Category: MCHANGANYIKO
Mawaziri wameondoka, Kikwete rekebisha sheria
Mawaziri wameondoka, Kikwete rekebisha sheria
Wiki iliyopita kwa mara nyingine nchi yetu imepata mtikisiko. Imepata mtikisiko kutokana na mawaziri wanne kupoteza nyadhifa zao. Haya yametokea Ijumaa ya Desemba 20, 2013. Mawaziri hawa; Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Mathayo David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) na Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), wameacha sura mbili.
Taarifa kamili ya Kamati ya Lembeli iliyowang’oa mawaziri wanne wa JK
Taarifa kamili ya Kamati ya Lembeli iliyowang’oa mawaziri wanne wa JK
Desemba 20, mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, aliwasilisha bungeni mjini Dodoma taarifa ya kamati hiyo kuhusu tathmini ya matatizo yaliyojitokeza katika Operesheni Tokomeza. Gazeti Jamhuri tumeamua kuchapisha taarifa hiyo neno kwa neno mwanzo hadi mwisho kama ifuatavyo:
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, wakati Bunge likijadili hoja ya kuahirisha shughuli za Bunge ili kujadili jambo muhimu la dharura kwa mujibu wa Kanuni ya 47 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2013, iliyowasilishwa na Mhe. Said Nkumba, Mbunge wa Sikonge kuhusu Mgogoro kati ya Wafugaji na Wakulima, Hifadhi na Uwekezaji, Mheshimiwa Spika alitoa Uamuzi ‘Speakers Ruling’ kuwa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ishughulikie kazi ya kutathmini na kuangalia jinsi Mpango wa Kupambana na Majangili ulivyopangwa na kutekelezwa na Serikali kupitia ‘Operesheni Tokomeza’.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Taarifa Rasmi za Bunge za tarehe 1 Novemba 2013, wakati Bunge likihitimisha Hoja ya Kuairisha Shughuli za Bunge, Mhe. Spika alitoa uamuzi ufuatao:-
…Kamati ile ya kawaida ya Maliasili itaendelea na kazi yake ya kufanya tathmini ya kuangalia jinsi mpango ule wa Kupambana na Majangili ulivyopangwa na ndani yake itashughulikia kama kulikuwa na uzembe ama kuna watu wanahusika katika kuondoa maisha ya watu kwa sababu za uzembe …
1.1 Kuundwa kwa Kamati Ndogo ya Uchunguzi
Mheshimiwa Spika, kufuatia uamuzi ulioutoa tarehe 01 Novemba, 2013 Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ilikutana Dodoma tarehe 9 Novemba, 2013 kwa lengo la kujadili utaratibu wa kutekeleza jukumu hilo.
Katika kikao hicho Kamati iliazimia kuunda Kamati Ndogo kwa mujibu wa Kanuni ya 117(18), ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Tole la 2013 ili iweze kushughulikia suala hilo kikamilifu.
1.2 Hadidu za Rejea, Wajumbe wa Kamati na muda wa kazi
Mheshimiwa Spika, Kamati Ndogo ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyoundwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kwa agizo lako la tarehe 01 Novemba, 2013, ilipewa Hadidu za Rejea Nne (4) zifuatazo:-
1) Kutathmini na kuangalia jinsi Mipango ya Kupambana na Majangili ilivyopangwa;
2) Kuangalia kasoro zilizojitokeza katika kutekeleza mpango huo;
3) Kutathmini iwapo kulikuwa na uzembe katika kutekeleza Operesheni Tokomeza ambao ulisababisha watu wasio na hatia kupoteza maisha na mali zao; na
4) Kuchunguza migogoro ya Ardhi inayohusu Wakulima, Wafugaji na Wawekezaji kwenye maeneo yanayozunguka hifadhi.
Mheshimiwa Spika, Kamati hii ya uchunguzi iliundwa na Wajumbe Tisa (9) kama ifuatavyo:-
i. Mhe. James Daudi Lembeli, Mb.
ii. Mhe. Abdulkarim Esmail Shah, Mb.
iii. Mhe. Susan Limbweni Kiwanga, Mb.
iv. Mhe. Kaika Sanin’go Telele, Mb.
v. Mhe. Dk. Henry Daffa Shekifu, Mb.
vi. Mhe. Amina Andrew Clement, Mb.
vii. Mhe. Haji Khatibu Kai, Mb.
viii. Mhe. Muhammad Amour Chomboh, Mb.
ix. Mhe. Dk. Mary Mwanjelwa
Mheshimiwa Spika, Sekretarieti iliyohudumia Kamati Ndogo ya Uchunguzi iliundwa na Wajumbe wafuatao:-
i. Ndg. Theonest K. Ruhilabake
ii. Ndg. Gerald S. Magili
iii. Ndg. Chacha T. Nyakega
iv. Ndg. Stanslaus W.Kagisa
Mheshimiwa Spika, Kamati Ndogo ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilitakiwa kutekeleza majukumu yake na kuwasilisha ripoti katika Mkutano wa Kumi na Nne (14) wa Bunge. Hivyo basi, baada ya uteuzi huo, Wajumbe wa Kamati Ndogo walipanga kuanza kazi tarehe 25 Novemba, 2013 na kuikamilisha ifikapo tarehe 15 Desemba, 2013.
