Serikali ya Canada imetangaza vikwazo vya kiuchumi na kisiasa dhidi ya Rwanda, ikisema vikosi vyake vinasaidia kundi la M23 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Canada ilikosoa mauaji na mashambulizi dhidi ya raia, wakimbizi, na vikosi vya Umoja wa Mataifa katika Mashariki mwa DRC.
Vikwazo vya Canada vinajumuisha kusitisha huduma za teknolojia na ushirikiano wa kibiashara na Rwanda.
Rwanda imejibu kwa kusema kuwa Canada inashindwa kuhusisha DRC na mashambulizi dhidi ya raia wa kabila la Banyamulenge, na kudai hatua za Canada hazitasuluhisha mzozo.
Canada inachukua hatua hii baada ya Ubelgiji, Uingereza na Marekani kumuwekea vikwazo Jenerali James Kabarebe wa Rwanda, ambaye anahusishwa na msaada kwa M23.
Rwanda inakanusha kutuma wanajeshi wake, ikisema inalinda mipaka yake dhidi ya vikosi vya DRC na kundi la waasi la FDLR.
