Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw. Charles Kichere amepongeza kasi ya ujenzi wa uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato wenye ukubwa wa hekta 4,500 ( hekari 11000).

CAG Kichere ametoa pongezi hizo leo tarehe 4 Februari 2025 wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja cha ndege wa Msalato jijini Dodoma.

Katika ziara hiyo ambayo aliambatana na maafisa kutoka ofisi ya CAG amempongeza Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania-TANROADS Mhandisi Mohamed Besta, pamoja na wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa uwanja huo wa Msalato ambapo amesema kuwa muda mwingi hutumika akiwa ofisini kusoma ripoti za miradi pasipo kujionea mambo makubwa yayofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Katika ripoti zetu za ukaguzi tunasoma lakini ni vyema kuja kama hivi kujionea ni kitu gani kinachoendelea eneo la mradi, kwahiyo tumeona nini kimetokea” amekaririwa CAG Kichere.

Bw. Kichere amehimiza wakandarasi wa mradi huo kufanya kazi usiku na mchana ili kukanilisha mradi huo kwa wakati unaotakiwa ambapo pia ametoa wito kwa wananchi kutovamia maeneo hayo ya uwanja kwani ni alama ya mkoa wa Dodoma na Taifa kwa ujumla wake.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania-TANROADS Mhandisi Mohamed Besta amesema kuwa uwanja huu utakamilika rasmi mwezi Novemba 2025 na kuanza kutumika ifikapo Julai 2025.

Mhandisi Besta amesisitiza kuwa wananchi wanautazama uwanja huo kama sehemu ya uwekezaji nchini hivyo kasi ya ujenzi itaendelea ili ukamilike kwa wakati.

Naye Msimamizi wa mradi Mhandisi Kendrick Chawe amesema kuwa uwezo wa uwanja huo kiteknolojia na ufanisi wa maegesho ya ndege una uwezo wa kuchukua ndege 17 kwa wakati mmoja ” Parking space zipo za kutosha, hivyo unaweza kupokea ndege 17 kwa wakati moja” Amekaririwa

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato unatakuwa kiungo muhimu cha usafiri wa anga nchini Tanzania, Afrika Mashariki na Ulimwengu kwa ujumla wake ambao utachochea maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kuimarisha nafasi ya Tanzania kimataifa.