Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro
MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Rebecca Nsemwa, amekipongeza Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kwa kuanzisha kozi ya uchunguzi wa masuala ya ufisadi na kupambana na rushwa.
Amesema kozi hiyo itasiadia kwa kiwango kikubwa nchi katika mapambano dhidi ya ufisadi na rushwa kwani watu wengi watakuwa na uelewa kuhusu madhara ya rushwa na namna ya kupambana nayo.
Ameyasema hayo leo kwenye mafunzo ya muda mafupi ya kuwajengea uwezo watumishi wa sekta ya umma na sekta binafsi katika masuala ya kupambana na rushwa.
Amesema suala la rushwa ni changamoto hapa nchini kwa upatikanaji wa haki kwenye vyombo vya kutoa maamuzi ikiwemo mahakama na Polisi.
Ametaja vyombo vingine vinavyotajwa kwa rushwa kuwa ni pamoja na vile vinavyotoa huduma za kijamii ikiwemo Hospitali ambapo mtu hawezi kupata huduma bila kutoa rushwa.
Mkuu wa chuo hicho Profesa Edda Lwoga, alisema tayari CBE imeshaanzisha mchakato wa kutoa elimu hiyo umeshaanza ambapo aliwakaribisha watu kutoka mataifa mbalimbali kuja kujifunza chuoni hapo.
Alifafanua kuwa ili kuhakikisha taratibu za kozi hiyo zinafuatwa watashirikiana na Baraza la Taifa la Mitihani NECTA ili kupata Mtaala ambao utakaokidhi vigezo vya kufundishia.
Mkuu huyo wa chuo, amesema kozi hiyo itaanza kufundishwa kwa ngazi ya cheti na baadaye wanafunzi hao watapatiwa mitihani itakayotambulika hapa nchini na ndani ya nchi na kumfanya mhitimu kufanya kazi sehemu yoyote.
“ Kwa sasa CBE tunatoa kozi fupi kwa taasisi za serikali na binafsi kuhusu uchunguzi wa rushwa na ufisadi lakini kwa sasa tumejipanga kuanza kutoa kozi za muda mrefu kuanzia cheti na kuendelea tunaandaa mtaala ukikamilika tunapeleka Baraza la mitihani kwaajili ya kupitiwa” alisema Profesa Lwoga.
Naye Wakili na Mkufunzi wa masuala ya ufisadi kutoka CBE, Stella Cosmas, alisema baada ya kuanzisha kwa kozi hiyo ya muda mrefu ya cheti wanafunzi watafanya mitihani ya kimataifa utakaowezesha watanzania wengi kutambulika kimataifa.
Amesema kwa sasa taaisisi nyingi zimeajili kufanya kazi hiyo kutoka nje wakati wapo hapa nchini vijana wengi ambao wakipatiwa elimu hiyo wanawaweza kufanya kazi nzuri tena kwa ushindani mkubwa.