Kampuni ya Tancoal inayochimba makaa ya mawe wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma imekubali kuilipa Kampuni ya Caspian shilingi bilioni 18.4 na kuvunja mkataba baada ya fedha hizo kuzuiliwa miaka miwili kutokana na utata wa kimasilahi.
Uchunguzi uliofanywa na Gazeti la JAMHURI umebaini kwamba mgogoro huo wa kimasilahi ulikuwa wa muda mrefu baada ya Tancoal kuitaka Kampuni ya Caspian kutafuta muafaka lakini walikuwa wakikataa kufanya hivyo kwa madai kuwa mkataba ulikwisha kusainiwa.
Naibu Meneja wa Tancoal – mgodi wa Ngaka, wilayani Mbinga, Edward Mwanga, amesema kilio chao kwa muda mrefu ni kutaka kukaa pamoja na Caspian ili kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama za uzalishaji kwa saa ili ziendane na hali halisi ya uzalishaji wa makaa hayo.
Amesema mashine (excavator) za Caspian ambazo zina uwezo pc 800 walikubaliana zitazalisha BCM 350 hadi 400 kwa saa lakini mashine hizo zikawa na uwezo wa kuzalisha BCM 170 hadi 200 kwa saa huku zikitumia lita 75 hadi 80 za dizeli kwa muda huo.
Neno pc ni kiwakilishi cha uzito wa mashine au mtambo huo, hivyo inaposemwa pc 800, maana yake ni uzito wa tani 80 kwa kuwa unachukua namba mbili za mwanzo.
Seti ya excavator inajumuisha magari (truks) yanayobeba mkaa ghafi ambao bado haujachenjuliwa, mashine aina ya Dozer, mashine ya mwanga na greda ambavyo hivyo vyote vinategemeana.
“Kwa mfano unapokuwa na mashine ya ukubwa wa hiyo ya Caspian lazima uiendeshe na truck nne, lakini inapokuwa haifikii malengo ina maana itafanya kazi na truck tatu, wewe tayari umelipia nne, hivyo inakulazimu ukodi mashine nyingine ili iweze kuendesha iliyobaki, jambo ambalo linaongeza gharama za uendeshaji.
Amesema kitaalamu ili upate mkaa tani moja ambayo ni sawa na kilo 1,000 lazima uzalishe BCM 6. BCM (Bank Cubic Meter) ni neno la kitaalamu ambalo tafsiri yake ni tabaka la mkaa ambalo lina udongo na mawe yaliyofunika mkaa lakini pia neno hilo halina tofauti na neno mita za ujazo, hivyo ukichimba na kutoa matabaka sita kisha kuchakata ndipo unapata tani moja.
“Kwenye mgodi kuna kiwango cha uchafu kiitwacho kitaalamu ‘stripping ratio’ (waste material/overburden) gawia mali uichimbayo ambapo kwao ni mkaa, hivyo kiwango chao cha kugawa kwenye kampuni yao wameweka 6,” amesema Mwanga.
Hivyo amesema wamekubaliana na Caspian inayokodisha vifaa vya uchimbaji kuvunja mkataba baada ya kukaa mezani kutokana na mashine zao kutumia gharama kubwa za uzalishaji makaa ya mawe tofauti na matarajio yao.
Mwanga amesema uzalishaji huo ulikuwa mdogo ukilinganishwa na bei ya kuilipa mashine hiyo kwa saa dola za Marekani 110, kwani walipokuwa wanalinganisha na gharama za uendeshaji wanazozitumia Tancoal, kazi hiyo ilionekana inawanufaisha Caspian kwa asilimia 75.
Kwa hali hiyo amesema walifanya mlinganisho na kampuni zingine zinazokodisha mashine kwao wakabaini Caspian lazima waachane nao au wakubali kubadilisha mkataba ili kuwe na uwiano wa masilahi pande zote.
Amesema Kampuni ya Ramani wamekodisha mashine (excavator) nne ambapo mbili zikiwa na uwezo wa kuzalisha BCM 200 kwa saa na zinakodiwa kwa dola za Marekani 75 na zingine mbili 345D na 349D zenye uwezo wa kuzalisha BCM 250 zinazotumia mafuta ya dizeli lita 30 hadi 40 zinakodiwa kwa dola 85 na 90 za Marekani kwa saa.
Kampuni ya NAM wamekodisha mashine (excavator) 3 ambazo uwezo wake mbili aina ya Lib 944 zinazalisha BCM 200 kwa saa na zinakodiwa kwa dola 80 za Marekani kwa saa na wakati huo zinatumia mafuta ya dizeli lita 28 hadi 35 kwa saa.