1.3 Njia zilizotumika katika kukamilisha kazi
Mheshimiwa Spika, Kamati Ndogo ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilitekeleza majukumu yake kwa kuongozwa na Hadidu za Rejea ilizopewa kwa kufanya rejea na kuzingatia yafuatayo:-
a) Kusoma na kuchambua nyaraka zilizoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuandaa na kutekeleza Operesheni Tokomeza nchini. Nyaraka hizo ni hizi zifuatazo:-
i. Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza (Concept Paper)
ii. Tathmini ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
iii. Sheria ya Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge (Na.3) 1988
iv. Sheria ya Wanyamapori (Na. 5) 2009
v. Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la mwaka 2013
b) Kufanya mahojiano na watu mbalimbali:-
i. Waziri wa Maliasili na Utalii
ii. Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii
iii. Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori
iv. Mkurugenzi Msaidizi Kikosi wa Dhidi ya Ujangili
v. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
vi. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)
vii. Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)
viii. Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Hifadhi za Misitu (TFS)
ix. Mahojiano na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge
c) Kuzuru maeneo yaliyoanishwa katika Taarifa ya Wizara kuhusiana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na yale yenye migogoro kati ya Wakulima au Wafugaji na Wawekezaji katika maeneo ya hifadhi kwa lengo la kuhakiki (verify) masuala yaliyoainishwa kupitia uchambuzi uliofanywa na Kamati.
2.0 KUPOKEA NA KUCHAMBUA NYARAKA MBALIMBALI ZILIZOHUSU OPERESHENI TOKOMEZA
Mheshimiwa Spika, Hadidu Rejea ya kwanza iliitaka Kamati Ndogo ya Ardhi, Malisili na Mazingira, kufanya tathmini na kuangalia jinsi mipango ya kupambana na majangili ilivyopangwa. Ili kukamilisha jukumu hilo, Kamati ilifanya yafuatayo:-
a) Kupitia na kuchambaua Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza (Concept Paper) ulioandaliwa na Wizara
b) Kupitia na kuchambua Tathmini ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
2.1 Uchambuzi kuhusu Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, katika kuchambua Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza kwa lengo la kupata uelewa zaidi wa namna operesheni hiyo ilivyopangwa na kutekelezwa, Kamati ilibaini kuwa, mpango huo uliandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na ulikuwa na mambo yafuatayo:-
i. Ukubwa wa tatizo la ujangili
ii. Aina za ujangili na sababu za ukuaji wake
iii. Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ujangili
iv. Malengo ya Operesheni Tokomeza
v. Njia zilizotumika kutekeleza operesheni
vi. Maeneo ya operesheni na gharama za utekelezaji
vii. Tamko la Serikali kusitisha Operesheni Tokomeza
2.1.1 Ukubwa wa tatizo la ujangili
Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini kuwa, tatizo la ujangili ni kubwa na limekuwa likisababisha idadi ya Tembo iendelee kupungua nchini. Takwimu zinaonesha kuwa, idadi ya Tembo
imepungua kutoka 350,000 (miaka ya 1970) hadi kufikia 55,000 (mwaka 1989). Juhudi za kukabiliana na hali hiyo kupitia Operesheni zilizowahi kutekelezwa huko nyuma zilisaidia kuongeza idadi ya
Tembo hadi 141,000 (mwaka 2006) ingawa ilishuka tena hadi kufikia 110,000 (mwaka 2009).
2.1.2 Aina za ujangili na sababu za ukuaji wake
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya Serikali, vitendo vya ujangili vinavyofanyika nchini vimegawanyika katika makundi mawili yafuatayo:-
i. Ujangili wa Kujikimu (subsistance poaching)
Aina hii ya ujangili inahusisha watu wenye kipato kidogo na hulenga zaidi katika kujipatia kitoweo na fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji mengine. Ujangili wa aina hii huathiri zaidi wanyama wanaoliwa na si Tembo.
ii. Ujangili wa Biashara (commercial poaching)
Aina hii ya ujangili inahusisha zaidi watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha na hulenga kupata nyara zenye thamani kubwa. Wanyama wanaoathiriwa zaidi na aina hii ya ujangili ni pamoja na Tembo, Faru, Simba na Chui.
Mheshimiwa Spika, taarifa ilibainisha kuwa, kuongezeka kwa masoko haramu katika nchi za Asia na Mashariki ya Kati ambayo yanatoa bei kubwa ya nyara hizo, imekuwa ni chachu ya kuimarika kwa mitandao inayojihusisha na ujangili (ndani na nje ya nchi) na hivyo kusababisha ongezeko kubwa la vitendo vya ujangili.
