Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Charles Kichere ameipongeza Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake.

Bw. Kichere ametoa pongezi hizo wakati alipotembelea banda la PPAA katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Huduma ya Sheria PPAA, Bi. Agnes Sayi akiongea kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa PPAA Bw. James Sando memueleza CAG kuwa Sheria mpya ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 imeboresha masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja kupunguzwa kwa muda wa kushughulikia malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya Ununuzi wa Umma kutoka siku 45 hadi siku 40.

“Mabadiliko ya Sheria ya Ununuzi yamekuwa yakifanyika mara kwa mara kwa lengo la kupunguza muda, kuongeza uwazi na usawa katika shughuli za ununuzi wa umma, kuongeza ushindani,” alisema Bi. Sayi

Kadhalika Bi. Sayi ameongeza kuwa PPAA imefanikiwa kuanzisha Moduli ya kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia kieletroniki ambapo moduli hiyo ipo katika mfumo wa ununuzi wa umma kieletroniki (NeST) ambapo kupitia moduli hiyo wazabuni wataawasilisha malalamiko yao kieletroniki jambo ambalo litasaidia kuokoa muda na gharama.