete na Lowassa.
Wakasema Lowassa alikuwa amejipanga kugombea urais mwaka 2010. Lowassa hakuchukua fomu kugombea urais mwaka 2010, lakini bado hawakuridhika. Mwaka 2012 wakasema Lowassa ana kampeni ya kumvua madaraka Mwenyekiti Kikwete kwa nia ya kutenganisha kofia ya urais na uenyekiti. Mashushu walimwagwa Chimwaga sijapata kuona siku ya Mkutano Mkuu wa CCM mwaka 2012 kwa uongo uliofungashwa vyema wakidai Lowassa na wafuasi wake wanatoa hoja ya kumwondoa mwenyekiti madarakani.
Lowassa hakugombea uenyekiti kama walivyovumisha, walivyoona hiyo haikufanikiwa, wakaanzisha zengwe kuwa sasa Lowassa alikuwa anagombea urais kulipiza kisasa kwa Kikwete. Hawakupata kusema ni kisasi kipi. Yaliyopita ni historia na kwa kufupisha, hatimaye Lowassa alijitoa CCM na kwenda Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Sitanii, na hili ndilo lililonifanya niandike makala hii. Binafsi nilidhani baada ya Lowassa, aliyeonekana ni adui namba moja wa Mwenyekiti kuondoka CCM, hali ya hewa ingetulia.
Rais John Magufuli amechaguliwa; utaratibu unaandaliwa akabidhiwe uenyekiti sawa na alivyofanya Mwalimu Julius Nyerere, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.
Wafitini wameona hii ni fursa ya kuwafitinisha Kikwete na Magufuli. Baada ya Mchungaji Josephat Gwajima kusema wapo watu wanazunguka nchi nzima kushawishi wajumbe kuwa Kikwete aendelee kuwa Mwenyekiti na kwamba kofia ya urais na uenyekiti zitenganishwe, nimejaribu kufanya uchunguzi wa hapa na pale pamoja na kwamba niko mbali.
Nilichobaini; umbea huu umesambaa kwa kiasi kikubwa. Gwajima alichofanya ni kuwa mesenja tu, kwamba ameleta balaa nyumbani kwa mwenye nyumba. Barua ya nyumbani kapeleka ofisini na ya ofisini kaipeleka nyumbani. Si ajabu na naamini hata Christopher ole Sendeka amekwishausikia umbea huu, ingawa yeye kama msemaji wa chama anapaswa kuukanusha.
Wiki chache zilizopita, niliandika makala nikimsihi Rais Magufuli kuwapuuza au kuzipuuza kauli kwamba anahujumiwa na wauza sukari. Nilijenga hoja kuwa hatukuwa na takwimu sahihi. Tulidhani tunatumia sukari tani 420,000 na kwamba viwanda vyetu vina uwezo wa kuzalisha tani 320,000, hivyo tulipaswa kuagiza nje tani 100,000 tu, kumbe uhalisia; kwa ukosefu wa takwimu huenda tunatumia hadi tani 800,000 hivyo alipodhibiti uingizaji sukari holela tumeona mahitaji halisi na kuzalisha upungufu mkubwa ajabu.
Nilichokiona kwenye suala la sukari na kinachoendelea sasa kuwa Kikwete hataki kuachia madaraka, ni mpango uliosukwa kwa ustadi mkubwa na wapenda ugomvi, ambao hatimaye kama Rais Magufuli hatawabaini na kuwapuuza, ataanza kutumia nguvu kubwa kwenye ugomvi kama alivyofanya Kikwete tangu mwaka 2007, akaishia na Chuo Kikuu cha Dodoma na shule za kata walizojenga kabla ya ugomvi wake na Lowassa.
Sitanii, nimepitia historia ya migogoro katika uongozi wa nchi yetu kwa nia ya kuutahadharisha uongozi wa Rais Magufuli kuwa ugomvi wake ujikite kwenye kuanzisha viwanda na si umbea wa madaraka kama walivyoanza kufanya ndani ya chama. Watajenga hoja kuwa utakuwa rais wa kipindi kimoja si muda mrefu. Rais Magufuli ukifanya kosa la kusahau kukusanya kodi, kujenga viwanda na kuwaondoa Watanzania katika umaskini ukaingia kwenye mtego wa kugombana na wanasiasa wenzako, utamaliza miaka 10, na kila ukigeuka nyuma hutaona ulichofanya.
Narudia, Rais Magufuli wapuuze wote wanaotaka kukutengenezea ugomvi wa kisiasa. Wewe gombana na kukusanya kodi, kufumua mifumo ya kinyonyaji, kuboresha huduma ya afya, elimu, miundombinu (barabara, reli, viwanja vya ndege na ndege)…
Ajenda yako kuu ni TANZANIA YA VIWANDA, huko ndiko kuliko na ajira, kodi za uhakika na maendeleo ya kweli na si ugomvi wa kisiasa. Waambie wana-CCM kuwa waache majungu, wajenge nchi. Mungu ibariki Tanzania.