Watu 300 wanahofiwa kufariki dunia baada ya bwawa la maji kuvunja kingo zake katika mgodi wa kampuni ya chuma kusini mashariki mwa Brazil.
Maji yaliyochanganyika na matope yaliwafunika mamia ya wafanyakazi wa shirika hilo.
Shughuli ya kuwatafuta walionusurika inaendelea karibu na mji wa Brumadinho, katika Jimbo la Minas Gerais.
Gavana wa jimbo hilo, Romeu Zema, amesema kuna hofu huenda watu wengi wamefariki dunia katika mkasa huo. Hadi tunakwenda mitamboni, watu 27 walikuwa wamethibika kufariki dunia, huku wengine karibu 300 wakiwa hawajulikani walipo.
Baadhi ya watu waliokwama kwenye matope waliokolewa kwa kutumia helikopta baada ya barabara kuharibika. Watu wengine wamehamishiwa kutoka katika makazi yao kutokana na sababu za kiusalama.
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya uchimbaji madini ya Vale, Fabio Schvartsman, theluthi moja ya wafanyakazi karibu 300 hawajulikani waliko.
“Nina hofu nataka kujua hali ni mbaya kiasi gani,” amesema Helton Pereira, mmoja wa jamaa za watu walioathiriwa na mkasa huo aliyezungumza na BBC nje ya Hospitali ya Belo Horizonte.
Amesema mke wake na dada yake wote hawajulikani waliko kwa sababu walikuwa wanaendesha biashara ya chakula karibu na eneo la tukio.
Shughuli ya kuwatafuta manusura inafanywa na maofisa 100 wa Jeshi la Zimamoto na Dharura, huku wengine zaidi wakitarajiwa kupelekwa katika eneo hilo.
“Kuanzia sasa matumaini ya kuwapata walio hai haupo. Pengine tutoe miili iliyokwama kwenye matope,” amesema Gavana Romeu Zema wa Jimbo la Minas Gerais.