2.1.3 Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ujangili
Mheshimiwa Spika,Mpango Kazi waKupambana na Ujangili ulilenga kujikita katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ujangili wa wanyamapori na misitu. Mpango huo ulioelezewa kuwa niwa muda mrefu na kusimamiwa na kikosi kazi cha Taifa (national task force),umeanisha maeneo yafuatayo kuwa ndiyo yaliyoathirika zaidi:-
i. Pori la Akiba Selous
ii. Hifadhi ya Taifa Serengeti, Pori la Akiba Maswa na Pori Tengefu la Loliondo.
iii. Hifadhi ya Taifa Katavi na Mapori ya Akiba Rukwa na Lukwati.
iv. Hifadhi ya Taifa Mikumi
v. Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi za Taifa Tarangire na Ziwa Manyara.
vi. Mapori ya Akiba Burigi, Biharamuro, Ibanda na Rumanyika.
vii. Mapori ya Akiba Moyowosi, Kimisi, Ugalla na Hifadhi ya Misitu Luganzo.
2.1.4 Malengo ya Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, Operesheni Tokomeza ambayo ilizinduliwa rasmi tarehe 04 Oktoba, 2013 ilikuwa na malengo yafuatayo:-
i. Kuzuia vitendo vya ujangili ndani na nje ya Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro na Misitu ya Hifadhi na kufanya operesheni maeneo yote yaliyoathiriwa na ujangili.
ii. Kuwatambua mapema majangili na kujua nyendo zao ndani na nje ya maeneo ya hifadhi.
iii. Kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wafanyabiashara haramu wa nyara za Serikali na mazao ya misitu.
iv. Kuvunja mitandao ya wafadhili, wanunuzi wadogo na wakubwa pamoja na mawakala wa biashara haramu ya nyara za Serikali na mazao ya misitu.
v. Kufuatilia na kukamata mali za majangili zilizotokana na biashara haramu ya nyara za Serikali na mazao ya misitu.
2.1.5 Njia zilizotumika kutekeleza Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini kuwa, Mpango Kazi wa Serikali kuhusiana na Operesheni Tokomeza, uliainisha kuwa operesheni hiyo itaendeshwa kwa kutekeleza mambo yafuatayo:-
i. Kufanya uchambuzi wa kina wa watuhumiwa wa mtandao wa ujangili wa nyara za Serikali na wavunaji na wasafirishaji haramu wa mazao ya misitu.
ii. Kuwakamata watuhumiwa wote waliobainishwa kwenye taarifa za kiintelijensia.
iii. Kupiga picha na kuchora ramani ya eneo la tukio kwa kila mtuhumiwa (sketch map).
iv. Kuhoji na kuandika maelezo ya watuhumiwa wa ujangili wa nyara za Serikali na wavunaji na wasafirishaji haramu wa mazao ya misitu.
v. Kukusanya na kuhifadhi vielelezo vyote vitakavyokamatwa kutoka kwa majangili kwa ajili ya kujenga ushahidi mahakamani.
vi. Kuandika maelezo ya mashahidi na askari wakamataji kwa ajili ya kujenga ushahidi mahakamani.
vii. Kuandaa mashitaka dhidi ya watuhumiwa na kuwapeleka mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
2.1.6 Maeneo ya Operesheni na gharama za utekelezaji
Mheshimiwa Spika,Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza ulianisha kuwepo awamu mbili za utekelezaji ambazoni; Mpango Kazi wa Muda Mfupi na Mpango Kazi wa Muda Mrefu.
Katika Mpango Kazi wa Muda mfupi itafanyika operesheni maalum katika maeneo yote ya ndani na nje ya hifadhi za wanyamapori na misitu nchi nzima. Maeneo hayo yaligawanywa katika kanda 12 za utekelezaji kama ifuatavyo:-
i. Selous, Mikumi, Udzungwa, Lukwika/ Lumesule na Liparamba,
ii. Burigi/Biharamuro, Ibanda/Rumanyika na Rubondo,
iii. Moyowosi, Ugalla na Lugazo,
iv. Serengeti, Loliondo, Maswa, Ikorongo na Kijeshi,
v. Kilimanjaro, Arusha, Mkomazi/Umba, Simanjiro na Longido,
vi. Tarangile, Manyara, Karatu/Ngorongoro, Swagaswaga na Mkungunero,
vii. Rungwa, Ruaha, Mpanda – Kipengele,
viii. Rukwa, Lukwati, Katavi, Lwafi, Piti na Wembere,
ix. Mahale na Gombe,
x. Saadani na kwenye maeneo yenye misitu ya mikoko,
xi. Pori Tengefu la Handeni, Kilindi na Mkinga na
xii. Msitu wa Kazimzumbwi, Kisarawe, Rufiji na Mkuranga,
Mheshimiwa Spika, ilianishwa kuwa, awamu ya kwanza ya Mpango Kazi wa muda mfupi ingegharimu jumla ya Tshs. 3,968,168,667/= ambazo zingechangwa na Taasisi za wanyamapori (WD, TANAPA, NCAA na TFS) kwa kila moja jumla ya Tshs. 992,042,167/=
2.1.7 Tamko la Serikali kusitisha Operesheni
Mheshimiwa Spika, kufuatia michango na malalamiko ya Waheshimiwa Wabunge wakati wakichangia hoja iliyotolewa na Mhe. Said Nkumba Mbunge wa Sikonge, pamoja na maagizo ya Bunge kutaka Serikaliitoe maelezo kuhusu hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge, Serikali ilitoa Tamko la kusitisha Operesheni Tokomeza tarehe 01 Novemba, 2013.