Pia ile ya tatu yenye uwezo wa Lib 980 inazalisha BCM 380 hadi 450 kwa saa na inakodiwa kwa dola 130 kwa saa huku ikitumia mafuta ya dizeli lita 75 hadi 85 kwa saa.
Wakati kampuni ya EFFCO wana excavator tatu zenye uwezo wa pc 600 ambayo kwa sasa imeharibika lakini ilipokuwa nzima ilizalisha BCM 200 hadi 250 kwa saa na ilikodiwa kwa dola 75 kwa saa na ilitumia lita za mafuta ya dizeli 75 hadi 80 kwa saa.
Hitachi 870 inazalisha BCM 300 hadi 350 kwa saa na inakodiwa kwa dola 112 kwa saa huku ikitumia dizeli lita 75 hadi 80 kwa saa.
Pia ile ya tatu Hitachi 1200 inazalisha BCM 350 hadi 450 kwa saa na inatumia lita 100 hadi 115 za dizeli kwa saa huku bei yake ikiwa kati ya dola 145 hadi 155 kwa saa.
Wakati Kampuni ya Caspian ilikuwa na mashine zenye uwezo mkubwa “heavy duty” ambazo zina sifa ya kuzalisha BCM 250 hadi 400 kwa saa na kutumia mafuta lita 75 hadi 80 za dizeli kwa saa lakini zilikuwa zinazalisha BCM 175 hadi 200 kwa saa huku zikikodiwa kwa dola 110 kwa saa.
Amesema bei za mkaa aina ya Crushed kwa wateja wenye mkataba tani moja ni dola 45 na wale wasio na mkataba ni dola 50 wakati aina ya mkaa Cobbles na Peas kwa wenye mkataba ni dola 55 na wasio na mkataba ni dola 59.
Ukiangalia uwiano huo amesema ndipo utaona kwa nini walikuwa wanawaomba Caspian wazungumze ili hatimaye gharama zishuke ama wavunje mkataba kwa masilahi ya pande zote mbili.
Kwa saa 20 muda ambao mashine za Caspian zilikuwa zinafanya kazi zilizalisha BCM kati ya 3,500 na 4,000 ambazo ni makadirio kati ya tani 583 na 667 za makaa ya mawe.
Wakati wao kwa muda huo walitarajia kupata wastani wa tani kati ya 1,167 hadi 1,333 kwa uwiano wa kuzalisha BCM kati ya 7,000 hadi 8,000 kwa saa 20.
Amesema kiasi hicho cha makaa kilichozalishwa kilitumia mafuta ya dizeli kati ya lita 45,000 na 50,000 kwa saa 600 katika mwezi kwa gharama ya makadirio kati ya shilingi milioni 103.5 hadi 110.4.
Wakati mashine za EFFCO zina uwezo wa kuzalisha BCM 180,000 hadi 270,000 kwa saa 600 katika mwezi ambapo wanapata makadirio ya tani 30,000 hadi 45,000 za mkaa. Huku zikitumia mafuta lita 36,000 hadi 60,000 kwa mwezi kwa gharama ya makadirio kati ya shilingi milioni 82.8 hadi 138.
Mwanga amesema Tancoal kwa mwezi wanazalisha tani 70,000 za makaa ya mawe yenye makadirio ya thamani kati ya shilingi bilioni 7.245 hadi 8.855, ambapo mchango wa Caspian ulikuwa chini ya tani 20,000, makadirio kati ya shilingi bilioni 2.07 hadi 2.53.
Kwa mantiki hiyo mashine ya Caspian ilikuwa inalipwa dola za Marekani 66,000 kwa saa 600 za mwezi, makadirio ya shilingi za Tanzania milioni 151.8. Huku ikitumia lita za mafuta 45,000 hadi 48,000, makadirio ya gharama ya shilingi milioni 103.5 hadi 110.4 kwa saa 600 za mwezi.
Wakati Kampuni ya NAM kwa saa 600 za mwezi inalipwa dola 48,000 ambazo ni makadirio ya shilingi milioni 110.4 kwa wastani wa matumizi ya mafuta lita 16,800 hadi 21,000 kwa shilingi milioni 38.64 hadi 48.3.
Mwanga amesema Tancoal kwa mwezi wanazalisha tani 70,000 za makaa ya mawe yenye makadirio ya thamani kati ya shilingi bilioni 7.245 na 8.855, ambapo mchango wa Caspian ulikuwa tani 20,000, makadirio kati ya shilingi bilioni 2.07 na 2.530.
