Karne ya 21 ina mambo mengi yanayogonga vichwa vya habari duniani, achana na kifo cha Rais wa 41 wa Marekani, George H.W. Bush, ambaye mazishi yake yamefanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Achana na habari ya Bernard Membe na CCM yake, sahau kuhusu kipigo cha mbwa koko ambacho Simba SC wamewachapa Mbambane Swallows ya Swaziland na kuwasukuma nje ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika kwa jumla ya mabao 8-1. Simba sasa watakuwa wageni wa Nkana FC ya nchini Zambia mwishoni mwa wiki hii.
Unajiuliza kuhusu Mtibwa Sugar kuweza kuvuka kucheza raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya kuwabamiza Northern Dynamo ya Seychelles kwa mabao 5-0, ambapo katika Dimba la Azam Complex, Chamazi walishinda magoli 4-0, na katika mchezo wa marudiano uliofanyika nchini Seychelles wenyeji walilala kwa bao 1-0. Sasa Mtibwa watakuwa wageni wa Kampala City ya nchini Uganda mwishoni mwa wiki hii.
Kipigo walichokitoa Mtibwa Sugar sasa kinawashtua vigogo wa soka barani Afrika kama vile TP Mazembe, Etoile du Sahel, Al Ahly na wengine.
Achana pia na kuachiwa huru viongozi wakubwa wa upinzani nchini Rwanda, Diane Rwigara na mama yake, Adeline, ambao walikuwa wakishutumiwa kwa kosa la kufanya uchochezi dhidi ya serikali ya Rais Kagame.
Habari kubwa zaidi ni ile ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), chini ya Rais wake, Ahmad Ahmad, kukiomba Chama cha Mpira wa Miguu nchini Afrika Kusini (SAFA) kuandaa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani baada ya Cameroon kupokwa nafasi hiyo.
CAF wameiomba SAFA kuandaa michuano hiyo baada ya nchi ya Cameroon ambao ndio walitakiwa kuwa wenyeji wa michuano hiyo kushindwa kujiandaa kwa wakati.
Rais wa SAFA, Danny Jordaan, kimsingi amekubali nchi yake kuwa mwenyeji wa mashindano hayo lakini hana mamlaka ya moja kwa moja kuidhinisha suala hilo, hivyo amelipeleka kwa viongozi wakubwa wa nchi ili kutoa uamuzi kuhusu kuwa wenyeji wa mashindano hayo makubwa barani Afrika.
Mashindano ya AFCON yaliyopita yalitakiwa kufanyika nchini Morocco, lakini mashindano hayo hayakufanyika nchini humo kwa kwa kile kilichoelezwa ni kuogopa maambukizi ya ugonjwa wa Ebola.
Baada ya Morocco kujiondoa, nchi ya Gabon ilichaguliwa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo, ambapo timu ya taifa ya Cameroon (Simba Wasiofugika) ilitwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kuitandika Misri mabao 2-1.
Mashindano yajayo ya AFCON (2019) yanatarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza kati ya Juni 15 hadi Julai 13, 2019 badala ya Januari/Februari kama ilivyozoeleka.
Ikumbukwe Afrika Kusini ndiyo nchi pekee barani Afrika iliyopata fursa ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2010. Afrika Kusini inatajwa kuwa nchi pekee barani Afrika kuwa na viwanja vizuri vya kuchezea soka.