2.2 Uchambuzi wa Taarifa ya awali ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, taarifa hii ya awali kuhusiana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ilikuwa na mambo yafuatayo:-
i. Washiriki wa operesheni
ii. Awamu za operesheni
iii. Mafanikio ya operesheni
iv. Idadi ya watuhumiwa na kesi zilizofunguliwa
v. Changamoto za operesheni
2.2.1 Washiriki wa Operesheni
Mheshimiwa Spika, Operesheni Tokomeza ilihusisha jumla ya washiriki 2,371 kutoka vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa mgawanyo ufuatao:-
i. Wanajeshi (885) kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania,
ii. Askari (480) kutoka Jeshi la Polisi,
iii. Askari (440) kutoka Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU)
iv. Askari Wanyamapori (383) kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)
v. Askari (99) kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS)
vi. Askari Wanyamapori (51) kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)
vii. Waendesha Mashitaka (23) na
viii. Mahakimu (100)
2.2.2 Awamu za Operesheni
Mheshimiwa Spika, Operesheni Tokomeza ilipangwa kutekelezwa katika awamu Nne (4) kama ifuatavyo:-
i. Awamu ya kwanza ambayo ililenga kusaka Silaha za Kivita na Meno ya Tembo kutoka miongoni mwa wanaojihusisha na vitendo vya ujangili.
ii. Awamu ya pili ambayo ililenga kusaka silaha zisizomilikiwa kihalali na zile zinazomilikiwa kihalali lakini zinasadikiwa kutumika kwenye vitendo vya ujangili.
iii. Awamu ya tatu, ambayo ililenga kutafuta yalipo Maghala ya Nyara, kusaka Wafadhili na Wanunuzi wa nyara hizo na kuwabaini watu wanaowakingia kifua wahusika wa vitendo vya ujangili.
iv. Awamu ya nne, ambayo ililenga kukamata Nyara nyingine mbali na Meno ya Tembo na kuhakikisha watu walio katika makundi yafuatayo wanakamatwa:-
– Wawindaji haramu,
– Wavunaji haramu wa mazao ya misitu,
– Watu wanaolisha Mifugo ndani ya hifadhi, na
– Watu waliojenga ndani ya maeneo ya hifadhi
2.2.3 Mafanikio ya Operesheni Tokomeza
a) Idadi ya watuhumiwa na kesi zilizofunguliwa
Mheshimiwa Spika, tangu kuanza kutekelezwa kwaOperesheni Tokomeza (tarehe 04 Oktoba, 2013 hadi ilipositishwa (tarehe 01 Novemba, 2013) jumla ya kesi 687 zilifunguliwa zikiwahusisha watuhumiwa 1,030 katika maeneo yote kama ifuatavyo:-
i. Kanda ya Kwanza kesi 105 zikiwahusisha watuhumiwa 105
ii. Kanda ya Pili kesi 370 ambazo zilihusisha watuhumiwa 375
iii. Kanda ya Tatu kesi 165 zilizohusisha watuhumiwa 498
iv. Kanda ya Nne kesi 47 zilizohusisha watuhumiwa 52
Mheshimiwa Spika, hadi wakati Operesheni Tokomeza inasitishwa tarehe 01 Novemba, 2013 kati ya Kesi 687 zilizokuwa zimefunguliwa ni 132 tu ndiyo zilikuwa zimetolewa maamuzi na 555 bado zilikuwa katika hatua ya kusikilizwa. (Tazama Kiambatisho Na. 1)
i. Kukamatwa kwa meno ya Tembo 211 yenye uzito wa kilo 522, meno ya Ngiri 11, Mikia ya wanyama mbalimbali 36, Ngozi za wanyama mbalimbali 21, Pembe za Swala 46, Mitego ya wanyama 134, ng’ombe 7,621 Baiskeli 58, Pikipiki 8 na Magari 9.
ii. Kupungua kwa kasi ya mauaji ya Tembo kutoka wastani wa Tembo wawili (2) kwa siku hadi tembo wawili tu katika kipindi chote cha operesheni (siku 29).
iii. Hadi kufikia tarehe 11 Novemba, 2013 jumla ya Bunduki za Kijeshi 18 zilikamatwa, Bunduki za kiraia 1579, Risasi 1964, Mbao vipande 27,913, Mkaa Magunia 1242, Magogo 858 na Misumeno 60. Vyote hivyo vilikamatwa katika Kanda ya Nne.
2.2.4 Changamoto za Operesheni Tokomeza
a) Vifo vilivyotokea wakati wa Operesheni
Mheshimiwa Spika,Taarifa ya Serikaliiliainisha vifo kamachangamoto kubwa iliyojitokeza wakati wautekelezaji wa Operesheni Tokomeza kutokana na watumishi 6 na watuhumiwa 13 kupoteza maisha. (Tazama Kiambatisho Na. 2)
b) Hujuma dhidi ya Operesheni
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Serikali ilifafanua kuwa,utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ulikumbwa na vitendo vya hujuma kutoka kwa baadhi ya makundi ya jamii kama ifuatavyo:-
i. Mamluki miongoni wa washiriki wa Operesheni. Mfano; kukamatwa kwa Askari Polisi na Askari Wanyamapori wakisindikiza gari lenye Meno ya Tembo, na gari la Serikalikutumika kusafirisha Meno ya Tembo.
ii. Vyombo vya Habari kutumika kuvuruga operesheni kwakueneza propaganda zilizolenga kushawishi wananchi kupinga operesheni hiyo.
iii. Baadhi ya wamiliki wa silaha kutuhumiwa kutoa silaha zao ili zitumike kwa ajili ya vitendo vya ujangili.
