Na Mwandishi Wetu

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimewataka wazazi nchini kuwahamasisha watoto wao kuchangamkia mafunzo ya sayansi ya vipimo na viwango kwani soko la ajira liko wazi kwa nchi za Afrika Mashariki.

Hayo yamesemwa jana chuoni hapo na Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Tandi Lwoga, wakati akizungumzia siku ya vipimo duniani ambayo huadhimishwa kila Mei 20 ya kila mwaka.

Kauli mbiu ya siku ya vipimo duniani mwaka huu ni  “Vipimo vinavyosaidia mfumo wa chakula duniani,”  na inasisitiza jukumu muhimu ambalo vipimo vinafanya  katika kuhakikisha ubora na usalama wa chakula.

Kaimu Makamu Mkuu wa chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), (Taaluma), kushoto Dk. Nasib Rajabu, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Profesa Tandi Lwoga na Profesa Emmanuel Munishi ambaye ni Makamu Mkuu wa chuo hicho, Utawala na Fedha wakimsikiliza Mhadhiri wa Idara ya Vipimo na Viwango (Kulia) akizungumza kuhusu siku ya vipimo duniani ambayo hufanyika kila Mei 20 ya kila mwaka.

Amesema kozi hiyo inatolewa na chuo hicho pekee kwa nchi za Afrika Mashariki hivyo kuwa rahisi kwa wanafunzi wanaohitimu kupata ajira kwenye nchi zinazoizunguka Tanzania na kwingineko duniani.

Amesema chuo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo hayo kuanzia ngazi ya cheti, astashahada na shahada ya sayansi ya vipimo na kwamba kwa sasa kuna wanafunzi 761 wanaosomea kozi hiyo.

Amesema wamekuwa wakifanya utafiti kuhusu ubora wa miundombinu pamoja na kutambua maeneo ya kukuza teknolojia na njia mpya ya za upimaji wa bidhaa mbalimbali.

“Pia tumekuwa tukiboresha mitaala na mwaka jana tuliboresha mitaala ili iendane na sayansi na teknolojia ya vipimo na viwango duniani kwa hiyo tunakaribisha mlete vijana wenu waje kusoma haya mafunzo ambayo tumeyaboresha zaidi,” amesema

Amesema pia wamekuwa wakitoa mafunzo hayo kwa vitendo na kwamba wameanzisha mradi wa ujenzi wa ghorofa 10 ambalo litaitwa Metrology Complex ambapo kutakuwa na maabara ya kisasa ambayo itathibitishwa kimataifa ili kutoa mafunzo.

Amesema watakuwa pia kutakuwa na karakana ambapo wanafunzi wa sayansi ya vipimo watakuwa wakisoma kwa vitendo ambapo pia kutakuwa na kumbi za mihadhara na kwamba jingo hilo litakauwa na uwezo wa kuchukua zaidi ya wanafunzi 4,460.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Profesa Tandi Lwoga akizungumza kuhusu siku ya vipimo duniani inayoadhmishwa kila tarehe 20 Mei ya kila mwaka. Kushoto ni Kaimu Makamu Mkuu wa chuo (Taaluma), Dk. Nasib Rajabu.

Amesema lengo ka kusherehekea Siku ya vipimo duniani ni kunatambua umuhimu wa vipimo sahihi kwenye biashara duniani.

Amesema wakati idadi ya watu duniani inafikia bilioni 8, ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote kuhakikisha kuwa usambazaji wa chakula na bidhaa mbalimbali ni salama.

“Tunakabiliwa na changamoto zinazozidi kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na sababu nyingine za mazingira, ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote kuwa na vipimo sahihi na vya kuaminika,” amesema.

Amesema CBE itaadhimisha Siku ya vipimo duniani kama nchi nyingine na kwamba  watakuwa na matukio na shughuli mbalimbali zinazoonyesha umuhimu wa vipimo sahihi.

 Ametaja shughuli hizo kuwa ni pamoja na semina, warsha, maonyesho, na mihadhara ya umma kwa kwa kushirikiana na wanasayansi, wataalamu wa vipimo na viwango kote nchini.