Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Rufiji
Mgawo wa umeme uliolisumbua taifa kwa muda mrefu sasa unafikia ukomo baada ya Bwawa la Mwalimu Nyerere kuanza kuzalisha umeme kwa kuingiza kwenye gridi ya taifa megawati 235 mwezi huu, JAMHURI linathibitisha.
Kuanzia Febaruari 22, 2024 mtambo namba 9 umeanza kuzalisha umeme na JAMHURI linafahamu kuwa kama kila kitu kitakwenda kama ilivyopangwa, mtambo namba 8 nao utaanza kuzalisha umeme na kuingiza megawati 235 nyingine kwenye gridi ya taifa, hivyo kuongeza jumla ya megawati 470 mpya kwa mpigo kwenye gridi ya taifa.
Kwa sasa nchi inahangaishwa na mgawo, hali inayowafanya Watanzania kudai kuwa kuna hujuma kwa baadhi ya viongozi kutaka kuuza majenereta, lakini lawama na tuhuma hizo sasa zinaelekea ukingoni baada ya mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambao ukikamilika utazalisha megawati 2,115 kuanza kufanya kazi.
Jumapili Februari 25, 2024 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, akiwa kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere aliwaambia wahariri na waandishi wa habari kuwa kuanzia Februari 22, 2024 mtambo wa kwanza kati ya mitambo 9 umeanza kuzalisha umeme katika Bwalwa hilo la Mwalimu Nyerere linalogharimu Sh trilioni 6.5 kulijenga.
“Upungufu kwa Jumapili [kama] leo unakuwa megawati 200. Upungufu kwenye high pick (wakati wa matumizi makubwa) ni megawati 400… Tumefanikiwa kuingiza kwenye gridi megawati 235 siku 3 kabla ya siku iliyokuwa imepangwa. Kufikia mwezi wa tatu Mungu akipenda tutaingiza jumla megawati 470, tutakuwa na megawati za ziada zaidi ya 70. Baada ya mwezi wa tatu hatutazungumza upungufu wa umeme tena,” amesema Dk. Biteko.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, Mhandisi Mkazi, Injinia Lutengano Mwandambo, amesema kufikia mwishoni mwa Januari 2024, ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ulikuwa umefikia asilimia 96.28. Amesema hadi Jumapili ujazo wa maji ulifikia mita za mraba 180 na kwa bwawa kuzalisha umeme megawati zote 2,115 ujazo unapaswa kufikia mita 184, hivyo bado mita 4 tu.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Biteko, alipoulizwa juu ya taarifa zilizosambaa mtandaoni kuwa wahandisi wamekataa kuanza kuzalisha umeme kabla ya maji kufikia ujazo, amesema: “Huku mitandaoni kuna mambo mengi. Kuna kiu kubwa ya watu kutamani jambo likwame. Mimi naona awepo mwingine wa kusema na mwingine wa kutenda. Mimi sijapanga kabisa kuwa maarufu hapa nchini kwa kusema [kujibizana na watu],” amesema Dk. Biteko.
Amesema wakati watu wakidai imeshindikana kuwasha umeme, sasa mtambo wa kwanza umewashwa na megawati 235 zimeingia kwenye gridi ya taifa, hivyo yeye na watendaji wa wizara wanajibu watu kwa vitendo badala ya maneno.
Dk. Biteko amesema hadi sasa nchi ina vyanzo vinavyozalisha umeme megawati 1,935, ila kutokana na wingi wa viwanda vilivyoanzishwa nchini umeme uliopo hautoshi. Ameongeza kuwa mwaka 2012 hadi 2015 kulikuwapo tatizo kubwa la umeme nchini, hali iliyoilazimu nchi kukodisha mitambo inayotoza capacity charge, hivyo kuigharimu nchi fedha nyingi.
“Miaka mitano iliyopita hatukuwa na shida ya umeme. Sasa hivi tuna mgawo wa umeme. Mwaka 2012 hadi 2015 kulikuwa na upungufu wa umeme kwenye nchi. Serikali ikajenga bomba la gesi kutoka Mtwara na 2015 likafika Dar es Salaam. 2015 tukaingiza megawati 150 za mtambo wa gesi.