C) Tuhuma dhidi ya Operesheni
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Serikai ilifafanua kuwa,ingawa lengo la operesheni lilikuwa ni kupambana na vitendo vya ujangili dhidi ya raslimali za Taifa, utekelezaji wake ulikumbwa na tuhuma kadhaa zikiwemo zifuatazo:-
i. Mateso dhidi ya watuhumiwa yaliyosababisha maumivu, kupata ulemavu wa kudumu na hata wengine kupoteza maisha (Mfano; Marehemu Emiliana Gasper Maro wa Gallapo – Babati).
ii. Matumizi mabaya ya Silaha (Mfano; Mzee wa miaka 70 kuuawa kwa kupigwa risasi 3).
iii. Nyumba za wananchi kuchomwa moto (Mfano; Kijiji cha Kabage Wilaya ya Mpanda – Katavi).
iv. Mifugo kuuawa kikatili kwa kuchomwa moto na kupigwa risasi (Mfano; Ng’ombe 60 kuuawa kwakupigwa risasi).
v. Kukosekana kwa mwongozo wa utoaji wa taarifa jambo lililosababisha viongozi husika wa Serikali kutopewa taarifa muhimu za utekelezaji wa Operesheni. (Mfano; Waziri wa Maliasili naUtalii, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri wa Ulinzi na Wakuu wa Mikoa na Wilaya).
vi. Askari waliotuhumiwa kukiuka taratibu kukataa kutoa ushirikiano wa kutosha pale walipohitajika kufanya hivyo.
vii. Kutoshirikishwa kwa viongozi wa Mamlaka za Utawala katika ngazi za Mikoa na Wilaya.
3.0 MAHOJIANO BAINA YA KAMATI NA WIZARA PAMOJA NA WABUNGE
Mheshimiwa Spika, Kamati ilifanya mahojiano na makundi yafuatayo:-
i. Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake
ii. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
iii. Waheshimiwa Wabunge
3.1 Mahojiano baina ya Kamati na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha wajumbe wa Kamati wanapata uelewa wa kutosha kuhusiana na Operesheni Tokomeza, Kamati liagiza uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii ukiongozwa na Waziri, kufika mbele ya Kamati ili kueleza namna Operesheni Tokomeza ilivyoandaliwa na kutekelezwa hadi ilipositishwa kupitia tamko la Serikali lililotolewa Bungeni tarehe 01 Novemba, 2013.
Mheshimiwa Spika, Kamati ilikutana na Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na timu yake kwa siku tatu, tarehe 28- 29 Novemba, na tarehe 01 Desemba, 2013. Katika vikao hivyo, Waziri aliieleza Kamati juu ya Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza, raslimali (watu na fedha) pamoja na tathmini iliyofanyika kwa kipindi ambacho Operesheni Tokomeza ilitekelezwa.
Mheshimiwa Spika, katika mahojiano na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Khamis Kagasheki, Mb na watendaji wake Kamati ilifahamishwa yafuatayo:-
i. Kwamba Operesheni Tokomeza ilikuwa ya kijeshikama alivyonukuliwa katika Taarifa Rasmi za Bunge (Hansard) akisema: “…Operesheni ilikuwa ya kijeshi. Ilikuwa ya kijeshi kwa sababu ilitekelezwa kwa amri ya jeshi Namba 0001/13 iliyotolewa tarehe 28 Septemba, 2013 na kusainiwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi…”
ii. Kwamba, kinadharia inaonekana kwamba, Waziri wa Maliasili na Utalii ndiye alikuwa Msemaji Mkuu, lakini kiuhalisia hakuwa msemaji mkuu wa Operesheni Tokomeza kama alivyonukuliwa katika Taarifa Rasmi za Bunge akisema; “…kinadharia inaweza ikasemekana kwamba mimi ndiye msemaji mkuu, lakini mimi sikuwa msemaji mkuu wa Operesheni Tokomeza …”
iii. Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ulisimamiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
iv. Taarifa za mwenendo wa operesheni zilikuwa zinapelekwa moja kwa moja kwa Mkuu wa Majeshi na kwamba, hazikumfikia Waziri wa Maliasili na Utalii.
v. Operesheni Tokomeza iliingiliwa na Wanasiasa.
