Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimetoa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 4.4 kwa shule ya elimu jumuishi ya Benjamin Mkapa ya jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa msaada huo ni mashine ya kukuzia maandishi kwa wanafunzi wenye uoni hafifu, hearing aid, kwa wenye usikivu hafifu na wanafunzi wenye albinism.
Msaada huo umekabidhiwa leo na Mkuu wa chuo hicho Profesa Edda Tandi Lwoga kwa Mkuu wa shule ya sekondari ya Benjamin Mkapa, Joseph Deo.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Profesa Lwoga aliomba wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia shule hiyo kwani inamahitaji mengi.
Alisema chuo hicho nkikongwe nchini ni mashuhuri kwa kutengeneza wataalamu wa masuala ya biashara na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na metrolojia.
Alisema CBE imezungukwa na shule nyingi za sekondari na kwamba kila mwaka wamekuwa wakianisha shule ambazo huenda kutoa msaada kama sehemu ya kurudisha faida kwa jamii inayowazunguka.

“Tunaona umuhimu wa kuboresha mazingira ya kusomea kuanzia huku chini kwenye sekondari kwasababu tunaamini elimu ikiboreshwa kuanzia huku chini huku juu mambo yanakuwa rahisi tu,” alisema
“Mwaka huu wakati tunasherehekea siku ya jinsia tuliainisha mahitaji ya shule ya Benjamin Mkapa na tuliona mlivyo na mahitaji mengi sana tukaona hii ni shule muafaka ya kupata msaada wa CBE kwa sababuinawanafunzi wengi mahitaji maalum kwa hiyo,” alisema Prof Lwoga
Mkuu wa shule hiyo, Joseph Deo aliishukuru CBE kwa msaada wa mashine ya kurudufia kwani walikuwa wanajipanga kutafuta fedha za kununua mashine hiyo.

Alisema kwa muda mrefu wanafunzi wenye uoni hafifu walikuwa wanapata shida kwa hiyo mashine hiyo ni ukombozi kwao kwani wataweza kusoma kama wenzao wasio na matatizo ya uoni.
“Sisi tulileta maombi ya vitu vingi sasa tukadhani mtachagua kusaidia vitu vidogo vidogo lakini mmechagua kutusaidia kitu kikubwa san asana mashine ya kurudufia ndiyo ilikuwa inatuumiza kichwa tunaipataje tunawashukuru sana,” alisema
Alisema shule hiyo ina wanafunzi 160 wenye usikivu hafifu hivyo alitoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kusaidia shule hiyo ili wanafunzi wenye uoni na usikivu hafifu wapate vifaa vya kuwasiaidia kwenye masomo.
“Kwa msaada huu wa mashine ya kukuzia maandishi hawa wanafunzi watafanya vizuri darasani kwasababu watakuwa wanafuatilia masomo kama wenzao na wale wenye usikivu hafifu vifaa vilivyotolewa vitawasaidia, tunaomba wadau wengine nao wajitoleee maana wanafunzi 120 bado wanahitaji vifaa vya aina hiyo,” alisema.

Mkuu wa Kitengo cha Wanafunzi Wenye Majitaji Maalum shuleni hapo, Alfonsi Tangaza, alisema kuna shule nyingi zenye mahitaji maalum lakini hatua ya CBE kuona shule hiyo kama kipaumbele chao ni jambo ambalo limewafariji sana.
“Hapa kuna wanafunzi wengi wenye uoni hafifu ambao wanahitaji kukuziwa maandishi kwenye mitihani yao na nilikuwa namsumbua sana mkuu wa shule kuhusu mashine hii ambayo mmeleta nawashukuru sana,” alisema