“Mwaka 2016 tukawa na ziada ya megawati 300 kwa kutumia gesi. Usingekuwa na mgawo kwa vyovyote vile, ila vyanzo vikabaki vilevile, uchumi unakua. Mahitaji yanaongezeka, miji inaongezeka, mkuu wa Mkoa wa Pwani amesema kuna viwanda vipya 30 na 17 vinajengwa. REA inapeleka umeme vijijini ambapo wachomeleaji sasa wanachomea huko huko vijijini. Migodi mipya inajengwa ambayo mgodi unatumia hadi megawati 8 sawa na Mkoa wa Manyara, ni lazima umeme upungue,” amesema Dk. Biteko.
Amesema hata baada ya umeme wa Bwawa la Nyerere kuingia kwenye gridi ya taifa, inabidi serikali ianze kuendeleza vyanzo vipya kwani bila kufanya hivyo, hii starehe ya umeme utakaopatikana kufikia miaka 15 nchi itakuwa na tatizo la umeme. Ametaja miradi inayolengwa kujengwa kuwa ni pamoja na wa Mtwara megawati 1,000, Somanga Fungu megawati 1,600 na mingine.
Pia wizara yake inalenga kujenga bomba la kusafirisha gesi kwenda Zambia na Uganda, ambayo yatasaidia kuzalisha umeme katika maeneo mbalimbali ya nchi yanapopitia mabomba hayo. Vyanzo vingine wanaangalia jotoardhi kama Kenya umeme wao mwingi unavyotokana na jotoardhi.
“Sisi tunazo reserve nyingi kuliko wao, tunaelekea huko. Ifikapo 2035, tuwe tumepata megawati 10,000. Baada ya Julius Nyerere itakuwa tumeongeza hadi [megawati] 4,000,” amesema.
Amesema tangu mwaka 2016 vyanzo vimebaki kuwa vilevile na kwa kulifahamu hilo ndiyo maana mwaka 2018 serikali ilifanya uamuzi wa kuanza kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere, ila Uviko – 19 ikachelewesha mradi huo kumalizika kwa wakati.
“Bwawa la Mwalimu Nyerere ni holiday ya miaka 15, baada ya hapo tutarejea hapa. Ni lazima sasa tujenge miradi kama Rumakali, Ruhuji, Kakono na vyanzo vingine vingi,” amesema Dk. Biteko na kuongeza kuwa Rais Samia anataka kutatua tatizo la umeme milele. “Mheshimiwa Rais haangalii matatizo ya umeme kwenye kipindi cha utawala wake, anaangalia beyond 2030 au 40 years to come. Tuangalie miaka 30 au 40 ijayo tusiwe na tatizo lolote,” amesisitiza.
Amesema kwa sasa serikali inashindwa kuzima mitambo ya Mtera, Kidatu na Hale kuifanyia matengenezo kwani ikiizima kutakuwapo upungufu mkubwa wa umeme na hali hii itawapa Watanzania mtanziko mkubwa, suala ambalo asingependa litokee, hapo mitambo hiyo ilipaswa kufanyiwa matengenezo zaidi ya miaka mitatu iliyopita.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema mkoa huo una viwanda 1,533, ambapo kati yake viwanda 120 ni viwanda vikubwa, 124 vya kati na vilivyobaki ni vidogo. “Viwanda vikubwa vilivyokamilika na kuanza kazi ndani ya mwaka ni 30. Viwanda 7 vimekua kutoka viwanda vya kati na kuwa viwanda vikubwa. Viwanda 17 vikubwa vipo katika hatua ya ujenzi. Rais alisema mkoa huu upate nishati ya kutosha kwa maana ya maji na gesi,” amesema Kunenge.
Pwani ilikuwa na upungufu wa megawati 70 kati ya 130 inazotumia, ila kutokana na mtambo mmoja wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kuwashwa hadi jana ilikuwa imebaki na upungufu wa megawati 15 pekee, ambazo nazo ilielezwa kuwa zitapatikana ndani ya muda mfupi.
Bwawa la Mwalimu Nyerere kuanza kuzalisha umeme inathibitisha kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa kupitia kaulimbiu yake ya “Kazi Iendelee” kuwa ataendeleza mazuri yote yaliyoanzishwa na watangulizi wake likiwamo hili Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo alilikuta katika asilimia 33 na sasa lipo zaidi ya asilimia 96.28 na limeanza kuzalisha umeme.