vi. Pamoja na Mpango kazi huo kuandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa namna ambayo haieleweki Waziri hakuuona wala kuidhinisha rasimu ya mwisho ya Mpango huo. Hiyo ilidhihirika mbele ya Kamati kutokana na Waziri kukiri kwamba hakuuona wala kuudhinisha
3.1.1 Tathmini ya Kamati kuhusu majibu ya Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na watendaji wa Wizara
Mheshimiwa Spika,kwa kutumia tathmini ya awali ya nyaraka zilizowasilishwa pamoja na mahojiano na Waziri ilionekana kwamba, Operesheni Tokomeza iliandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini yake na kushirikisha vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Mheshimiwa Spika, licha Mpango wa Operesheni Tokomeza kuandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, hata hivyo utekelezaji wake ulisimamiwa na kuongozwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
Hatua ya jeshi kuchukua jukumu la kuongoza Operesheni Tokomeza, lilifanya viongozi wa Wizara kujiengua katika jukumu la kuongoza (ead agency) na badala yake kuacha jukumu hilo kwa Jeshi pekee jambo lililotafsiriwa kwamba, Operesheni Tokomeza ilikuwa ya kijeshi.
Mheshimiwa Spika, kupitia mahojiano ilibainika kwamba, hakukuwa na utaratibu mzuri wa kupashana habari kuhusiana na mwenendo mzima wa Operesheni Tokomeza jambo lililofanya baadhi ya wahusika kutotambua kikamilifu wajibu waokatika Operesheni hiyo.Mfano mzuri ni kwamba, licha ya kuelezwa kwenye Kanuni za Utendaji (Operational Guidelines)za Operesheni Tokomeza kwamba, Waziri wa Maliasili na Utalii ndiye atakuwa Msemaji Mkuu wa Operesheni Tokomeza, bado Mhe. Waziri hakutekeleza jukumu hilokwani alikwishatoa mapendekezo katika rasimu kwamba Msemaji Mkuu awe ni Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Aidha, Kamati ilibaini kuwa baadhi ya Watendaji wa juu wa Wizara walidaiwakukwamishautekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Maliasili na Utalii kutokana na kuingilia mawasiliano aliyokuwa anayafanya na baadhi ya Watumishi. Mfano ni majibizano kwa njia ya barua pepe kati ya Waziri na Katibu Mkuu, Waziri na Mkurugenzi wa Wanyamapori na pia Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Wanyamapori. Kwa mujibu wa majibizano hayo Waziri anaonekana kushangazwa na hatua ya Katibu Mkuu kuhoji hatua ya yeye kumuita mmoja wa mtumishi wa Wizara ofisini kwake. (Kiambatisho Na. 3)
Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa mfumo mzuri wa kupashana habari kwa pande husika kuhusu mwenendo mzima wa Operesheni Tokomeza, kulionekana kuathiri utaratibu mzima wa viongozi husika akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii, kupata taarifa zinazotakiwa kwa wakati. Hali hiyo ilichangia utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kukumbwa na athari ambazo zingeweza kuepukika iwapo kungekuwa na mfumo mzuri wa mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, kupitia mahojiano pia Kamati ilibaini uwepo wa hujuma kutoka kwa viongozi wa kisiasa na Serikali ambao kwa namna moja au nyingine walionekana kuhusishwa na Operesheni Tokomeza ama wao binafsi au ndugu zao.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa hujuma ambazo Kamati ilizibaini kupitia mahojiano naWaziri wa Maliasili na Utalii na Watendaji wake ni pamoja na:-
i. Baadhi ya watuhumiwa wenye mahusiano na viongozi wa kisiasa kutumia majina ya viongozi hao kuingilia utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
ii. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ujangili na biashara haramu ya nyara za Serikali.
iii. Baadhi ya Mawaziri kutoa kauli zenye kuingilia utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. (Mfano: kutoa maelekezo kwa wahusika wa Operesheni Tokomeza kwamba wasiguse viongozi wa kisiasa wa ngazi zote).
iv. Baadhi ya viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama kushiriki kudhoofisha utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kwa kusindikiza au kusaidia watuhumiwa wa ujangili kutoroka. (Mfano; viongozi wa Polisi wa Wilaya na Mikoa)
Mheshimiwa Spika, kubainika kwa hujuma hizo ni ishara tosha kwamba hata ndani ya Serikali yenyewe hakukuwa na dhamira ya dhati kwa baadhi ya kwa viongozi na watendaji katika kuhakikisha vita dhidi ya vitendo vya kijangili inapiganwa kikamilifu.
Hali hiyo ilisababisha utekelezaji wa operesheni kukumbwa na athari nyingi kama vile; wananchi kupoteza maisha, mifugo kuuawa kwa kuchomwa moto, njaa, kiu au kupigwa risasi), upotevu wa mali, nyumba kuchomwa moto na vitendo vya ukatili dhidi ya wananchi ambavyo vilikiuka haki za kibinadamu. Hali hiyo imesababisha utekelezaji wazoezi la Operesheni Tokomeza kutafsiriwa kwamba ulilenga wananchi wasio na hatia na kuacha wahusika wa ujangili.
