Kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF), imetupilia mbali malalamiko ya timu ya taifa ya Guinea dhidi ya Taifa Stars ya Tanzania, yaliyowasilishwa na Shirikisho la Mpira la Guinea kuhusu uhalali wa mchezaji wa Tanzania, Mohammed Ame.

Taarifa iliyotolewa cha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), inaeleza kuwa, kwenye malalamiko hayo Guinea ilihoji uhalali wa mchezaji huyo kwa madai kuwa namba yake ya jezi aliyovaa, haikuwepo kwenye orodha ya wachezaji iliyowasilishwa kwa ajili ya mchezo huo.

Kutokana na uamuzi huo wa kamati ya nidhamu, matokeo ya mchezo huo mamba 143 yanabaki kama yalivyo na safari ya Tanzania kuelekea michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) inabaki pale pale.

Mchezo huo ulimalizika kwa Taifa Stars kuibuka na ushindi wa bao 1-0 mwezi Novemba, na kufuzu kwenye michuano ya AFCON, nchini Morocco, itakayofanyika Desemba mwakani.