Maeneo manane ya ujenzi wa mradi
Mradi huu umejengwa katika maeneo manane hadi uanze kuzalisha umeme kama ifuatavyo:- 1. Kazi za kuchepusha mto (Diversion works), 2. Tuta Kuu (Main Dam), 3. Njia za maji ya kuendesha mitambo (Power Waterways), 4. Jengo na mitambo (Powerhouse), 5. Kituo cha kusafirisha umeme (Switchyard), 6. Matuta madogo (Saddle Dams), 7. Makazi ya kudumu (Operation Village) na 8. Barabara na daraja la kudumu (Permanent Roads & Bridge).
Bwawa hili lina mahandaki matatu yenye urefu wa mita 12 kwa 17 na njia tatu za kupitisha maji, ambayo mbele yanagawanyika na kuwa na mitambo tisa ya kuzalisha umeme. Kila mtambo utazalisha megawati 235, ambapo mitambo 9 kwa ujumla itazalisha megawati 2,115.
Kwa upande wa tuta la Bwawa la Nyerere kwenye kitako chini ukuta una upana wa mita 100 na ukuta huo unakwenda unapungua hadi juu ambako una upana wa mita 10. Ukuta wa tuta una urefu wa mita 190 kutoka usawa wa bahari. Juu ya ukuta huu wa bwawa hili itakuwapo barabara inayopitisha magari.
Mito inayojaza maji kwenye bwawa
Mito kutoka mikoa 11 inajaza maji katika Bwawa la Mwalimu Nyerere. Mito mikubwa mitatu inayojaza maji kwenye Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere inaanzia katika mikoa 10. Mito hiyo ambayo ni Ruaha, Kilombero na Luwengu, inakusanya vijito kutoka mikoa ya Tabora, Singida, Dodoma, Iringa, Mbeya, Morogoro, Pwani, Ruvuma, Dar es Salaam na Njombe. Mito kutoka mikoa hii yote inamwaga maji katika Bonde la Mto Ruvu.
Wataalamu wanasema kutokana na sababu hii, Bwawa la Mwalimu Nyerere halitakaukiwa maji kwa urahisi kama ilivyo kwa Bwawa la Mtera ambalo kwa mwaka 2022 pamoja na ukame, uzalishaji wa umeme ulipungua kwa megawati 5 tu, ikilinganishwa na Kihansi iliyopoteza megawati 153. “Hii ni kwa sababu bwawa hili litakuwa linakusanya maji, halitiririshi kama mto,” amesema mtaalamu.
Bwawa hili linalokadiriwa kudumu kwa miaka 100 na zaidi, limeleta faida kubwa nchini. Saruji yote inayojenga Bwawa la Nyerere ambayo ni tani 850,000, nondo tani 70,000 na udongo maalumu tani 250,000, ajira 12,298 vyote hivi vimekuwa vya manufaa kwa Tanzania.
Ujazo wa bwawa
Bwawa hili lenye urefu wa kilomita 100 kutoka ncha moja kwenda nyingine na ukubwa sawa na nusu ya Mkoa wa Dar es Salaam, litajaza maji wastani wa lita za ujazo bilioni 33.2.
Bwawa la Mwalimu Nyerere utafiti unaonyesha kuwa bwawa hilo halina uwezekano wa kujaa tope kama walivyokuwa wakidai wanaharakati wa mazingira, kwa Afisa Mwandamizi kusema: “Utafiti umeonyesha kuwa ndani ya miaka 100 ijayo bwawa linaweza kuwa na tope wastani wa asilimia 0.92. Hiki ni kiwango kidogo sana.”
Baada ya kusaini mkataba makandarasi walianza kazi ya kutengeneza miundombinu wezeshi, ikiwemo barabara, maji, umeme na reli kwa ajili ya kubebea mizigo ya kwenda eneo la mradi. Mwaka wa kwanza walifanya kazi ya kuchepusha maji ambapo mtaro (tunnel) ulijengwa na kuuhamisha njia mto wote kuruhusu ujenzi wa tuta kwenye kitanda cha mto.
Kwa sasa ujenzi wa mradi unaelekea ukingoni kwa kuanza uzalishaji, tayari umekamilisha ujenzi wa njia ya kusafirishia umeme kutoka kwenye mradi kwenda Chalinze mkoani Pwani na ambapo baada ya kufika Chalinze njia moja inakwenda Dar es Salaam na nyingine Dodoma ili kuwezesha umeme huo kusambazwa nchi nzima.