3.2 Mahojiano baina ya Kamati na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 30 Novemba, 2013 Kamati ilikutana na kufanya mahojiano na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kubaini namna ilivyoshiriki katika Operesheni Tokomeza.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Dk. Emmanuel Nchimbi, Mb alieleza kuwa, operesheni hii ilikuwa na lengo la kutimiza azma (Commitment) ya Serikali iliyoitoa Bungeni kwamba, inakusudia kufanya Operesheni ya kupambana na majangili. Wizara yake ilishiriki kwa kutoa Askari Polisi 504 pamoja na baadhi ya vyombo vya usafiri na kwamba vyombo vya Ulinzi na Usalama vya nchi vilikuwa vikikutana mara kwa mara kwa lengo la kuandaa mkakati wa namna ya kushirikiana katika kutekeleza mpango huo wa vita dhidi ya ujangili.
Mheshimiwa Spika,Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alikiri kuwa, licha ya lengo la operesheni kuwa zuri, kulijitokeza changamoto kadhaa zilizotokana na baadhi ya washiriki wa operesheni kwenda kinyume na malengo yaliyokusudiwa kama vile; ukatili dhidi ya mifugo na vitendo vya unyanyasaji wa wananchi kwa kuwatesa kiasi cha kuwasababishia ulemavu wa kudumu au vifo.
Pia Mheshimiwa Waziri alikiri kwamba, kutokuwepo mfumo mzuri wa mawasiliano na Operesheni kuongozwa na jeshi, iliashiria kwamba taarifa za operesheni zilikuwa zinakwenda kwa Mkuu wa Majeshi – CDF moja kwa moja na hivyo kufanya pande zingine zinazohusika zisijue kinachoendelea.
3.2.1 Tathmini ya Kamati kuhusu majibu ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na watendaji wake
Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini kuwepo kwamawasiliano hafifu kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara nyingine zilizoshiriki katika operesheni hii.Pia,kukosekana kwa mfumo mzuri wa mawasiliano, kuliikosesha Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo iliandaa na kugharamia Operesheni Tokomeza,fursa ambazo zingeiwezesha kufanya tathmini kuhusu utekelezaji wa Operesheni hii.
Aidha, Kamati ilibaini kwamba, hatua ya kutoshirikisha Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya ililenga kutovujisha siri dhidi ya watuhumiwa wa ujangili. Hatua hiyo ilisababisha usumbufu mkubwa kwa viongozi wa mamlaka za utawala za Wilaya na Mikoa kutokana na kulaumiwa na wananchi kwa kushindwa kuwasaidia pale walipokumbwa na matatizo.
3.3 Mahojiano baina ya Kamati na Waheshimiwa Wabunge
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa suala hili liliibukia Bungeni baadaya wawakilishi wa wananchi kupaza sauti kuhusu athari zilizowakumba wapiga kura wao, Kamati iliona ni busara kuhoji baadhi ya Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja hii. Wabunge hao walitoa taarifa muhimu kuhusu vitendo vilivyofanyika katika maeneo yao wakati wa operesheni.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge walieleza kusikitishwa na namna ambavyo Operesheni Tokomeza ilikiuka malengo yaliyokusudiwa na badala yake ikanyanyasa wafugaji kwa kuangamiza mifugo yao na kuwaharibia mali zao kama vile; kuchoma moto nyumba, kupora fedha na vitu vingine. Mbunge mmoja alinukuliwa katika Taarifa Rasmi za Bunge akisema:-
“…badala ya Operesheni Tokomeza kusaka majangili, ikageuka kuwa Operesheni Tokomeza Ufugaji…”
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge waliieleza Kamati kuwa, siyo jambo la kawaida kwa watu wanaoagizwa kufanya jambo fulani kwenda kinyume na maagizo. Wakashauri kuwa, wahusika wote waliotenda kinyume namaagizo wachukuliwe hatua stahiki ili kuepusha vitendo vya aina hiyo visijirudie katika operesheni zitakazofuata. Pia Waheshimiwa Wabunge walishauri kasoro zilizojitokeza zirekebishwe na operesheni iweze kuendelea ili kutowapa mwanya majangili kujipanga upya.
3.3.1 Tathmini ya Kamati kuhusu majibu ya Waheshimiwa Wabunge Mheshimiwa Spika, kimsingi Waheshimiwa Wabunge wanaunga mkono Operesheni Tokomeza ambayo ililenga kukomesha vitendo vya kijangili na kunusuru raslimali za nchi hasa wanyamapori na misitu. Hata hivyo, walieleza kusikitishwa na vitendo vilivyojitokeza wakati wa utekelezaji wa operesheni na walisema haviwezi kuvumilika.
Mheshimiwa Spika, baada ya kupata taarifa mbalimbali kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge, mahojiano na viongozi na watendaji wa Wizara na kuzingatia taarifa zilizowasilishwa na Serikali, Kamati iliazimia kuzuru baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na Operesheni Tokomeza ili kufanya uhakiki.
4.0 KAMATI KUZURU MAENEO YALIYOATHIRIKA KWA AJILI YA KUHAKIKI (VERIFICATION/OUTREACH)
Mheshimwa Spika, kutokana na wingi wa maeneo pamoja na ufinyu wa muda, Kamati ilijigawa katika makundi matatu ili yaweze kutembelea baadhi ya maeneo yaliyoainishwa katika Taarifa ya Serikali ili kufanya tathmini (verification) kwa utaratibu ufuatao:-
4.1 Kundi la kwanza lilielekea Kanda ‘C’iliyohusisha maeneo yaliyoathiriwa na Operesheni Tokomeza katika Mikoa ya Shinyanga, Kagera, Tabora, Kigoma, Rukwa, Katavi na Singida.