Caspian imekuwa na makadirio ya kufanya kazi saa 600 kwa gharama ya dola 110 kwa saa, na walikuwa wanapata makadirio ya malipo ya shilingi milioni 151.8 kwa saa 600, wakati kwa muda huo huo na uzalishaji unaofanana, NAM walilipwa shilingi milioni 110.4, ambayo ni tofauti ya shilingi milioni 41.4.
Amesema mashine ya Hitachi 1200 ina uwezo wa kuzalisha BCM 400 kwa saa na inafanya kazi saa 10 tu inatoa BCM 4,000, makadirio ya tani 667 za mkaa kwa gharama ndogo na uzalishaji mkubwa.
Hivyo si kweli uzalishaji wa makaa umeshuka kwani kiwango kinachozalishwa baada ya Caspian kuhamisha vifaa vyake vyote ni kile kile na kuanzia kiangazi mwaka huu amesema watapandisha uzalishaji kutoka tani 70,000 hadi 100,000 kwa mwezi.
Hivi sasa kwa mwezi wanauza tani 65,000 hadi 70,000 kwa bei ya tani moja dola 45, mkaa wenye ukubwa wa milimita 0 hadi 75, unaoitwa kitaalamu “Crushed coal”, bei ambayo wanauziwa wenye mkataba lakini kwa wasio na mkataba ni dola 50 kwa tani, makadirio ya shilingi 103,500 hadi 115,000.
Wakati kwa aina ya mkaa wenye ukubwa wa milimita (mm) 30 hadi 75 ambayo kitaalamu unaitwa “Cobbles and pease coal” bei wanayouziwa wenye mkataba kwa tani moja ni dola 55 na wasio na mkataba ni dola 59, kiasi ambacho ni makadirio ya shilingi 126,500 hadi 135,700 kwa tani moja ya mkaa.
Amesema kiasi hicho cha mkaa kinachozalishwa kwa mwezi kinaweza kubebwa na malori yenye uzito wa tani 30, makadirio ya malori 2,333.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji Tancoal Taifa, James Shedd, yamekuwapo makubaliano na Kampuni ya Caspian kuvunja mkataba baada ya majadiliano na mmiliki wa kampuni hiyo, Rostam Azizi.
Shedd amesema katika kikao hicho walikubaliana kwamba madai ya asilimia 100 wanayodaiwa na Caspian walipe asilimia 75 ya madai zaidi ya dola milioni 10 kwa kuwa uzalishaji wa makaa hayo kwa kutumia mashine zao ulikuwa tofauti na matarajio, kwa sababu si za kisasa, zimechoka na umri wake ni zaidi ya miaka 25 na ndiyo maana zinatumia mafuta mengi na uzalishaji mdogo.
Hivyo amesema katika malipo ya awali, baada ya makubaliano wamekwisha kutoa dola milioni mbili kati ya dola milioni nane walizokubaliana kulipa, makadirio ya zaidi ya shilingi bilioni 4.6 za Tanzania.
Imeelezwa na Shedd kwamba kiasi cha fedha kilichobaki dola milioni sita za Marekani makadirio ya shilingi bilioni 13.8 zitakuwa zinalipwa kila mwezi kwa muda wa miezi minane na mwisho ni Desemba 31, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Caspian, Akhram Azizi, kampuni yake imevunja mkataba na Tancoal kwa sababu za kutoelewana. Mkataba huo ulikuwa wa miaka mitatu lakini kwa miaka miwili walikuwa hawalipwi.
Azizi amesema pamoja na kodi ya mapato walikuwa wanawadai kama dola zaidi ya milioni 11, kwa hiyo, kutokana na maelewano hayo wakalazimika kupata ufumbuzi ambao ni kuvunja mkataba Aprili 30, mwaka huu.
Amesema: “Chanzo kikuu cha tatizo hilo ni kwamba walisaini mkataba kwa tozo ya mashine kwa saa, halafu baadaye wakasema bei zetu zipo juu, sasa inakuwaje walalamike tena kwamba bei ipo juu wakati wamesaini mkataba?
“Baada ya kuona hivyo tukaona bora kufungua kesi Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara kwa kuwa tumemalizana na Tancoal,” amesema Mkurugenzi Azizi.
Amesema wao walikodisha mashine 15 ambazo tayari wamezitoa zote na kwamba suala la kuvunja mkataba wao wamelipokea kwa mikono miwili, kwa sababu wasingeweza kufanya kazi kwa miaka miwili bila kulipwa wakati kwa upande wao wanalipa mishahara kila mwisho wa mwezi na kutengeneza mashine kwa gharama kati ya shilingi milioni 500 hadi 600 kwa mwezi.