Uwekezaji huu mkubwa wa Sh trilioni 6.5 katika Bwawa la Nyerere unatokana na ukweli kwamba umeme wa maji ndio umeme rahisi kuliko umeme wowote hapa duniani. Gharama ya kuzalisha uniti moja ya umeme wa maji ni Sh 36 na baada ya muda mrefu gharama hizi hushuka, ilhali kwa sasa kupitia vyanzo mbalimbali Tanzania inazalisha uniti moja kwa wastani wa senti 10.7 za dola sawa na Sh 249 kwa uniti.
Misri inazalisha umeme kwa senti 4.6 za dola sawa na Sh 107, Afrika Kusini senti za dola 7.4 sawa na Sh 172, Ethiopia wanatumia maji senti za dola 2.4 sawa Sh 56 na India senti za dola 6.8 sawa na Sh 158.
Faida za Bwawa la Mwalimu Nyerere
Bwawa la Mwalimu Nyerere likikamilika litakuwa na manufaa mengi. Kati ya manufaa yanayotajwa ni kudhibiti mafuriko katika Bonde la Mto Rufiji. Kwa kawaida kabla ya ujenzi wa bwawa hili, maji kutoka mikoa hiyo 10 yalikuwa wakati wa masika yanakusanyika kwa wingi katika Mto Rufiji na kuleta adha kubwa ya mafuriko kwa wananchi.
Adha hiyo sasa itakwisha. Maji yatatoka kwa kiwango cha wastani wa lita milioni 2 kwa sekunde na kiwango hiki kitaendelea kutoka iwe wakati wa kiangazi au masika. Hii inatoa fursa kwa watu wanaoishi kwenye Bonde la Mto Rufiji kujipanga na maeneo yaliyokuwa yanafurika maji, sasa kupitia kilimo cha umwagiliaji wanaweza kulima mwaka mzima.
Pamoja na kwamba baadhi ya watu wanahoji umuhimu wa kuwekeza katika mradi mkubwa wa umeme wa maji wakiangalia mabadiliko ya tabianchi, ambapo ukame unazidi kuongezeka, mtaalamu anasema: “Umeme utakaozalishwa ni megawati 2,115. Kwa sasa tunatumia wastani wa megawati 1,500. Hivyo hata kikitokea kiangazi maji yakapungua kwa nusu, bado tutakuwa na megawati zaidi ya 1,000, hivyo hata ukitokea ukame Tanzania baada ya mradi huu haiwezi tena kurudi kwenye unyonge wa umeme.”
Ukiacha udhibiti wa mafuriko na kuongezeka kwa umeme kwenye gridi ya taifa, ongezeko hili la umeme linaongeza mapato ya TANESCO na serikali. Kuingia kwa megawati 2,115 ina maana mapato ya mauzo ya umeme ya TANESCO yanaongezeka mara mbili, hivyo kuongeza mapato ya shirika na serikali. Mradi huu pia utaongezea ufanisi kilimo cha umwagiliaji kwa wastani wa hekta 450,000. Mradi utaleta ulinzi bora wa mazingira.
Ukiacha sasa uhakika uliojitokeza kwa mazingira kutomomonyolewa na mafuriko, mainjinia Watanzania walioshiriki katika ujenzi wa mradi huu wamepata ujuzi mkubwa ambao nchi itaendelea kuutumia kwa kujenga miradi mingine ya mabwawa kama walivyofanya Misri kwa kujenga Aswan High Dam na Aswan Low Dam katika Mto Nile, yanayowapatia umeme kwa wastani wa megawati 2,370, kwa maana ya Aswan High Dam megawati 2,100 na Low Dam Megawati 270.
Kupitia Bwawa hili la Nyerere wanyama watapata maji ya kutosha, kutakuwapo uvuvi endelevu na utalii kama inavyofanyika kwa nchi nyingine zenye mabwawa ya kimkakati kama haya. Kuna dhana ya masuala la maendeleo ya jamii, ambapo umeme wa kutosha utasaidia maendeleo ya viwanda.
Mwezi Februari utabaki kuwa wa historia katika nchi hii kwani ile safari ya kufuta mgawo wa umeme hapa nchini inaanza rasmi. Ombi moja lililotolewa na watendaji wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ni wananchi kutunza mazingira kwa kuepuka kukata miti na kuchoma mkaa, suala linaloonekana kuwa janga kubwa kwa taifa hili, kwani miti inakatwa kwa kasi ya kutisha.