Mheshimiwa Spika, kundi hili liliundwa na Wajumbe wafuatao:-
Mheshimiwa James Daudi Lembeli, Mb, Mheshimiwa Haji Khatibu Kai, Mb na Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mb.
4.2 Kundi la pili lilielekea Kanda ‘B’iliyohusisha maeneo yaliyoathiriwa na Operesheni Tokomeza katika Mikoa ya Simiyu, Mara, Arusha na Manyara.
Mheshimiwa Spika,kundi hili liliundwa na wajumbe wafuatao, Mheshimiwa Abdulkarim E. Shah, Mb, Mheshimiwa Henry Daffa Shekifu, Mb na Mheshimiwa Amina Andrew Clement, Mb.
4.3 Kundi la tatu lilielekea Kanda ‘D’iliyohusisha maeneo yaliyoathiriwa na Operesheni Tokomeza katika Mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa, Ruvuma na Mtwara.
Mheshimiwa Spika, kundi hili liliundwa na wajumbe wafuatao; Mheshimiwa Kaika Saning’o Telele, Mb, Mheshimiwa Muhammad Amour Chomboh, Mb na Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, ambaye hata hivyo hakushiriki kutokana na dharura.
Mheshimiwa Spika,kama ilivyoainishwa hapo juu lengo la Kamati kutawanyika Mikoani lilikuwa kutathmini athari zilizotokana na Operesheni Tokomeza ambayo iliendeshwa nchini kuanzia tarehe 04 Oktoba, 2013 hadi tarehe 01 Novemba, 2013.
Mheshimiwa Spika, ili kutimiza jukumu hilo kikamilifu, Kamati iliongozwa na taarifa zifuatazo;
i. Mpango Kazi wa Operesheni Maalum ya kupambana na Ujangili nchini,
ii. Taarifa ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza iliyotolewa na Serikali.
iii. Michango ya Waheshimiwa Wabunge kama ilivyonukuliwa katika Taarifa Rasmi za Bunge (Hansard).
iv. Madai yaliyotolewa na Wabunge kuhusiana na athari zilizotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
v. Maelezo yaliyotolewa na Mashahidi ambao walihojiwa na Kamati.
vi. Vielelezo vilivyowasilishwa na Mashahidi waliofika mbele ya Kamati.
5.0 MAKUNDI YA KAMATI YALIVYOTEKELEZA MAJUKUMU YAKE
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu hili, Kamati ilikutanana makundi yafuatayo:-
i. Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya
ii. Waheshimiwa Madiwani
iii. Waathirika wa Operesheni Tokomeza
5.1 Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya
Mheshimiwa Spika, Kamati ilikukutana na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya na kupokea taarifa iliyohusu hali ya Ulinzi na Usalama hususan wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
Mheshimiwa Spika, kwa sehemu kubwa taarifa za Ulinzi na Usalama za Wilaya zilisaidia kuanisha ma
Dk. Remmy Ongala bado anakumbukwa
Siku hazigandi. Nathubutu kusema hivyo kwani Desemba 13, 2013 ndiyo siku ambayo nguli Ramadhan Mtoro Ongala ‘Dk, Remmy’ alitimiza miaka mitatu tangu aiage dunia. Dk. Remmy alifariki usiku wa kuamkia Jumatatu, Desemba 13, 2010 nyumbani kwake Sinza jijini Dar es Salaam, baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na maradhi ya kisukari. Akawaacha wapenzi wake wa muziki wa dansi na Injili pia wananchi kwa ujumla katika dimbwi la majonzi yasiyosahaulika kutokana na tungo za nyimbo zake, ambazo hadi leo zinarindima katika vituo vingi vya redio hapa nchini na hata nje ya mipaka yetu.
Dunia inalilia mawazo sahihi ya Mandela
Usiku wa Desemba 5, 2013 dunia ilipata habari mbaya. Nasema ilipata habari mbaya ambazo kimsingi zilitarajiwa, ndiyo maana sikutumia neno mshituko. Mzee wetu Nelson Madiba Mandela aliaga dunia.
KAULI ZA WASOMAJI
JAMHURI linatufaa kuhusu JWTZ Hakika ni ukweli usiopingika kuwa habari zinazochapishwa kwenye Gazeti Jamhuri kuhusu vikosi vya askari wetu wa JWTZ wanaolinda amani nchini Congo zimekonga mioyo yetu na zimetuongezea shauku ya kulipenda jeshi letu, hasa sisi tuliopo mpakani…
Nazuiwa kumwona Jaji Mkuu Tanzania
Mhariri,
Nimekuwa nikifuatilia haki yangu katika mahakama kwa miaka 14 sasa bila mafanikio. Kwamba nimekuwa nikifanya jitihada za kuomba kukutana na Mheshimiwa Jaji Mkuu, lakini hadi sasa sijafanikiwa kutokana na kunyimwa nafasi hiyo na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.