Amesema kampuni yake ina uzoefu mkubwa wa masuala ya uchimbaji wa madini kwa miaka mingi, kwa mfano Mwadui wapo tangu mwaka 1998 hadi sasa, na huko Ngaka waliingia baada ya Tancoal kushindwa kuendelea na uzalishaji.
Amesema kuondoa mashine zote hizo na ujuzi walionao kutaathiri uzalishaji wa mkaa kwa kiasi kikubwa, kwa kuwa uzalishaji si mashine peke yake, bali ujuzi ndio msingi wa mafanikio.
Kuhusu suala la kudorora kwa uzalishaji amesema hana taarifa lakini kwa siku zijazo uzalishaji wa mkaa utaendelea kudorora kwa sababu mashine nyingi zimeondolewa.
“Ukiangalia kabla ya sisi kuingia uzalishaji ulikuwa mbovu sana na ndiyo maana walikuja kutaka msaada wetu na mashine zetu na watu wetu kwenda kusaidia uzalishaji, lakini madhali sisi hatupo tena inatakiwa wao wenyewe wajizatiti kuongeza uzalishaji na kulitosheleza soko,” amesema Azizi.
Amesema, kinyume cha hapo, viwanda vya ndani vitaathirika na gharama za uendeshaji zitapanda.
Kuhusu mashine zake kuwa na uwezo mdogo wa kuzalisha makaa, amesema si kweli kwa kuwa hata unapochumbia, ukaoa halafu mke ukamchoka, utamzushia mambo mengi sana ili umuache.
Japo ni kweli amekiri mashine zao si mpya, lakini zina hali nzuri na ndiyo maana katika kipindi chote cha miaka miwili mashine zilifanya kazi kwa asilimia 75 hadi 80 na hapakuwa na ubovu wa mashine hata siku moja.
Hata ukiangalia kwenye kiwango cha uzalishaji tangu wameingia hadi wametoka, uzalishaji umepanda kwa kiasi kikubwa na hiyo ni kwa sababu mashine ilizalisha kwa asilimia 85, kwa hiyo suala la kusema mashine zao ni za zamani si la msingi, kwa kuwa katika mkataba wao hakuna sehemu waliyoandikiana kuwa mashine zinazokodishwa ziwe mpya.
Amesema ili kuhitimisha jambo hilo wamepunguza deni kwa kuwaondolea asilimia 25 ya deni la dola milioni 11 pamoja na kodi ya mapato (VAT), kiasi hicho ni sawa na shilingi bilioni 25.3 na kuwataka walipe dola milioni nane, takriban shilingi bilioni 18.4 za Tanzania.
Kwa upande wake, Meneja Viwango na Mauzo Tancoal, Bosco Mabena, amesema hivi sasa wanapata wateja wengi wa ndani na nje ya nchi, kwa kuwa mkaa unaozalishwa na Tancoal mgodi wa Ngaka una ubora unaozingatia viwango vya kimataifa.
Kwa joto la mkaa lisilopungua 5,800 hadi 6,500 ambapo kipimo cha kitaalamu hujulikana kwa jina la ‘Kilo calories per kilogram’, kwa sababu unadhibitiwa kuanzia kwenye uchimbaji hadi uchakataji kwa kutumia maabara yao iliyopo mgodini hapo. Amesema uvumi unaovumishwa kuwa Tancoal mkaa wao hauna viwango ndiyo maana wateja wanakimbia, si kweli.
Amesisitiza kuwa wateja wamekuwa wakiongezeka, na kwamba ongezeko hilo ni kutoka viwanda 10 hadi 29 vya ndani, na vya nje kutoka vinne hadi tisa vya nchi za Kenya, Uganda na Rwanda.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Juma Mnwele, amesema taarifa ya Kampuni ya Caspian kuondoa vifaa vyao baada ya kuvunja mkataba na Tancoal anayo lakini shughuli za uzalishaji wa mkaa zinaendelea.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Mbinga amesema anayo taarifa ya kuvunjika kwa mkataba baina ya kampuni hizo, lakini wanatarajia kupata kampuni mpya tatu; Marketing Insights, Ruvuma Coal Mining na Mbuyula Coal Mining ambazo zitaanzisha machimbo mapya mwaka huu, ingawa moja kati ya kampuni hizo, Mbuyula Coal Mining, imeanza kazi katika Kijiji cha Mtunduwalo, wilayani humo.